Vijana 500 wachaguliwa kujiunga Uhamiaji

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Anna Makakala.
Muktasari:
- Jeshi la Uhamiaji limewaita vijana 500 waliochaguliwa na kuwataka kuripoti katika Chuo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Dar es Salaam. Vijana 500 wamechaguliwa kujiunga na Jeshi la Uhamiaji na wametakiwa kuripoti Chuo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Vijana hao ambao wametakiwa kuripoti Jumatano ya Machi 1, 2023 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana watahitajika kubeba vifaa mbalimbali ikiwemo Sh60,000 ya godoro.
Mwanzoni mwa Desemba mwaka jana, Uhamiaji ilitangaza nafasi hizi huku ikieleza kuwa ajira hizo zitawahusu vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) walio kambini au nje ya kambi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, walioomba na kuchaguliwa kupitia Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, wanatakiwa kuripoti Ofisi Kuu Zanzibar Jumatano ya Februari 22, 2023.
“Atakayeripoti chuoni baada ya muda uliotajwa hatapokelewa,’ ilisisitiza taarifa hiyo.
Mahitaji na vifaa anavyotakiwa kwenda navyo kila mmoja mashuka manne yenye rangi ya bluu bahari, mto mmoja na foronya mbili rangi ya bluu bahari, chandarua cha duara cha rangi ya bluu bahari, madaftari makubwa 11, sanduku la chuma (trunker), ndoo mbili za plastiki (moja ya lita 20 na moja ya lita 10).
Fulana mbili za rangi ya dark blue zenye nembo ya Jeshi la Uhamiaji, Vifaa vya Usafi (Jembe na mpini wake, fyekeo, sururu, panga na shoka), nguo za michezo (tracksuit, bukta na raba), viatu vya mvua (rainboot), koti la mvua (raincoat).
“Nguo chache nadhifu na za heshima, kadi ya bima ya afya au Sh50,400 kwa wasio na bima, Sh20,000 kwa ajili ya upimaji afya, Sh60,000 ya kununua godoro na fedha za matumizi binafsi,” imeelezwa.
Taarifa hiyo inasema mahitaji na vifaa vilivyoainishwa vinapatikana katika duka la chuo huku gharama za usafiri kutoka nyumbani hadi chuoni zitagharamiwa na mhusika mwenyewe.
Aidha, kila mmoja ametakiwa kubeba vyeti halisi vya elimu ikiwemo kidato cha nne, cha sita, astashahada, stashahada, shahada, na vyeti vya ujuzi), cheti cha kuzaliwa, cheti cha JKT/JKU na Kitambulisho cha Taifa (Nida).
Majina ya waliochaguliwa kujiunga na Jeshi la Uhamiaji yanapatikana katika gazeti la Mwananchi leo 16, Febuari, 2023.