VIDEO: Miaka 14 hospitali akipigania uhai wake

Paulo Matemu mkazi wa Kirua vunjo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro akiwa kwenye kiti mwendo (wheel chair) katika Hospitali ya Kilema iliyopo Wilaya ya Moshi vijijini. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Hujafa hujaumbika. Ndivyo unavyoweza kusema ukimsikiliza Paulo Matemu (45) mkazi wa Kirua Vunjo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro akisimulia takribani miaka 14 ya maisha yake akiwa hospitalini.
Moshi. Hujafa hujaumbika. Ndivyo unavyoweza kusema ukimsikiliza Paulo Matemu (45) mkazi wa Kirua Vunjo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro akisimulia takribani miaka 14 ya maisha yake akiwa hospitalini.
Amekuwa sawa na mkazi katika hospitali kadhaa nchini, kufuatia ajali ya kuanguka kutoka ghorofani na kuvunjika uti wa mgongo, hali iliyosababisha apooze miguu.
Kwa sasa Matemu aliyepata ajali hiyo mwaka 2007 yupo hospitali ya Kilema mjini Moshi akiendelea na matibabu ambapo katika mahojiano na Mwananchi ameeleza jinsi ndugu zake walivyomkimbia, huku akihangaikia matibabu kuanzia wakati huo na anavyotamani kuanza maisha baada ya kutoka hospitali.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kilema, Dk Mayola Massawe alisema hali ya Matemu kwa sasa ni nzuri kwani wakati wanampokea mwaka 2013 alikuwa na vidonda vya kutisha na walipoona hali yake inazidi kuwa mbaya waliwasiliana na madaktari bingwa wa hospitali ya KCMC kuangalia namna ya kumsaidia.
Aeleza sababu ya maradhi
“Mwaka 2007 wakati nikiwa kwenye shughuli zangu mkoani Arusha nilidondoka kutoka ghorofani wakati nikirekebisha nyumba ya tajiri yangu. Nilivunjika uti wa mgongo ambapo baadaye hii hali ilisababisha kupooza miguu yangu yote mwili.”
“Nilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha nilipokaa kwa miaka miwili, baadaye nilihamishiwa hospitali ya KCMC nikakaa mwaka mmoja na baadaye Mwananyamala jijini Dar es salaam ambapo huku nako nilikaa miaka miwili kwa ajili ya mazoezi yaliyoniwezesha kuweza kukaa kwenye vitimwendo,” alisema.
Huku akiwa mwenye huzuni na mara chache kutabasamu aliongeza kusema: “Baada ya kuwa na uwezo wa kukaa kwenye kiti, niliomba nirudishwe nyumbani Moshi lakini baada ya muda mfupi nilipatwa na vidonda sehemu za makalio ndipo ikabidi niletwe hapa hospitali ya Kilema mwaka 2013 na tangu hapo nipo mpaka leo hii mnavyoniona.”
Alisema wazazi wake waliokuwa wakimhudumia walifariki dunia, huku mkewe waliyezaa mtoto mmoja naye akitokomea kusikojulikana jambo lililomfanya akose msaada wa karibu, “...lakini ninamshukuru Mwenyezi Mungu amenisaidia kwani hospitali ya Kilema hawakuniacha japo nilikuwa kwenye matatizo makubwa ya dunia ya namna hii.”
Alisema tangu mwaka 2013 amekuwa akitunzwa na hospitali hiyo, akiifananisha na ndugu na wazazi wake.
“Kwa kweli wamenisaidia kwa moyo mkunjufu na hapa nilipo Mwenyezi Mungu akinisaidia naweza kupona mapema kwani baada ya kufanyiwa upasuaji na haja kubwa na ndogo kutolewa kwa njia ya ubavu, vidonda vimeanza kukauka,”alisema na kuongeza;
“Baada ya kufanyiwa upasuaji mwaka jana Julai, nilibadilishwa utumbo wa haja kubwa ukawa unatolea haja kubwa na ndogo hapa ubavuni; hii imenisaidia kwa kiasi kikubwa kwani vidonda vilivyokuwa vikinitesa niliambiwa visingeweza kupona bila kufanyiwa upasuaji, lakini sasa hivi naendelea vizuri na vidonda vimeanza kupona.’’
Changamoto
Alibainisha kuwa changamoto kubwa inayomkabili baada ya kupona na kurudi nyumbani ni kutokuwa na sehemu ya kuishi, kwa kuwa hajui walipo ndugu zake aliowategemea huku wengine wakiwa wamefariki na wengine kumkimbia.
“Baada ya mke wangu kuona hakuna matumaini ya mimi kupona alinikimbia na kuniachia mtoto wa miaka sita wakati bado nimelazwa mwaka 2007 hospitali ya Mount Meru. Ilibidi niwaombe wazazi wangu wanisaidie kumwangalia mwanangu, lakini baadaye nao walifariki nikakosa msaada,’’ alieleza.
Akizungumzia changamoto zinazomkabili alisema: “Changamoto niliyonayo hata kiwanja ambacho marehemu baba yangu aliniachia sina uwezo hata wa kujenga vyumba viwili vya kukaa na kuweka biashara kidogo kulingana na ulemavu wangu. Sina uwezo hata wa kuuza kibiriti. Hapa nilipo mimi ni mlemavu. Niliowategemea wanisaidie wameshafariki.”
Aomba msaada
Ana wito gani kwa Watanzania wenzake? Matemu anasema: “Ninawaomba Watanzania wenzangu wenye moyo wa kunisaidia hata niweze kujenga nyumba ya kuishi kulingana na ulemavu wangu, hata kibanda ili niweze kufanya shughuli ndogondogo hata kama ni kuuza vibiriti ilimradi niweze kujikimu katika maisha yangu, kwani hapa nilipo tayari ni mlemavu na sina hata ndugu wa kunisaidia. Wanisaidie chochote cha kufanya ambacho kitaniondolea msongo wa mawazo.’’
Kauli ya daktari
Dk Massawe alizungumzia jinsi walivyompokea na kuomba msaada KCMC... “madaktari hao bingwa wa KCMC walishauri afanyiwe upasuaji ili kuruhusu vidonda vikauke.”
Alisema walimfanyia upasuaji tumboni uliomwezesha aweze kujisaidia haja kubwa na ndogo kupitia ubavuni mwa tumbo lake, na kwamba hali hiyo ndiyo iliyomsaidia vidonda vyake kukauka licha ya kuwa bado hajapona.
“Tuliamua kuchukua jukumu kumsaidia. Tunachoomba sisi arudi kwenye maisha yake ya kawaida, awe kama binadamu wengine, angalau apate nyumba itakayoendana na ulemavu wake,” alisema.
Aliongeza: “Pamoja na mambo mengine anahitaji msaada endelevu wa ‘colostomy bag’(mpira wa kuvalisha kwenye utumbo) ambapo kwa mwezi anatumia zaidi ya laki moja kwa ajili ya kununua mipira hiyo, kwa sasa kwa kweli anahitaji msaada wa hali na mali kutoka kwa Watanzania.”