Vipaumbele vinane vya Serikali kuimarisha uwekezaji 2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza katika mkutano na wahariri na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Januari 10, 2024. Picha na Sunday George
Muktasari:
- Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 901, ikilinganishwa na miradi 526 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 71.3
Dar es Salaam. Wakati kiwango cha uwekezaji wa miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikiongezeka kwa asilimia 71.3 mwaka 2024 kutoka 2023, Serikali imetaja vipaumbele vinane vitakavyofanyiwa kazi kuimarisha uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini 2025.
Kwa mujibu wa TIC, mwaka 2023 ilisajili miradi 526 na 2024 idadi iliongezeka kufikia 901 ikiwa ni rekodi mpya ndani ya kituo hicho kutoka mwaka 2013 waliposajili miradi 885.
Akitaja vipaumbele vya Serikali kuboresha uwekezaji nchini 2025, Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza na waandishi na waandishi wa habari leo Januari 10 2025, amesema kutaanzishwa utaratibu wa kuzipima mamlaka za Serikali za mitaa katika kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji.
“Tutaanza kutekeleza ujenzi wa miundombinu katika maeneo maalumu ya kiuchumi ikiwamo Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone) ili kuwezesha ujenzi wa viwanda,” amesema.
Amesema watashirikiana na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) na kuanzisha utaratibu wa kuhamasisha uwekezaji kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na TIC kwa kushirikiana na mamlaka zingine za Serikali.
Pia, amesema watavutia miradi mipya 1,500 ya uwekezaji na mitaji ya Dola 15 bilioni za Marekani ifikapo Desemba 2025. Amesema sekta zilizopewa kipaumbele ni viwanda, kilimo, uchukuzi, nishati safi, utalii, madini na huduma.
“Ongezeko hili litaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi tano bora katika uwekezaji barani Afrika, hasa kwa wingi wa mitaji na utoaji wa huduma,” amesema.
Profesa Mkumbo ametaja kipaumbele kingine ni uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani kufikia asilimia 50 ya miradi yote ya uwekezaji kwa mwaka imilikiwe na Watanzania.
Amesema watashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali kuwalenga wawekezaji wa ndani hasa wadogo wanaokua.
“Tutaboresha na kuwezesha ofisi za sekretarieti za mikoa katika kuhudumia na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ngazi ya mikoa na wilaya nchini.
“Mwaka 2025, tutaanza na kufungua ofisi ya kanda ya TIC mkoani Njombe ili kusogeza huduma za uwekezaji Njombe, Iringa na Ruvuma,” amesema.
Profesa Mkumbo amesema mwaka 2025 watatunga muswada wa sheria mpya ya uwekezaji Tanzania utakaopendekeza kuunganisha TIC na Mamlaka ya Kusimamia Uzalishaji wa Bidhaa kwa Ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (EPZA).
Amesema Serikali itaandaa awamu ya pili ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Mkumbi).
Hatua hiyo amesema ni baada ya kufanyika tathmini ya utekelezaji wa Mkumbi iliyobaini mafanikio katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Ikiwa ni hatua ya kuondoa kero kwa wafanyabiashara, Profesa Mkumbo amesema Serikali itahakikisha taasisi za udhibiti zinakuwa chache.
“Kodi haijawahi kuwa rahisi kulipa lakini lazima tuweke mazingira mazuri ya kisheria, haiwezekani taasisi tisa kwa siku mmoja kufuata kodi kwenye biashara moja,” amesema.
Profesa Mkumbo akijibu swali kuhusu mikakati ya Serikali kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanakuwa endelevu pasipo kutegemea hisani ya kiongozi, amesema ni ngumu kutenganisha maendeleo yanayopatikana na utawala wa kiongozi aliyepo madarakani.
Amesema zipo sheria zinatungwa ili usimamizi wa miradi uwe endelevu.
Sababu uwekezaji kupaa 2024
Profesa Mkumbo amesema sababu ya kuimarika kwa uwekezaji nchini ni kutokana na kuimarishwa kwa mifumo ya kisera na sheria katika kuwezesha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji Tanzania.
Jambo lingine amesema ni kuimarishwa na kuboreshwa huduma kwa wawekezaji, akisema zipo taasisi 16 zinazotoa huduma katika kituo cha pamoja.
“Viongozi katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa, hususani wakuu wa mikoa, wameendelea kuhamasisha shughuli za uchumi na uwekezaji katika maeneo yao,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza katika uwekezaji, akisema miradi saba iliongoza kwa mitaji 2024.
Miradi hiyo amesema ni Hoteli ya Southern Sun, Kunduchi Mall, miradi 11 ya ujenzi wa majengo ya biashara Dar es Salaam eneo la Mikocheni na kiwanda cha samani kilichopo Kigamboni.
Pia, uwekezaji wa Kampuni ya Twiga Cement, uwekezaji wa kiwanda cha tumbaku na kampuni ya DP World.