Usaili wagombea Chadema ngazi ya kanda waanza

Watia nia wa nafasi za mabaraza na uongozi wa kanda wakiwa ukumbini, kwa ajili ya kufanyiwa usaili na Kamati Kuu ya Chadema.
Muktasari:
- Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinafanya usaili kwa wagombea wa nafasi za uenyekiti, makamu wenyeviti na wahazini wa kanda nne za chama hicho.
Dar es Salaam. Baada ya kusubiri kwa saa kadhaa, sasa watia nia nafasi ya wahazini, uenyekiti na umakamu wa kanda nne za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameitwa mbele ya kamati kuu kwa ajili usaili wa nafasi walizoomba.
Mchakato huo ulipaswa kufanyika jana Jumapili pamoja na watia nia wa nafasi za mabaraza ya chama hicho ya wanawake, vijana na wazee kwa ngazi ya mikoa, lakini kutokana na ufinyu wa muda wakaombwa usaili ufanyike leo Jumatatu Mei 13, 2024.
Tayari baadhi ya watia nia wakiwemo wabunge wa zamani wameshawasili katika ofisi za makao makuu ya Chadema Mikocheni wilayani Kinondoni, mkoa wa Dar es Salaam wakisubiri kuitwa katika ukumbi unaotumiwa na wajumbe wa kamati kuu walioingia siku ya tatu ya kikao hicho.
Watia nia hao kutoka kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).
Kikao hicho cha kamati kuu ndicho kitakachopanga ratiba ya mchakato wa uchaguzi wa kanda za nne za Chadema ambazo zinatekeleza jukumu hilo baada ya kumaliza uchaguzi katika ngazi ya chini hadi mkoa.
Shughuli ya usaili ya watia nia hao inaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Tundu Lissu (Makamu Mwenyekiti bara), Said Issa Mohammed (Makamu Mwenyekiti Zanzibar), Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na manaibu wake Benson Kigaila na Salum Mwalimu.
Miongoni mwa watia nia waliofika ni pamoja Joseph Mbilinyi maarufu Sugu anayewania uenyekiti wa kanda ya Nyasa ambapo atachuana na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi hiyo. Wawili hawa watakutana endapo watapenya kwenye mchakato wa usaili utakaofanyika muda mchache ujao.
Wengine ni Alex Kimbe, Rhoda Kunchela, Lucas Ngoto, Frank Mwakajoka, Emmanuel Ntobi, Ester Jackson, Gimbi Masaba na wengine.
Kwa watia nia ambao ni wajumbe wa kamati kuu watatakiwa kukaa nje wakati usaili wagombea wa nafasi ya uenyekiti ikianza ili kuepusha mgongano wa kimasilahi na washindani wao wengine katika nafasi hiyo.
Shughuli ya usali imeanza saa 6:00 mchana kwa nafasi ya uhazini wa kanda ya Nyasa.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali kutoka ukumbini hapo.