Ummy: Tuzingatie ushauri kabla ya kutumia dawa

Muktasari:

  • Serikali imeeleza umuhimu wa kunywa dawa kwa kufuata ushauri wa daktari ili kuepuka kupata usugu wa dawa na kutopona kwa wakati.

Dar es Salaam. Serikali imeeleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa ndiyo chanzo  cha usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Uvida).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumzia kampeni inayoendelea nchini ya kukabiliana na Uvida, iliyopewa jina ‘Holela-Holela itakukosti’.

Kampeni hiyo ilizinduliwa jijini hapa mwishoni mwa Mei mwaka huu kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Mazingira, huku ikifadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Breakthrough Action.

Ummy amewataka Watanzania kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kutumia dawa.

“Tumieni dozi ya dawa kikamilifu kama mnavyoshauriwa na mtaalamu wa afya.”

“Pia fuateni maelekezo ya mtaalamu wa mifugo, kilimo juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa mifugo, mimea, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na usafi wa mazingira kwa ujumla,” amesema.

Vilevile, Ummy amesema ‘suala la Uvida’ ni tatizo kubwa lenye athari za kiafya ambazo hazijitokezi mara moja.

“Athari zake ni kama vile ugonjwa kujirudiarudia na kuchukua muda mrefu kupona, kuenea na kusambaa kwa vimelea sugu vya magonjwa dhidi ya dawa, ulemavu na hata kifo.

“Mbali na hapo kuna athari za kiuchumi kama vile kutumia gharama kubwa kwenye matibabu, hivyo kupungua kwa pato binafsi, la familia na Taifa,” amesema Ummy.

Amesema ndiyo maana zinafanyika juhudi kuhakikisha Uvida inaondoka.

Waziri Ummy alisema kuwa Serikali inafanya jitihada kabambe za kukabiliana na Uvida, ikiwemo kuzindua kampeni  hiyo ya “Holela Holela itakukosti”, lengo ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kukabiliana na suala hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania, Alex Klaits amesema kuna umuhimu wa juhudi za pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo. "Kampeni hii inaonyesha jukumu muhimu la ushirikiano katika kuleta athari chanya na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu, ikiwaleta pamoja wadau wa afya pamoja kutoka sekta mbalimbali kupambana na Uvida na magonjwa ya zuonotiki,” amesema.

Pamoja na kampeni hiyo, upo mpango kazi wa mapambano ya Uvida (NAP AMR 2023-2028), na kamati ya Taifa ya Mapambano ya Uvida (AMR MCC) inayofanya kazi chini ya mwavuli wa Afya moja.