Prime
Ukweli kuhusu dhana ya wajane kuishi zaidi ya wagane
Muktasari:
- Kifo cha mwenza hubadili maisha ya mtu kwa namna tofauti huku kukiwa na dhana katika jamii kwamba baadhi ya wajane huonekana kujijenga upya na kuendelea kuishi kwa miaka mingi baada ya kufiwa na wenza wao, tofauti na wagane ambao wengi hukumbana na changamoto za huzuni, upweke.
Dar es Salaam. Baada ya kumpoteza mwenza wa maisha, watu wengi hukumbwa na huzuni, msongo wa mawazo na mabadiliko ya maisha.
Katikati ya hali hiyo, kwa miaka mingi kuna dhana kuwa wanawake wajane baada ya kufiwa na wenza wao, huishi muda mrefu zaidi kuliko wanaume wagane, jambo ambalo katika muktadha wa sayansi, saikolojia na mtazamo wa jamii limekuwa likiibua mjadala.
Baadhi ya watu wamekuwa wakiamini wanaume hupata ugumu zaidi wa kuendelea na maisha baada ya kumpoteza mke kuliko wanawake anapofiwa na mume, lakini wengine huamini hiyo ni dhana tu ya kijamii.
Hata hivyo, kisayansi na kisaikolojia inaelezwa kinachosababisha nadharia hiyo ni tofauti ya mfumo wa maisha kati ya mwanamke na mwanaume.
Kulingana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina wajane 1,396,262, idadi ambayo ni asilimia 4.4 ya wanawake wote nchini.
Hata hivyo, takwimu hizo hazionyeshi kwamba wanawake huishi muda mrefu zaidi baada ya kufiwa kuliko wanaume, ingawa wanasaikolojia na sosholojia wanaeleza msingi wa dhana hiyo katika jamii.
Shuhuda za wahusika
Mwanariadha nyota wa zamani, Filbert Bayi ni miongoni mwa wagane wanaoeleza maisha yalivyokuwa baada ya kufiwa na mke.
Baada ya kufiwa na mkewe Anna miaka zaidi ya minne iliyopita, anasema kwa wanaume wengi wanapopoteza wenza, huwa wanashindwa kukubaliana na hali halisi, hasa kwenye majukumu ya ndani ya familia.
Huku akitabasamu, Bayi anasema," suala la kufa mapema sina hakika nalo, japo jamii kubwa huwa inaona hivyo lakini mbona mimi sijafa!
"Ninachokiona kwa sisi wanaume huwa tunashindwa kubeba yale majukumu ya mke, hivyo tunajikuta kwenye msongo na hofu ya vipi tutaweza kuwa baba na wakati huohuo mama. Huo msongo ndio unatusababishia matatizo mengine na kujikuta mtu anapoteza maisha kwa maradhi mara tu baada ya kifo cha mke," amesema.
Mgane mwingine, Ramadhan Mwenda wa Temeke aliyefiwa na mke wake hivi karibuni, anaeleza namna maisha yake yalivyobadilika baada ya msiba huo.
Anasema mkewe ndiye aliyekuwa injini ya maisha yake akiratibu dawa zake za kisukari, akihakikisha anakula mlo sahihi kwa wakati, na kuweka mazingira ya nyumba katika mpangilio mzuri.
Akizungumza kwa kukata tamaa, Mwenda (65) anasema anatamani kuoa tena, japo kutokana na umri wake anapata shinikizo kutoka kwa watoto wake, wakimpinga.
"Nakumbuka rafiki yangu, alipoteza maisha siku tatu tu baada ya kifo cha mkewe, naye akadondoka ghafla na kupoteza maisha, japo sitaki kuamini wengi tunapofiwa nasi tunaondoka, lakini najiona siwezi peke yangu," amesema.
Kwa upande wa Asha Matata wa Kibaha, amesema alimpoteza mumewe miaka 12 iliyopita kutokana na shinikizo la damu, akiacha watoto watatu waliokuwa bado wanasoma.
"Lilikuwa pigo zito kwangu kulinda familia na kuhakikisha watoto hawakwami, wiki kadhaa baada ya msiba wa mume wangu nilijiambia kukaa na kulia hakutalipa ada wala kuleta chakula mezani, nikakubali hali halisi na kuanza upya," amesema.
Simulizi ya Asha, haina toifauti na ya Maria Deus (48), mkazi wa Arusha aliyepoteza mumewe miaka minane iliyopita, akibainisha kuwa uwezo wa wanawake kujihudumia katika mambo ya kila siku, ndiyo ulimpa ustahimilivu baada ya kifo cha mumewe.
"Kabla hata ya msiba huo, tayari nilikuwa nikipanga ratiba zote za nyumbani kuanzia chakula, usafi mpaka usimamizi wa watoto, niliumizwa na kifo cha mwenzangu lakini nilikubaliana na hali halisi, nikafuta machozi na kuendesha maisha ya kila siku hadi wanangu wameweza kujitegemea
Swali ni je, simulizi za wajane na wagane zinaweza kutumika kuthibitisha suala hilo wa kisayansi?
Wataalamu wa afya, saikolojia na sosholojia wanaeleza namna wanaume na wanawake wanavyokabiliana na changamoto za huzuni, mtindo wa maisha na usimamizi wa afya ya mwili na akili baada ya kufiwa na wenza, jambo linalosaidia wanawake kuwa imara zaidi.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ambaye pia ni mshauri wa saikolojia na jamii, Daniel Sendoro amesema mjane kuishi zaidi ya mgane baada ya kufiwqa ni nadharia iliyojengeka kijamii na si matokeo ya utafiti.
“Nadharia hiyo imekuwepo kutokana na mahusiano ya ndoa Afrika, ambapo mama ndiye anayebeba majukumu mengi katika kutunza familia kuliko baba, hata kama baba ndiye anayelea kwa kuleta mkate wa kila siku,” amesema.
Amesema katika familia nyingi, mke anapofariki, mume huzidiwa na namna ya kuongoza na kusimamia nyumba yake, hali inayoweza kumsababishia msongo wa mawazo. Hivyo, kama ana changamoto nyingine za kiafya, nazo huongezeka na kufikia kumfanya akose utulivu.
“Hapo anaweza kuamsha magonjwa mengine yaliyokuwa yamelala. Hicho ndicho kinachowakuta wanaume. Lakini kisaikolojia hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa kihisia na kiakili, anasema.
Hata hivyo, anasema kijamii, katika majukumu ya kuendesha familia, mwanamke huwa na moyo mkubwa, ndiyo maana wengi hata wanapofiwa na wenza wao huweza kustahimili,” amesema.
Mchungaji Sendoro anabainisha kuwa changamoto hiyo huwakumba zaidi wanaume wenye umri wa miaka 50 na kuendelea kuliko wale walio chini ya umri huo.
Daktari wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Lotalus Gadau amesema mfadhaiko na msongo wa mawazo unaotokana na kupoteza mwenza au kupitia mapito mazito ya maisha, una mchango mkubwa katika kuchochea magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
“Hali hii huweka afya ya mtu kwenye hatari kubwa zaidi. Japo wanawake mara nyingi huwa wepesi kufunguka, kuomba msaada wa kisaikolojia na kuzungumza kuhusu changamoto zao, jambo linalowasaidia kupata ahueni mapema, tofauti na wanaume ambao mfumo wa kijamii umewajenga kujikaza na kukaa kimya,” amesema.
“Usiri huu huwafanya wengi wao kuumia kwa ndani na kuathirika zaidi na msongo wa mawazo,” anaongeza.
Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Ahadi Mental Health, Anna Jengo amesema kila binadamu hupitia changamoto za afya ya akili, na si dhambi kupitia changamoto hizo.
“Afya ya akili ina sababu nyingi. Hata kufiwa na mwenza kunaweza kusababisha msongo wa mawazo ambao ukizidi unaweza kusababisha ugonjwa wa sonona,” amesema.
Kuhusu nani huathirika zaidi akipoteza mwenza kati ya mjane na mgane, Anna amesema hilo hutegemea mazingira ya mhusika, kwa kuwa binadamu wameumbwa na kulelewa tofauti, hivyo uwezo wao wa kuhimili matatizo ya aina hiyo hutofautiana.