Upelelezi kesi ya Kinemo, anayedaiwa kutapeli Sh90 milioni wakamilika

Muktasari:
- Kinemo anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa madai kuwa atamnunulia mlalamikaji gari tatu, lakini hakufanya hivyo.
Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kujipatia Sh90 milioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili Mashella Kinemo (34) umekamilika.
Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Aprili 23, 2025 wakati kesi hiyo ya jinai ilipoitwa kwa kutajwa.
Wakili Mafuru ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
"Kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake umekamilika, hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH)," amesema Mafuru.
Hakimu Mushi baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, 2025 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na shitaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kinemo anadaiwa kutenda kosa hilo, Februari 3, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kwa njia ya ulaghai na udanganyifu alijipatia Sh90 milioni kutoka kwa Osiana Waiguta kwa madai kuwa atamnunulia gari tatu wakati akijua kuwa ni uongo.