Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti waonyesha Kilimanjaro ilivyochafuka kwa ulevi

Muktasari:

Utafiti uliopita umethibitisha kwamba asilimia 60 ya wakazi wa Moshi wanatumia pombe mara kwa mara na asilimia 23 wanakabiliwa na shida za matumizi ya pombe

Dar/ Mikoani. Wakati matumizi makubwa ya pombe yakielezwa kuwa ndio kisababishi cha ulemavu, vifo, ajali, ugomvi na migogoro ya kifamilia, utafiti mpya umeweka wazi kukithiri kwa tatizo hilo mkoani Kilimanjaro.

Matokeo ya awali ya utafiti huo ulioangalia mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, umetajwa kuwa na viwango vya juu vya matumizi ya pombe, mara 2.5 zaidi kuliko katika maeneo jirani.

Utafiti uliopita umethibitisha kwamba asilimia 60 ya wakazi wa Moshi wanatumia pombe mara kwa mara na asilimia 23 wanakabiliwa na shida za matumizi ya pombe.

Katika eneo hili, matumizi ya pombe yamehusishwa pia na unyanyapaa mkubwa, tabia hatarishi za kijinsia na kuongezeka kwa kasi ya majeraha.

Kiongozi wa utafiti huo ulioangalia tabia mbalimbali za unywaji wa pombe kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini, Mkurugenzi wa utafiti Hospitali ya Rufaa KCMC, Profesa Blandina Mmbaga amesema matokeo ya awali yameonyesha Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza.

“Tafiti kuhusu unywaji pombe zimekuwa zikifanyika kwa kipindi cha miaka minane sasa, tukijaribu kuelewa tabia mbalimbali zinazosababisha unywaji.

“Lakini pia tunafanya ufuatiliaji kwa wagonjwa mbalimbali wanaopata madhara na changamoto ya afya ya akili kwa ajili ya unywaji wa pombe, ili waweze kupunguza kiasi cha pombe na ikiwezekana kubadili tabia. Bado hatujakamilisha utafiti huu,” amesema Profesa Blandina.

Utafiti huo umekuja wakati viongozi wa dini wakionya ongezeko la ulevi kwa mikoa ya kaskazini hususani Kilimanjaro.

Akihubiri katika ibada ya sikukuu ya Krismasi Desemba 25, 2022 katika Usharika wa Moshi mjini, aliyekuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo aliwataka vijana kuacha matumizi ya pombe kali, kwani ni hatari kwa usalama wa afya zao na zinachangia kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Alisema mtindo wa sasa wa vijana kunywa pombe kali zenye viwango vya vilevi vya asilimia 40, ni hatari kwa afya zao.

“Kumetokea mtindo wa vijana wachanga, wenye umri mdogo kunywa pombe kali na wanafikiri huo ndiyo mtindo kama unataka kuonekana wa kisasa, pombe kali hizi ni hatari, kweli vijana nawaonya nimeona wimbi hilo ni hatari,” alisema.

Kutokana kukithiri kwa tatizo la ulevi wilayani Moshi, Machi 25, mwaka huu, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kibosho, Padri Beatus Vumilia alisema vijana wameshindwa kuoa na kuzaa watoto.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zahanati mpya ya Matela iliyopo katika Kijiji cha Singa, Kata ya Kibosho Mashariki, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Padri huyo alisema imefika mahali jamii imeshindwa kujitawala na kutawaliwa na pombe.

“Kumekuwepo na changamoto baada ya jamii kuporomoka katika malezi na maadili hata katika suala la uzao nalo limepungua sana, limeathiri sana hata katika wale watoto wanaoingia katika malezi ngazi za mafundisho kwa upande wa wakatoliki, mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara idadi yao imeshuka sana.

"Jumatatu ya Pasaka tunategemea kubatiza, imekuwa ni tofauti na siku za nyuma tulikuwa tuna batiza watoto 100 lakini kwa kipindi hiki tunabatiza watoto wanane pekee,” alisema Padri Vumilia.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema atatangaza operesheni maalumu ya siku 21 kupambana na unywaji wa pombe haramu aina ya gongo, mirungi na bangi kwa wanaokunywa pombe saa za kazi, ili kuirejesha wilaya hiyo kama ilivyokuwa zamani.


Utafiti wenyewe

Utafiti huo uliofanyika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kilimanjaro (KCMC) kati ya Oktoba 2021 na Mei 2022 uliwahoji wagonjwa 678 wazima (miaka zaidi ya 18) katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro waliofika kupata huduma katika hospitali hiyo.

Matokeo ya awali yalionyesha kuwa wanaume waliohudumiwa matibabu ya kawaida walikuwa wameathirika zaidi kuliko wanawake wa matibabu ya kawaida na wanawake wa kliniki ya uzazi salama.

Washiriki

Katika utafiti huo, baadhi ya washiriki wamesema kuwa pombe husababisha unyanyapaa, unyanyasaji wa kijinsia, tabia za ngono hatari na uwezo wa wanajamii kutekeleza majukumu yao binafsi.

Wengi pia waliona kuwa inachangia katika ugomvi wa kimwili, kimaneno na kihisia kati ya wanafamilia na waliamini inachangia katika masuala ya afya ya muda mrefu na kutokuwa na uhakika wa kifedha.

"Ninachoweza kusema ni kwamba jamii haina matarajio chanya kuhusu matumizi ya pombe, kwa sababu tunaona familia zikivunjika, watu wakipatwa na maradhi kwa sababu ya pombe.

“Wapo wanaokunywa mwanzoni wanaweza kufanya kazi zao za kila siku, lakini baadaye wanashindwa kutekeleza majukumu kwa sababu pombe inawafanya kuwa dhaifu," amesema mmoja wa washiriki.

Kuhusu kutokutekeleza majukumu ya familia, washiriki wengi wamesema pombe imekuwa kizuizi katika uwezo wa mtu kutekeleza majukumu yake kwa familia yake.

“Watoto wanaoachwa nyumbani na wazazi wanaokunywa pombe wanaweza hata kupata unyanyasaji wa aina tofauti kwa sababu wazazi hawapo kumlinda,” amesema.

Kuhusu unyanyapaa, mshiriki mwingine amesema, "Kunywa pombe Tanzania ni kama ibada. Mtu yeyote anaweza kunywa. Unyanyapaa unatokea wakati mtu anashindwa kudhibiti tabia yake ya kunywa, kama vile mtu anakunywa kila wakati na anashindwa kutimiza majukumu yake, au ikiwa mtu anakunywa bia zile zinazotengenezwa nyumbani (vinywaji vya kienyeji) ambavyo havijajaribiwa na havijastahiliwa na shirika la viwango.

“Watu wanaokunywa gongo na dadii wananyanyapaliwa sana katika jamii. Kwa sababu mara tu unapokunywa vile, unaweza hata kushindwa kudhibiti haja yako ya choo, ambayo inapelekea aibu na fedheha," amesema mshiriki huyo.

Washiriki wa mahojiano wameripoti kwamba matumizi ya pombe yamesababisha au kuchangia katika matokeo makubwa ya kijinsia ambayo yalikuwa ya kipekee kwa kila jinsia.