VIDEO: Idadi waliofariki dunia ajalini Arusha yafika 25
Muktasari:
- Ajali ilitokea Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), wilayani Arumeru ikihusisha magari manne.
Arusha. Idadi ya vifo vilivyotokana na ajali iliyohusisha magari manne eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), Barabara Kuu ya Arusha-Namanga imeongezeka na kufikia 25, majeruhi wakiwa 21.
Ajali ilitokea Jumamosi Februari 24, 2024 ikihusisha lori na magari mengine madogo matatu.
Akitoa taarifa jana usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji amesema miongoni mwa waliofariki wanawake ni 11, akiwamo mtoto mdogo wa kike na raia wa kigeni saba.
Ajali ilihusisha lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi nchini Kenya.
"Idadi ya majeruhi ni 21 kati yao wanaume ni 14 na wanawake ni saba,” amesema.
Magari mengine yaliyopata ajali katika tukio hilo ni T 623 CQF aina ya Nissan Caravan, T 879 DBY aina ya Mercedes Benz Saloon na T 673 DEW aina ya Toyota Coaster mali ya shule ya mchepuo wa Kingereza ya New Vision.
Kuhusu chanzo cha ajali, amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa ni kufeli mfumo wa breki wa lori, hivyo kusababisha liyagonge magari mengine yaliyokuwa mbele yake.
Amesema Jeshi hilo linaendelea kumsaka dereva wa lori hilo anayedaiwa kutoroka baada ya ajali.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alitaja idadi ya waliofariki kuwa ni 15 na kati yao raia wa kigeni walikuwa watatu.