Video: Mfahamu baharia wa kwanza mwanamke Tanzania
Dar es Salaam. Tangu utotoni alikuwa na ndoto ya kufanya kazi isiyofanywa na wanawake wengi, akitamani kuwa dereva wa treni au rubani lakini haikuwa hivyo baada ya kuhitimu kidato cha sita.
Alama alizopata kwenye mtihani hazikumwezesha kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu, hivyo alikwenda kusoma diploma katika Chuo cha Uvuvi Kunduchi, alikoingiwa shauku ya kufanya kazi ndani ya meli.
Huyu ni Regina Mbilinyi, anayeshika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza Mtanzania kufanya kazi ya mhandisi mitambo ndani ya meli.
Safari ya ubaharia ilianza mwaka 1994 baada ya mafunzo kwa vitendo kwenye meli za uvuvi, ikiwa ni mojawapo ya sharti la masomo katika kozi ya uvuvi aliyokuwa akisoma, akitakiwa kuwa sehemu ya wanaokwenda kuvua na meli za uvuvi.
“Nilikuwa na shauku ya kufanya kitu cha tofauti ingawa mwanzoni sikujua ni kitu gani hasa nataka, ndiyo maana nilikuwa natamani vitu vingi hadi nilipokuwa chuo cha uvuvi nikajikuta navutiwa na kufanya kazi kwenye meli.
“Hii ilitokea baada ya kwenda field (mafunzo kwa vitendo) kwenye meli za uvuvi. Nilivutiwa na maisha ya kwenye meli, akili yangu ikaniambia hiyo ndiyo sehemu natakiwa kuwa. Nilipomaliza diploma nikajiunga na chuo cha bahari kwa ajili ya kusoma kozi itakayoniwezesha nifanye kazi melini,” anasema.
Mambo hayakuwa rahisi kama alivyofikiria alipofika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI). Anasema alijikuta msichana pekee katika darasa la wanafunzi 22.
Mazingira hayo anasema kuna wakati yalimpa changamoto kutokana na namna wanafunzi wenzake walivyokuwa wakimtazama, wakiona hastahili kusoma kozi hiyo.
Baada ya mwaka wa kwanza wa masomo, wanafunzi waliofaulu mtihani walikuwa 13, Regina akiwa miongoni mwao.
Matokeo hayo anasema yalimtia moyo na kumhakikishia alikuwa eneo sahihi, hivyo akajipa moyo wa kupambana ili kutimiza ndoto ya kufanya kazi melini.
Anasema mwaka wa pili ulipomalizika, alikwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye meli iliyokuwa ikifanya safari kati ya Zanzibar, Pemba na Mombasa.
Regina anasema mambo yalikuwa mepesi kwake mwaka wa kwanza wa mafunzo kwa vitendo kwa kuwa nahodha wa meli hiyo, raia wa Norway, hakuwa na tatizo kwa mwanamke kufanya kazi kwenye meli.
Changamoto anasema zilianza baada ya nahodha huyo kuondoka na kuja mwingine Mtanzania ambaye hakufurahishwa na uwepo wa mwanamke kama sehemu ya mabaharia kwenye meli anayoiongoza.
“Yule nahodha alikuwa anasema wazi kwamba hii si kazi ya wanawake, hakuishia kunikatisha tamaa, hadi kile chumba nilichokuwa nalala alininyang’anya akaniambia nitajua mwenyewe nitalala wapi. Kwa kuwa nilishatengeneza uhusiano mzuri na wanaume wote waliokuwa ndani ya meli, basi wapishi wakajitolea kunipisha kwenye kitanda chao.
“Nasema kitanda siyo chumba kwa sababu chumba kina vitanda vya juu na chini, mimi nilikuwa nalala juu, chini wanalala wanaume wengine. Sikujali hayo niliamini ni njia ninayopita kufikia ndoto yangu, hivyo haikunisumbua,” anasema.
Kwa kuwa jukumu lake lilikuwa kuangalia mitambo, alikuwa anachagua zamu za kulala mapema muda ambao watu wengi wapo macho. Hivyo alikuwa akiamka usiku wa manane kwenda kufanya kazi hadi alfajiri.
Tukio ambalo hawezi kulisahau katika kipindi alichofanya kazi melini, anasema ni safari ya kwanza ndefu kwenda Somalia kupeleka mafuta.
“Wengi niliofanya nao kazi waliamini hiyo itakuwa safari yangu ya mwisho, nitaacha kazi kutokana na hatari iliyokuwa inasimuliwa kuhusu safari ya Somalia. Nilikwenda nikiwa na hofu kwa yale niliyoambiwa, na kweli njiani tulikutana na dhoruba kali. Kuna wakati unaona kabisa meli inazidiwa na mawimbi,” anasema.
Regina anasema maisha yaliendelea hadi alipomaliza mafunzo kwa vitendo na kurejea chuoni kukamilisha awamu ya mwisho ya masomo akiamini atafanya kazi ya ndoto yake melini.
Kazi ya ualimu
Mambo yalikuwa tofauti, anasema uongozi wa chuo ulimtaka abaki chuoni kufundisha na kuhamasisha wanawake kusoma fani za ubaharia.
“Kitendo cha kukaa melini kwa miaka miwili kiliwashangaza wengi, hata walimu wangu wakasema kama nimeweza kufanya kazi hiyo, basi nina kila sababu ya kubaki chuoni nihamasishe wanafunzi wengine, nikapewa jukumu la kufundisha.
“Kwa mara nyingine nikawa mwalimu wa kike peke yangu chuoni. Nilifundisha kwa muda kidogo nikapata fursa ya kwenda kuongeza ujuzi nchini Norway katika eneo la kuunda meli,’’ anasema.
Ushauri kwa wasichana
Regina anasema tofauti na ilivyokuwa zamani siku hizi kuna fursa nyingi kwenye ubaharia, hivyo ni eneo ambalo wanawake wanapaswa kulichangamkia kwa kuwa lina ajira za uhakika.