Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vicky Kamata abwagwa usimamizi mali za Dk Likwelile

Muktasari:

  • Mahakama Kuu imesema kuwa marehemu Dk Servacius na Mbunge mstaafu Vicky Kamata hawakuwa na nguvu ya kuingia katika ndoa na kwamba inayodhaniwa kuwa ilikuwa ni ndoa batili na mbunge huyo alikuwa kimada.

Dar es Salaam. Mbunge mstaafu wa viti maalumu na pia mwanamuziki, Vicky Kamata amegonga ukuta katika mgogoro wa mirathi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kubatilisha ndoa yao.

 Mirathi ya Dk Likwelile ambaye alifariki dunia Februari 19, 2021, bila kuacha wosia, imekuwa katika mgogoro mkubwa baina ya familia yake yaani watoto wake na ndugu wengine kwa upande mmoja na mbunge huyo mstaafu wa viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mgogoro huo ulipamba moto hasa mahakamani baada mmoja wa watoto wa marehemu Dk Likwelile kufungua shauri la mirathi akiomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi, lakini akawekewa pingamizi na mbunge huyo.

Mbunge huyo mstaafu alikuwa akidai kuwa alikuwa mke halali wa ndoa na Dk Likwelile, waliyoifunga Januari 30, 2016 katika Kanisa la Deliverance and Restoration Arusha.

Lakini watoto na familia ya marehemu Dk Likwelile wanamkana kuwa hakuwa mke halali wa marehemu bali alikuwa ni kimada tu aliyejipenyeza kwa haraka katika maisha ya baba yao kwa maslahi yake binafsi.

Baada ya mvutano huo baina ya pande hizo mbili, hatimaye Mahakama imekata mzizi wa fitina baada ya kumwengua mbunge huyo wa zamani katika mirathi hiyo, katika hukumu yake ya shauri la usimamizi wa mirathi.

Shauri hilo la mirathi namba 50 la mwaka 2021, lililofunguliwa na mmoja wa watoto wa  marehemu, Raymond Babu Likwelile akiomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo lakini Vicky aliweka pingamizi akipinga shauri hilo akitoa sababu mbalimbali.

Alidai kuwa mwombaji alihusisha kimakosa katika mali za marehemu mali ambazo ni zake.

Mosi, alizitaja mali hizo alizodai kuwa ni sehemu ya mali za marehemu bali ni za kwake binafsi kuwa ni pamoja na nyumba iliyoko kiwanja namba 116, Block namba 3 Mbweni ambayo ni nyumba ya wanandoa.

Nyingine ni nyumba mbili zilizoko katika eneo la ekari 9.5, Mpigi Magohe ambapo yeye anamiliki hisa asilimia 50, nyumba iliyoko katika kiwanja namba 387 na 389 Block D eneo maalum Sinza zilizosajiliwa kwa jina lake.

Vicky alitaja mali nyingine kuwa ni nyumba iliyoko Kibamba iliyo kwa jina la binti yake wa kumzaa, Gloria Likwelile, magari aina ya Toyota Prado namba T73 CQR na Toyota namba MC 588 AHT.

Vilevile kuna viwanja vinne namba 318, 319, 320 na 321 vilivyoko Mpigi Magoe, Wilaya ya Ubungo ambavyo ni mali za kampuni inayoitwa Beda Group Limited/Beda Farms Limited ambavyo yeye anamiliki hisa asilimia 50.

Sababu ya pili Vicky kuweka pingamizi hilo alidai kuwa mwombaji aliidanganya mahakama kwa kuwasilisha muhtasari wa kikao cha familia na kujiwakilisha mwenyewe alipofungua shauri hilo kwa kutokuweka wazi muhtasari wa kikao cha familia kilichomteua yeye kuwa msimamizi mwenza wa mirathi.

Tatu, alidai kuwa mwombaji alieneza katika mitandao ya kijamii taarifa za kashfa dhidi yake jambo lililosababisha kuharibu uhusiano kiasi kwamba hawaweza kupeana taarifa zozote.

Nne, alidai kuwa mwombaji si mtu sahihi kuliko mjane halali aliyesalia, kujua mali na madeni ya marehemu kwa sababu mwombaji ni mtu wa mbali na utambuzi wa mali za marehemu haufanyiki kwa kukisia.

Tano, alidai kuwa kwa makusudi na kwa nia ovu mwombaji aliacha kuweka jina lake katika orodha ya wanufaika wa mirathi ya marehemu alipofungua maombi na sita alidai kuwa ana hisia na taarifa zilizothibitika kuwa mwombaji atambagua kama atateuliwa kwa sababu alivyokuwa anamtendea vibaya.

Saba, alidai kuwa mwombaji si mtu mwaminifu ambaye atakusanya na kugawanya mali za mirathi kwa usawa na kwamba kuna uwezekano atahodhi mali zote za marehemu kwa kisingizio cha kuwa baba yake wa kumzaa na kwamba hivyo hastahili kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.

Nane, Vicky alidai kuwa anaomba kuteuliwa kuwa msimamizi pekee wa mirathi hiyo kwa usimamizi mzuri wa ofisi na mirathi ya marehemu.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mwombaji aliwakilishwa na wakili Edwin Nkalani, huku Vicky akiwakilishwa na wakili Alex Balomi.

Kabla ya kuanza usikilizwaji pande zote zilikubaliana kwa pamoja hoja tano ambazo zilipaswa kuamuriwa. Hoja hizo pamoja na kwamba kama:

Mosi, mpingaji yaani Vicky aliolewa kihalali na Dk Likwelile; mbili, nani kati ya mwombaji (Raymond) na mpingaji (Vicky) anastahili kuteuliwa kuwa msimamizi; tatu, kama muhtasari wa kikao cha familia ulipatikana kihalali.

Hoja ya nne ilikuwa ni kama Dk Likwelile (marehemu) na mpingaji (Vicky) kuna mali yoyote waliyoipata kwa pamoja na tano, ni nafuu gani wadaawa wanastahili.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Augustine Rwizile Septemba 15, 2023, kuhusu hoja ya kwanza kama Vicky aliolewa kihalali na Dk Likwelile, amesema kuwa licha ya kwamba waliishi pamoja kwa miaka saba lakini hapakuwa na ndoa halali.

Jaji Rwizile amesema kuwa kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutengana kwa Dk Likwelile na mkewe wa kwanza aliyefunga naye ndoa ya Kikristo Desemba 5, 1986, Mary Ibrahimu ama kwa talaka au kwa kifo.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mary alifariki dunia mwaka 2020, miaka minne baada ya Vicky kufunga ndoa na Dk Likwelile kama alivyodai.

Jaji Rwizile amesema kuwa kwa mujibu wa ndoa ya Kikristo ni ndoa ya mke mmoja, basi ndoa yoyote inayofungwa ndani ya ndoa nyingine inakuwa ni ukimada.

Hivyo amesema kuwa hapakuwa na ndoa baina ya Dk Likwelile na Vicky na hawakuwa na nguvu ya kufunga ndoa na kwamba hiyo iliyodhaniwa kuwa ni ndoa ni batili na hivyo Vicky hakuwa mke halali wa Dk Likwelile bali alikuwa kimada tu.

Kuhusu hoja ya pili kuwa nani anastahili kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi, Jaji Rwizile amesema kuwa ingawa uteuzi wa msimamizi pale panapokuwa na waombaji zaidi ya mmoja ni jukumu la mahakama kumteua mmojawapo, lakini pia inazingatia mtu mwenye maslahi ya karibu katika mirathi husika.

Amesema kuwa kwa kuwa mwombaji ni mtoto wa damu wa marehemu ana maslahi ya karibu katika mirathi hiyo kuliko mpingaji (Vicky) ambaye aliishi na marehemu kama kimada na asiye mrithi na hivyo amemteua mtoto huyo wa marehemu.

Kuhusu hoja ya tatu kama muhtasari wa kikao cha familia ulipatikana kihali, Jaji Rwizile amesema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa pande zote hakuna chochote ambacho kinaonesha kuwa ulighushiwa.

Katika hoja ya nne kama Vicky na Dk Likwelile kuna mali zozote walizochuma pamoja, Jaji Rwizile amesema kuwa hakuna ushahidi kuwa mali alizoziorodhesha Vicky siyo sehemu ya mirathi ya marehemu kwa kuwa hilo ni shauri la mirathi mahakama hiyo haina mamlaka kuamua swali kama mali walizochuma pamoja.

Badala yake amesema kuwa hili linaweza kuamuriwa katika shauri la talaka ambako wenza wanakuwa na fursa ya kuthibitisha kuwa ni lini na kwa namna gani mali hizo zilipatikana.

Jaji Rwizile licha ya kumteua mtoto wa marehemu kuwa msimamizi wa mirathi hiyo, amemtaka atekeleze matakwa ya kanuni ya 66 ya Kanuni za mirathi kuweka bondi ya mara mbili ya thamani ya mirathi ambayo imekadiriwa Sh4 bilioni ndani ya siku 14 kutoka siku ya uamuzi.