VIDEO: Ajali basi la Esther, Rav4 yaua watatu Kilimanjaro

Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea leo asubuhi, eneo la Mdawi, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro basi la abiria la kampuni ya Esther Luxury lilikuwa likitokea Moshi kwenda mkoani Dar es salaam kugongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Rav4.
Moshi. Watu watatu wamefariki dunia papo hapo baada ya gari aina ya Toyota Rav4 waliokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na basi la abiria la Kampuni ya Esther Kuxury, mkoani Kilimanjaro leo Jumamosi Februari mosi, 2025.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema ajali hiyo imetokea eneo la Mdawi, Wilaya ya Moshi.
"Ajali imetokea leo asubuhi eneo la Mdawi, watu watatu waliokuwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Rav4 wamefariki dunia baada ya gari hilo kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Esther Luxury lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es Salaam," amesema Mkomagi.
Amesema chanzo cha ajali ni baada ya dereva wa gari dogo kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kwenda kugongana uso kwa uso na basi hilo.
Hata hivyo, Kamanda Mkomagi amesema hakuna majeruhi kwenye basi hilo, na miili ya marehemu waliokuwa kwenye gari dogo imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.
Endelea kufuatilia Mwananchi digital kwa taarifa zaidi.