Viongozi wanawake sekta ya afya watafanikisha malengo – Dk Haque

Mwenyekiti wa Bodi ya Kimataifa ya WomenLift Health, Dk Yasmin Ali Haque, akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano huo wa kimataifa ulioyakutanisha mataifa zaidi ya 40, ukijadili masuala ya uongozi kwa wanawake katika sekta ya afya.
Muktasari:
Wanawake wanapokuwa kwenye ngazi za maamuzi katika sekta ya afya, wametajwa kuingiza uzoefu, ubunifu na umahiri wao katika kuleta mabadiliko ya kudumu kwa lengo la kupata matokeo chanya
Dar es Salaam. Ili kufikia malengo ya kuwa na huduma bora za afya, dunia imetakiwa kuwapa kipaumbele wanawake katika uongozi, huku wanaume wakitakiwa kuwa mstari wa mbele kutekeleza takwa hilo.
Imeelezwa kuwa nchi zilizowapa kipaumbele wanawake katika uongozi wa sekta hiyo, zimefanikiwa kupiga hatua katika malengo yaliyowekwa kidunia baada ya kubadili mifumo ya uongozi kijinsia.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Aprili 8, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Kimataifa ya WomenLift Health, Dk Yasmin Ali Haque, wakati wa kuhitimisha mkutano huo wa kimataifa unaofadhiliwa na Bill and Melinda Gates ulioyakutanisha mataifa zaidi ya 40, ukijadili masuala ya uongozi kwa wanawake katika sekta ya afya.
Amesema dunia inahitaji wanawake waingie kwenye ngazi za uamuzi, lakini harakati za masuala ya haki za binadamu imekuwa kikwazo cha kupingana na hilo huku akisema sera pekee haitoshi bali muhimu ni utamaduni kubadilika.
“Wanawake wanapokuwa kwenye nafasi ya kuongoza wanaingiza uzoefu, ubunifu na umahiri wao katika kuleta mabadiliko ya kudumu kuleta matokeo chanya,” amesema.
Dk Haque amesema kuna faida nyingi zinazoonekana kwa kijamii, zinapowapa nafasi wanawake kuchukua nafasi za uongozi.
Amesema wanawake wanapoongoza familia, mashirika mbalimbali inaonyesha wazi namna uwezo wao kuwa mkubwa kutatua changamoto zilizopo, huku akisema mkutano huo unaikumbusha dunia kubadili hali iliyozoeleka katika mifumo ya kiuongozi.
“Viongozi wanaume lazima wawe sehemu ya haya mabadiliko na lisiwe jukumu la kuwaachia wanawake wawainue wanawake wenzao, wanaume wengi wamekuwa wakipigania ushiriki wa wanawake katika uongozi, hili la muhimu sababu wanao uwezo mkubwa kupigania wanawake,” amesema Dk Haque.
Akieleza alichojifunza katika uandaaji wa mkutano huo, Dk Haque amesema kila mwaka kumekuwa na upanukaji wa wigo wa ushiriki wa wanawake.
Amesema mwaka huu wamejifunza mengi zaidi yanayohitaji nguvu kubwa kuyashughulikia ikiwamo sera na siasa mahala pa kazi, usawa wa kijinsia, mabadiliko ya tabianchi na mengineyo.
Rais wa WomenLift Health, Amie Batson amesema majadiliano hayo ya siku tatu kila warsha inapofanyika yamekuwa chachu ya kukua na kuongezeka kwa viongozi wanawake katika sekta ya afya, pia kumekuwa na muunganiko mpya kwa ajili ya uongozi wa mwanamke kwa sekta hiyo.
“Miongoni mwa majadiliano tuliyoyafanya ni kuanzisha harakati za kidunia za kuchochea mabadiliko kwa wanawake wote, nimeguswa na dhamira kamili ya kuleta mabadiliko.
“Sasa ni wakati wa utekelezaji, tunatakiwa kuangalia zaidi katika kufanya kazi pamoja kuleta mabadiliko, tunatakiwa kuwa na uwajibikaji, maandalizi bora na malengo tuliyojiwekea. Kila mwanamke mwenye uwezo apewe nafasi, tusiwaache nyuma wanaume wawe washirika muhimu kama sehemu ya kutimiza malengo yetu,” amesema Batson.
Mwanzilishi wa WomenLift Health ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand, Hellen Clark ameelezea namna alivyopata wazo la kuanzisha mkutano huo unaowakutanisha wanawake viongozi katika sekta ya afya kote duniani.
“Nimefurahi kuona tuko zaidi ya viongozi wanawake 1000, nakumbuka mwaka 2016 tukiwa Nairobi meza tulizungukwa na wanaume, niliona kuna haja ya kufanya kwa Afrika kuinua wanawake. Ilikuwa ngumu, baada ya majadiliano nilienda kwa Bill and Melinda Gates wakasema vyovyote unavyoweza, niliwaambia nipeni rasilimali fedha.
“Kwa msaada wa Bill and Melinda Gates mwaka 2017 tukaanzisha huu mkutano, tulikuwa na watu 68 viongozi kutoka nchi za Afrika, wanawake walikuwa wachache na walisimulia uwepo wa upendeleo, ubaguzi kijinsia, malipo duni na walikuwa maono mapya katika uongozi,” amesimulia.
Clark amesema waliungana pamoja na kuanzisha kongamano hilo ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika jijini London na baadaye mwaka 2019 likafanyika Kigali, Rwanda na kukusanya watu zaidi ya 1000.
“Mkutano huu umesaidia kuongeza nguvu kwa wanawake katika uongozi wa sekta ya afya, kimataifa ingawaje kuanzia mwaka 2020 tulianza kufanya mtandaoni kutokana na Uviko19, hata hivyo WomenLift Health tulibaini kuwa nchi zilizoongozwa na wanawake zilifanya vizuri kwenye mapambano ya ugonjwa huo,” amesema Clark.
Mkutano huo uliofunguliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango Aprili 06, 2024 jijini Dar es Salaam umefungwa rasmi leo Jumatatu Aprili 8.