Usiyoyajua kuhusu meli ya Titanic

Muktasari:
- Mwaka 1912 meli ya Titanic iliyokuwa ikifanya safari zake katika bahari ya Atlantic ilizama na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,500 na upotevu wa mali. Ilikuwa ni ajali ambayo ilitabiriwa na watunzi wa vitabu.
Aprili 15, 1912 meli kubwa ya Titanic ilizama kwenye bahari ya Atlantic. Meli hiyo ilizama ikiwa ni siku ya nne baada ya kuanza safari yake kutoka Southampton Uingereza kwenda New York Marekani.
Ajali hiyo ilisababishwa na meli hiyo kugonga mwamba wa barafu saa 5:40 usiku wa Januari 14, 1912 na kuanza saa mbili baadaye.
Kuzama huko kulisababisha mauaji ya watu wapatao 1,500 kati ya abiria 2,224 waliokuwemo kwenye meli na kufanya kuwa ajali mbaya zaidi ya meli kuliko zote.
Kabla ya kugonga mwamba huo, nahodha na waongoza meli hiyo walipata maonyo sita ya kuwepo kwa hatari hiyo, lakini walipuuzia.
Taarifa ilitolewa sekunde 34 kabla ya meli kugonga barafu na kuzama, ilitahadharisha kuwa mbele kuna mwamba wa barafu lakini waongozaji wa meli walipuuza taarifa hizo hadi pale meli ilipogonga barafu na kuchukua saa mbili na dakika arobaini hadi kuzama.
Mpaka meli inaufikia mwamba huo, haikuweza tena kusimama haraka wala kugeuka na hivyo kujikuta ikiugonga na kusababisha mpasuko kwenye matanki sita kati ya 16 ukiwemo mtungi wa kuchemshia maji kwa kuwa meli ilitumia injini ya mvuke.
Mabaharia walijaribu kuwasiliana na meli nyingine na mamlaka nyingine kwa kutumia radio za masafa, lakini haikuwa rahisi kupata msaada.
Hata baada ya meli kupasuka na kuanza kuzama, abiria wengi bado walikuwa ndani wakijaribu kujiokoa. Meli haikuwa na boti za kuokolea za kutosha, hivyo watu wengi walijaa kwenye boti chache huku wengine wakiishia kujirusha ndani ya maji na kufa maji.
Meli iliyokuja kuwaokoa ilifika baada ya saa nne baadaye na kukuta watu wengi wameshakufa.
Ajali hiyo iliushtua ulimwengu na kusababisha sheria na kanuni nyingi za usafiri wa maji kutungwa.
Ajali hiyo imetungiwa filamu na imekuwa na simulizi nyingi. Miongoni mwa simulizi hizo zimeonyesha kuwepo kwa mambo ya kushangaza.
Kwa mfano, ajali hiyo ilitabiriwa tangu mwaka 1898, lakini hakuna aliyewahi kuwaza suala hilo. Mwaka huo Morgan Robertson aliandika kitabu cha ‘The Wreck Of Titan’ akieleza ajali iliyoipata meli iliyokuwa ikiitwa Titan.
Robertson licha ya kuwa mwandishi wa vitabu, aliwahi pia kuwa baharia, kwa hiyo baadhi ya vitabu vyake vilieleza mambo kuhusu usafiri wa maji.
Hata hivyo, kitabu hicho hakikupata umaarufu, hadi meli hiyo ilipozama, ndipo kilianza kutafutwa na kikajizolea umaarufu na watu wengi wakatamani kukisoma kwakuwa kilitabiri kutokea kwa ajali ya meli ya Titanic.
Kwa mfano, watu walijiuliza, kwa nini mwandishi alitumia jina la Titan? Kwa nini waliounda meli hiyo nao walitumia jina hilohilo?
Baada ya meli hiyo filamu nyingi zilitengenezwa, lakini filamu kali inayotamba mpaka sasa ni ile iliyotengenezwa mwaka 1997 ambayo imetumia fedha nyingi kuliko hata fedha zilizotumika kuijenga meli yenyewe.
James Cameroon alitumia Sh500.2 bilioni wakati wa kutengeneza filamu ya Titanic iliyotoka mwaka 1997 iliyotungwa na James Cameroon wakati mmiliki wa kampuni ya White Star Line walitumia Sh1.95 bilioni kutengeneza meli ya Titanic.
Umaarufu wa filamu hiyo ulichangiwa na ushiriki wa mastaa akiwemo Leonardo Di Caprio na Kate Winslet.
Mbali na filamu hiyo, kuna filamu takribani 11 zilizotengenezwa baada ya kuzama meli hiyo.
Mwezi mmoja baada ya kuzama kwa meli ya Titanic muvi ya ‘Saved from the Titan’ ilitoka, mwigizaji Dorothy Gibson alishirikishwa kwenye muvi hiyo kwakuwa aliokolewa wakati meli ikizama na nyingine iliitwa ‘A Night to Remember’ ya mwaka 1958.
Wakati meli ikizama kulikuwa na uhaba wa boti za kuokolea hivyo kipaumbele kikatolewa kwa wanawake na watoto. baadhi ya wanaume akiwemo tajiri Joseph Bruce Ismay aliyaokoa maisha yake baada ya kuvaa mavazi ya kike na kuruhusiwa kuingia kwenye boti.
Mbinu yake ilimsaidia ingawa alichafuliwa jina na Wamarekani baada ya kuitelekeza meli yake wakati ikizama.
Kwa kuwa meli hiyo ilikuwa ikitumia makaa ya mawe kujiendesha kulikuwa na watu 176 waliokuwa na kazi ya kuweka tani 600 za makaa ya mawe kwa siku.
Hivyo kila siku meli hiyo ilikuwa ikitumia tani 600 za makaa ya mawe. Hata hivyo inadaiwa kwa siku ilikuwa ikimwaga tani 100 za majivu kwenye bahari ya Atlantic majivu hayo yaliyotokana na tani 600 za makaa ya mawe ambayo yalikuwa yakitumika kwa siku.
Ujenzi wa meli
Mwaka 1909 White Star Line ilitoa zabuni ya kutengenezwa kwa meli ya Titanic, Lord Pirrie rafiki wa Joseph Bruce Ismay alichukua oda hiyo na kuanza kuitengeneza Titanic.
Wakati wa ujenzi wa meli hiyo, wajenzi wanane walifariki na 246 walijeruhiwa. Mwishoni mwa Machi 1912 meli hiyo ilikamilika na kuanza safari zake Aprili 10 mwaka huo hadi pale ilipozama Aprili 14.
Meli hiyo ilikuwa na madaraja matatu ambayo ni daraja la juu, la kati na la chini. Matajiri walikuwa kwenye daraja la juu, walipata huduma nzuri. Kwa wakati huo ulipaswa kulipia tiketi ya dola 4700 ambazo ni zaidi ya Sh12.2 milioni kwa sasa ili uwe daraja la kwanza.
Daraja la tatu au la chini lilikuwa na mabafu mawili tu, takribani abiria 700 wa daraja hilo walikuwa wakichangia mabafu hayo mawili. Hata hivyo, abiria wa daraja la chini hawakurusiwa kuingia sehemu za matajiri.
Ndani ya meli kulikuwa na bendi ya muziki ya watu wanane wakiongozwa na Wallace Hartley ilikuwa ikiwafariji abiria wakati meli ikizama, bendi hiyo iliendelea kuimba baada ya kuona abiria wameshtushwa na kuogopa wakati meli ikizama.
Waimbaji hao waliweza kuwafariji abiria huku wengine wakicheza na kukisubiria kifo kilichokuwa mbele yao. Sio tu kuwafariji wengine lakini pia bendi hiyo iliimba nyimbo ili kujifariji na wao. Waimbaji wote nane walifariki baada ya meli kuzama.
Ndani ya meli ya Titanic kulikuwa na wanyama wengi lakini mbwa wawili tu pomeranian na pekingese ndio waliookolewa wengine wote walikufa baada ya meli kuzama.