UDSM yajitosa kuboresha pombe za kienyeji

Dar es Salaam. Pombe za kienyeji zina mchango katika kipato cha kaya, baadhi ya wanajamii wamekuwa wakisomesha watoto na kuendesha maisha yao kila siku kupitia biashara hiyo.
Kutokana na hilo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ndaki ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula, kinafanya utafiti kuhakikisha pombe hizo zinakuwa salama na ubora.
Katika utekelezaji wa hilo, chuo kimetenga fedha za utafiti kwa kuanzia na ulanzi ili kuirasimisha pombe hiyo inayotokana na ugemaji wa mianzi ambayo haijakomaa.
Mtaalamu UDSM
Dk Lilian Kaale, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ndaki ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula, anasema ni muhimu kuzifanyia utafiti wa kina pombe za kienyeji kuangalia usalama na ubora wake.
Anasema baada ya utafiti kufanyika ni vema pombe irasimishwe na kupata nembo ya ubora wa bidhaa kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“Kwa kurasimishwa na kupata nembo ya ubora, wajasiriamali wataweza pia kukopesheka, kwa kuwa ilivyo sasa taasisi za kifedha zinaogopa kutupa fedha kwenye kapu ambalo kesho watakosa wa kumdai kwa kuwa wajasiriamali hao hawapo katika mfumo rasmi,” anasema.
Anasema chuo kimeufanyia utafiti ulanzi katika mikoa ya Njombe na Iringa kuanzia mwaka 2018, ili kurasimisha pombe hiyo kwa kuwa wanajua ubora, usalama na kiwango cha kilevi kilichomo.
Dk Lilian anasema ulanzi huchangia asilimia 70 ya pato la kaya zinazojihusisha na biashara hiyo katika mikoa hiyo.
Pia chuo hicho kimenunua mtambo wa kupima pombe uliowagharimu Sh180 milioni ambao pamoja na mambo mengine hupima kiwango cha kilevi.
Mhadhiri huyo anasema chuo kimetenga Sh300 milioni kwa ajili ya utafiti wa pombe za kienyeji, hivyo baada ya ulanzi, wanatarajia kutafiti mbege na pombe nyingine za kienyeji.
Anasema tafiti zinazofanyika zinalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo pia huchangiwa na ulaji usiofaa, ikiwamo unywaji wa pombe.
Miongoni mwa magonjwa hayo anasema ni ya moyo, kisukari na shinikizo la damu.
Dk Lilian alieleza hayo katika mahojiano na Mwananchi kuhusu biashara iliyoshamiri sasa ya mbege (pombe ya kienyeji inayotengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu na kimea cha ulezi).
Biashara ya mbege
Eneo la Kibamba, Kwa Mangi, wilayani Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam ni maarufu kwa biashara ya mbege ambayo kwa asili hunywewa zaidi mkoani Kilimanjaro.
Katika makala haya, kinamama watatu waliofikiwa na Mwananchi wanaeleza namna wanavyomudu maisha kutokana na utengenezaji na uuzaji wa mbege.
Simulizi za kinamama
Tabia Assey, maarufu kama Mama Kibakoo, anasema alianza kupika mbege mwaka 2003.
“Nilikuwa nikiuza ulezi jirani na kituo cha daladala cha Kwa Mangi kabla mabanda yetu kubomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro. Niliyumba kutokana na mtaji kupungua, ndipo nilipoamua kuingia kwenye biashara ya kutengeneza mbege,” anasema.
Tabia anasema ulezi huupata Sumbawanga mkoani Rukwa, ndizi zikipatikana Morogoro na kwa uchache Kilimanjaro.
Anasema ndizi hununua tenga moja Sh12,000 na wakati mwingine huzipata kutoka kwa wajasiriamali wanaoziuza mitaani.
Mjasiriamali huyu anasema huuza mbege jumla na rejareja, akipata wateja kutoka Chanika, Kariakoo, Mbezi, Malamba Mawili, Kongowe na Mlandizi.
Anasema wateja wa jumla huwauzia dumu la lita 20 kwa Sh8,000; ambao mtaani huuza lita moja kati ya Sh1,000 na Sh1,300 kulingana na eneo.
Kwa siku anasema huuza kati ya lita 70 na 80 za mbege na kupata Sh90,000 hadi Sh110,000.
Faida za biashara
Ni kwa biashara hii anasema amesomesha watoto wake wawili hadi kidato cha nne, ambao baadaye walijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).
“Nashukuru watoto wangu wamemaliza shule, wamejiajiri; mmoja ni fundi magari na mwingine dereva,” anasema.
Kupitia kazi hii, anasema amenunua kiwanja, ingawa bado hajaanza kujenga, hivyo anaishi nyumba ya kupanga akimudu kulipa kodi kupitia biashara hiyo.
Mbali ya hayo, ametoa ajira kwa watu wanaomsaidia kuosha vyombo na kumenya ndizi.
“Hizi kazi tunagawana riziki, huwezi kung’ang’ania kufanya kila kitu utaumia. Mpaka mbege inafaa kunywewa unafanya mambo mengi hapo katikati,” anasema.
Hali ikoje kwa Flora
Flora Assenga ‘Mama Vice’ anasema alijifunza kupika mbege mwaka 1991, baada ya kifo cha mumewe. Katika biashara anashirikiana na mtoto wake Vice, mwenye elimu ya kidato cha nne, ambaye ni wa pili kati ya watoto wake watatu.
“Kupitia kazi hii, mtoto wangu ambaye ana familia yake anapata kipato cha kuendesha maisha yake,” anasema Flora, anayeuza mbege rejareja kwa wateja wanaofika eneo lake la biashara.
Kwa biashara hii, anasema amejenga nyumba kwa kuwa kiwanja kilikuwapo.
Mjasiriamali mwingine
Rufina Ngowi, maarufu kama Mama Imma, ana miaka miwili katika biashara hiyo. Awali, alikuwa akiuza vyombo na mume wake sokoni Tandika.
Rufina anasema alijitosa kupika mbege ili kuendesha familia yao yenye watoto watatu.
“Hatuwezi kukaa kutwa sehemu moja tunasubiri biashara ya vyombo, lazima tuangalie na njia nyingine ili mambo yaende,” anasema.
Anasema ujuzi wa kuandaa mbege aliupata nyumbani kwao Moshi, kwa kuwa ilikuwa moja ya biashara ya familia yao.
Ukosefu wa mitaji
Ili kuboresha kinywaji hicho, wajasiriamali hao wanaiomba Serikali kuwapatia mikopo.
“Pia wasomi wa mambo ya vileo wasibaki ofisini, waje watufundishe namna ya kuboresha pombe hizi za asili ambazo wengi maeneo walikozaliwa ndiyo zimesaidia wao kusoma. Pia ni moja ya utamaduni wetu, hivyo tusiache ukapotea,” anasema Tabia na kuongeza:
“Ikiboreshwa tutaweza kuuza kwenye masoko ya kimataifa kama zilivyo pombe nyingine kutoka nje zinavyoletwa hapa kwetu.”
Kwa upande wake, Rufina anatoa wito kwa wanawake kujishughulisha badala ya kutegemea wanaume wao kuwapa fedha kwa kila kitu.
“Nyumba ni mwanamke, wewe ukilala na nyumba inalegalega. Siku baba akikosa unasaidia, hutaweza kufanya hivyo kama huna chanzo cha kukuingizia kipato,” anasema.
Kauli za wateja
Shauri Tarimo anasema, “nilijua mbege inapatikana kule tulikozaliwa Moshi, sikuwahi kuwaza nitaikuta Dar. Huwa nikifika hapa kunywa najiona nipo nyumbani kwa wazee wangu. Huwa tunakuwa na matambiko yanayotumia mbege, hulazimiki kuagiza Moshi, unanunua Dar.”
Naye Cecy Moshi, anasema huuza mbege Kariakoo akipata faida ya takriban Sh20,000 baada ya kuuza lita 20 zinazomgharimu Sh8,000.
Anasema alianza biashara miaka miwili iliyopita kwa mtaji mdogo wa Sh10,000.
Athari kiafya
Dk Shita Samwel, anasema mbege ni sawa na pombe nyingine isipokuwa inatengenezwa kienyeji.
Anasema isipoandaliwa katika mazingira safi, kuna uwezekano wa wanywaji kupata madhara.
Dk Shita anasema iwapo maji yanayotumika kuandaa mbege hayatakuwa salama, watu wanaweza kupata magonjwa ya matumbo kama vile amoeba, kuhara na kuhara maji au damu.
Anasema ni muhimu kuzingatia usafi wa vyombo vinavyotumika kuandaa pombe hiyo, maji yawe safi na salama na kuhakikisha nafaka inayotumika inahifadhiwa katika hali nzuri.
Madhara ya mbege, anasema ni sawa na ya pombe nyingine, ikiwamo uraibu, magonjwa ya akili na hata ya ini.
Mtazamo kiuchumi
Mchambuzi na mshauri wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude, anasema pombe za kienyeji zinatumika tangu enzi za mababu lakini hazitangazwi.
Anasema zinazopata matangazo ni za kutoka nje ya nchi, huku ukionekana unakunywa ya kienyeji au kuitangaza unatafsiriwa kuwa mshamba.
“Ukweli ni kuwa pombe za kienyeji ni nzuri hata katika uchumi kwa kuwa ni bidhaa inayohitajika, kutokana na ubunifu inaweza kuuzwa kwenye maduka makubwa na hata nje ya nchi,” anasema.
Akiitaja moja ya pombe za asili ya Afrika Kusini, anasema iliwahi kuuzwa nchini, hivyo kuhoji ni nini kinashindikana kuzipandisha hadhi za Tanzania.
“Kinachotofautisha hapa ni kwamba pombe za kienyeji hazitengenezwi katika utaratibu kama wa viwandani, hivyo kukosekana sifa ya ubora," anasema.
Anashauri wataalamu kuangalia namna ya kuziboresha ili kufikia viwango vya ubora ziuzwe hata nje ya nchi.
“Sekta hii kama ingeangaliwa ina faida nyingi, mbali ya wanaotengeneza kujiingizia kipato, ingesaidia kulinda afya za watumiaji. Tuache dhana kuwa kitu kizuri ni kile kilicholetwa na wazungu wakati tuna vya kwetu vya kujivunia," anasema.
Anasema nchini Japan pombe zinazouzwa zimetokana na asili ya makabila yao, hivyo hilo linaweza pia kufanyika nchini na kuongeza mnyororo wa thamani kuanzia kwa wakulima shambani.