Ulega amwonya mkandarasi Ifakara, atishia kumweka kwenye ‘blacklist’
Muktasari:
- Asema utekelezaji umefikia asilimia tano pekee licha ya malipo ya awali ya Sh9.5 bilioni kutolewa, huku akitaka kikao cha dharura kujadili hatma ya mradi huo.
Morogoro. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara mkoani Morogoro kufuata masharti ya mkataba, la sivyo utavunjwa na kampuni hiyo kupigwa marufuku kupewa kazi yoyote nchini.
Mkandarasi huyo ni kampuni ya Henan Railway kutoka China inayojenga barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5, ambapo, ingawa imelipwa malipo ya awali, kasi ya ujenzi haiendani na kiwango kilichotakiwa kufikiwa hadi sasa.
Akizungumza jana, Jumanne, Julai 14, 2026, wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Ulega amesema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi na maendeleo ya uchumi.
“Hivi hamuoni namna wananchi wanavyoumia kwa kutotimiza wajibu wenu kwa mujibu wa mkataba? Barabara haijengwi kwa kasi, vumbi ni jingi na usumbufu kwa wananchi ni mkubwa. Hili hatuwezi kuvumilia. Mkiendelea hivi, itabidi tuchukue hatua ngumu,” amesema.
Waziri huyo ametoa muda wa wiki moja kwa wataalamu wa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kukutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo katika kikao cha ngazi ya juu ili kujadili hatima ya utekelezaji wa mradi huo.
“Kikao hicho kifanyike Ijumaa na watueleze kwa nini mradi huu tusiwanyang’anye na vifaa vyao tukawapatia watu wengine? Na Jumatatu, Julai 20, nipate jarada la maelezo ya kina na kamili,” amesema Ulega.
Waziri huyo amesema mradi huo umechelewa kukamilika kwa kiwango kikubwa, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia takribani asilimia tano pekee, licha ya Serikali kuwa imeshalipa malipo ya awali ya Sh9.5 bilioni.
Amesema kiwango hicho cha fedha hakilingani na maendeleo halisi ya kazi yaliyopo eneo la mradi.
“Serikali haitakuwa tayari kuona fedha za umma zinatumika bila kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Mkandarasi lazima aoneshe uwezo na dhamira ya kukamilisha mradi huu, vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa,” amesisitiza Ulega.
Pia, amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kwa wakati ili kuondoa adha wanazokumbana nazo wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu, hali inayochangia ugumu wa usafiri na kuongezeka kwa gharama za nauli.
Aidha, Waziri Ulega amemuagiza mkandarasi kuanza mara moja kufanya uboreshaji wa barabara hiyo kwa kuziba mashimo na kumwaga maji mara kwa mara ili kupunguza vumbi linalowaathiri wananchi wanaoishi na wanaotumia barabara hiyo wakati ujenzi ukiendelea.
Katika hatua nyingine, Ulega ameagiza kipande cha barabara kinachoanzia Chita hadi Mkoa wa Njombe kifanyiwe matengenezo ya haraka ili kipitike kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema umuhimu wa barabara hiyo katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, mazao na abiria, hivyo kuchochea uchumi wa wananchi, huku akisisitiza kuwa barabara hiyo ni huduma muhimu inayogusa maisha ya wananchi wa Mlimba na Wilaya ya Kilombero.
Naye, mbunge wa Mlimba, Rose Rwakatare, amemuomba Waziri wa Ujenzi kumbana mkandarasi huyo ili aendeleze ujenzi wa barabara kwa kasi, kwani fedha alizolipwa haziendani na kazi iliyofanyika.
“Sisi wana Mlimba tunateseka sana kutokana na barabara hii. Tuambiwe, barabara hii inaanza kutekelezwa lini? Fedha zimetolewa, hatuoni barabara, hatuoni chochote. Sasa atueleze anaanza kutekeleza nini,” amesema Rose.