Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usafirishaji haramu wa binadamu bado tatizo kwa jamii

Katibu Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji haramu wa Binadamu ndani ya Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella akizungumza leo Jumanne Julai 4 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa maafisa kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Songwe. Kuelekea maadhimisho ya kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu duniani yatakayofanyika Julai 30, mwaka huu Mkoa wa Songwe umetajwa kama moja ya mikoa ambayo watu wake wanaathirika na biashara hii kwa watu kusafirishwa kwenda nje za nchi kutumikishwa.

Katibu Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji haramu wa Binadamu ndani ya Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella amesema hayo leo Jumanne Julai 4 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa maafisa kutoka taasisi mbambali za serikali zinazo shugulika na maswala ya usimamizi wa sheria na upambanaji wa maswala yanayoenda kinyume na taratibu na sheria za nchi ndani ya Mkoa wa Songwe.

Mafunzo hayo yanayotolewa na Shirika la Tanzania Relief Initiatives (TRI ) na kufadhiriwa na Hanna Seidlel Foundation maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo wadau mbalimbali Mkoa wa songwe wanaotekeleza sheria inayozuia usafirishaji haramu wa Binadamu ambapo Mkoa wa Songwe yanafanyika kwa mara ya kwanza.

"Katika utendaji wetu wa kazi imekuja kuonekana Songwe ni sehemu ambayo watu wanasafirishwa kutoka songwe kwenda sehemu mbalimbali na wanavushwa mapaka nje ya nchi, wengine wanapelekwa Kenya kwenda kutumikishwa," anasema Fella.

Ameongeza hali ya mapambano kwa Serikali inajitahidi kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kutumia mafunzo kama hayo katika kusaidia kupambana na biashara hiyo pamoja kufanya mabadiliko ya sheria ambazo zinasaidia katika mapambano ya biashara hiyo.

Aidha Mkurugenzi wa Miradi kutoka TRI, Damiani Edward amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuwajengea uwezo wadau mahususi wanaojikita katika kusimamia sheria mbalimbali ikiwemo sheria inayopinga usafirishaji haramu wa binadamu ,ambapo wadau walioshiriki mafunzo hayo ni pamoja na Jeshi la Polisi, maafisa uhamiaji, maafisa wa mahakama, maafisa kazi, maafisa ustawi wa jamii na waendesha mashtaka.

Edward ameongeza wahanga wakubwa wa biashara haramu ni wanawake, vijana na watoto ambao hudanganywa kwa kuahidiwa kazi nzuri mijini katika miji mikubwa kama Dar es Salam, Mwanza na Arusha au nje ya nchi.

Seradhine Msacky mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe amesema mafunzo hayo waliyoyapata yamewaongezea uelewa mkubwa juu ya mbinu na njia zinazotumiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu hivyo mafunzo hayo yanaenda kuwasaidia katika kupambana na tatizo hilo.

Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mbozi, Jeneth Mung'ong'o amesema usafirishaji haramu unamadhara makubwa kwa jamii kwani watu huenda maeneo ya vijijini na kuwadanganya wanawake na watoto kuwa wanaenda kuwapatia kazi mijini na badala yake huwachukua na kuwapeleka katika kuwatumikisha.

Ameongeza kusema bado kuna uelewa mdogo katika jamii juu ya madhara ya usafirishaji haramu wa binadamu na matokeo yake madhara makubwa yanatokea kutokana na kutokuwa na elimu.

"Sisi kama maafisa ustawi tunatoa jitihada za kutoa elimu kwenye jamii kutokana na madhara kwa wazazi kuwa makini na watoto wao pale mtu anapokuja kuwataka kwenda kuwafanyisha kazi sehemu za mbali."