Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana 1,000 watuma maombi kulipiwa mahari

Muktasari:

  • Ikiwa zimepita siku nne tangu Taasisi ya Al- Hikma kutangaza nia ya kuwalipia mahari vijana 50 ambao wapo tayari kuoa, inaelezwa kuwa zaidi ya watu 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi wametuma maombi ya kuhitaji ufadhili huo hata kabla ya utaratibu rasmi kutangazwa.


Dar es Salaam. Ikiwa zimepita siku nne tangu Taasisi ya dini ya Kiislamu ya Al- Hikma kutangaza nia ya kuwalipia mahari vijana 50 ambao wapo tayari kuoa inaelezwa kuwa zaidi ya watu 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi wametuma maombi ya kuhitaji ufadhili huo hata kabla ya utaratibu rasmi kutangazwa.

Taasisi hiyo ilitangaza nia ya kuwalipia mahari vijana hao Aprili 9, 2023 jijini Dar es Salaam katika mashindano ya 23 ya Afrika ya Uhifadhi wa Qur’an kama sehemu ya programu yao ya kuleta manufaa kwa jamii kupitia mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 13, 2023 Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sheikh Nurdin Kishki amesema watu hao walituma maombi kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia akaunti ya mitandao mbalimbali ya kijamii ya taasisi hiyo, kupiga simu na hata kutuma ujumbe mfupi wa maandishi.

Hata hivyo kupitia mkutano huo Kishki ametoa utaratibu rasmi wa ufadhili huo ambapo muhitaji atatakiwa kujaza fomu ya maombi ambayo inapatikana katika ofisi za taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam kuanzia leo Aprili 13-Mei 2 mwaka huu na kisha utafanyika usaili na wale watakaofaulu watapatiwa ufadhilli huo.

Pia alisema mchakato huo utawahusisha wale ambao wamekidhi masharti na vigezo vinavyotakiwa ikiwemo muoaji kuwa Mtanzania ambaye bado hajaoa lakini tayari alishaposa.

"Fursa hii imewalenga zaidi wale vijana ambao walishachumbia lakini walishindwa kuoa kutokana na kushindwa kulipa mahari walizotajiwa kwa mkupuo," amesema Kishki.

Vilevile ameongeza kuwa muoaji anatakiwa kuwa Muislamu kwani ndoa hiyo itafungwa kwa misingi ya dini hiyo na pia aidhinishwe na imamu wa eneo husika kwa barua.

"Pia awe tayari kufunga ndoa ya pamoja ambayo itafungwa jijini Dar es Salaam chini ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir," anasema.