VIDEO-Daktari bingwa Mtanzania achaguliwa, tuzo za uongozi Ujerumani

Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt Elisha Osati
Muktasari:
- Dkt Osati ni miongoni mwa madaktari watano vijana kutoka Afrika waliochaguliwa katika tuzo za Uongozi katika Utabibu inayoratibiwa nchini Ujerumani.
Dar es Salaam. Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt Elisha Osati ni miongoni mwa madaktari watano vijana kutoka Afrika waliochaguliwa katika tuzo za Uongozi katika Utabibu—yaani Young Physician Leaders Award inayoratibiwa nchini Ujerumani.
Kutokana na tuzo hiyo, Dkt Osati, ambaye ni daktari bingwa aliyehitimu hivi karibuni katika chuo kikuu cha tiba na sayansi shirikishi(Muhas), ataiwakilisha Tanzania katika mkutano wa afya wa dunia-(World Health Summit) utakaofanyika kuanzia Oktoba 12 huko Berlin.
Osati ni bingwa katika magonjwa ya ndani na anahudumu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Huku nchini Tanzania, aliteuliwa na taasisi ya kitaaluma katika sayansi(Tanzania Academy of Sciences), TAAS, na ni miongoni mwa matabibu 24 vijana watakaoudhuria mkutano wa afya wiki hii huko Berlin.
Wenzake waliochaguliwa kutoka Afrika ni Dkt Mohamed Abou El-Enein, kutoka Misri, Dkt Alaaddin Salih kutoka Sudan, Dkt Claudia Silva kutoka Cape Verde and Dkt Sean Wasserman kutoka Afrika Kusini.
Dkt Osati ameiambia MCL Digital kuwa hii ni fursa pekee ya kujifunza uongozi katika Nyanja ya utabibu. Mapema leo hii, emeitembelea kampuni ya Mwananchi Communications Limited na kufanya mahojiano maalumu-VIDEO
Amesema hiyo ni fursa ambayo imekuja muda muafaka wakati ambapo anatarajia kusimikwa rasmi kuwa Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania.