Ukonga walia ubovu wa barabara, Tarura yaahidi neema

Mwendesha bodaboda akipita kwenye barabara ya Virobo iliyopo Kata ya Chanika, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Picha na Pamela Chilongola
Muktasari:
- Tarura mkoa wa Dar es Salaam imesema zabuni nyingine wanatarajiwa kuzitangaza Julai mwaka huu kupitia mradi wa DMDP na wanatarajia kuboresha zaidi ya kilometa 120 za barabara.
Dar es Salaam. Wakati wananchi wa jimbo la Ukonga wakilalamikia ubovu wa barabara, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), umedai chanzo cha tatizo hilo ni baaadhi ya wananchi kujenga kwenye njia za asili zinazopitisha maji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Februari 20, 2024, wananchi hao wamesema barabara hizo ni mbovu na mvua zinaponyesha maji kutuama barabarani na kutengeneza madimbwi makubwa.
Wamesema hali hiyo inasababisha daladala kukatisha safari zake, huku wengine wakitozwa nauli ya juu kuanzia Sh1,500 hadi Sh2,000.
Rachel Malimbwi, mkazi wa Kibeberu amesema barabara inayoanzia Banana hadi Magole ni mbovu, kwani eneo la Madawa lina madimbwi makubwa ya maji.
“Bajaji nauli zimepanda, mwanzo tulikuwa tukipanda watu wanne kila mmoja alilipa Sh600, lakini sasa nauli imepanda hadi Sh2,500. Tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili,” amesema Rachel.
Mkazi mwingine wa eneo la Kivule, Bukuru Barajogoye amesema kwa kawaida daladala zinazoanzia Kariakoo hadi Hospitali ya Kivule nauli ni Sh800, lakini sasa kutokana na ubovu wa barabara wanatoza Sh1,500 na mvua zikinyesha inapanda mpaka kufikia Sh2,000.
“Dalala hizi wakati mwingine hukatisha safari, madereva hawataki kufika mwisho wakidai barabara ni mbovu,” amesema.
Naye mkazi wa Virobo iliyopo Chanika, Isaya Ismail amesema wanatumia usafiri wa bajaji au bodaboda inaponyesha mvua, huku wakito nauli Sh3,000.
Dereva wa daladala inayefanya safari zake kati ya Banana hadi Mzinga, John Sadan amesema kupanda kwa nauli kunasababishwa na ubovu wa barabara, hivyo hawawezi kukubali gari iingie kwenye madimbwi halafu nauli iwe ndogo.
“Lazima nichukue nauli kubwa kwa kuwa gari ikiharibika niweze kuitengeneza. Barabara ni mbovu kutoka Kitunda kwenda Magole au Mzinga, ina madimbwi makubwa. Tunachukua nauli kuanzia Sh1,000 hadi Sh1,500 inategemea na hali inavyokuwa siku hiyo,” amesema Sadan.
Amesema barabara zikitengenezwa watatumia nauli zilizopendekezwa na Serikali Sh600.
Kauli ya Tarura
Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga amesema barabara katika jimbo la Ukonga zimeharibika kutokana na baadhi ya wananchi kujenga kwenye njia za asili zinazopitisha maji, jambo linalosababisha maji kutuama barabarani.
Amesema kutokana na hali hiyo, Tarura hawana sehemu ya kuyatoa maji yaliyotuama kwenye barabara, hivyo inahitajika mradi mkubwa ili kuyaondoa maji hayo.
“Changamoto hii inahitaji mradi mkubwa, si mradi mdogo wa kuchonga na kuweka kifusi kwenye barabara,” amesema Mkinga.
Mkinga amesema baadhi ya barabara ikiwemo ya Banana kwenda Mwanagati na Mzinga itaingia kwenye awamu nyingine ya mradi wa DMDP zinayotarajiwa kujengwa Julai mwaka huu, hivyo wataendelea kuzichonga na kuweka vifusi ili kurahisisha upitaji wa watu pamoja na kupitisha kiurahisi mizigo inayosafirishwa na vyombo vya moto.
Amesema barabara zenye uhitaji mkubwa kwenye jamii wamezipa kipaumbele na wanatarajia kuziboresha kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam (DMDP) na katika awamu ya kwanza zaidi ya kilometa 150 zitajengwa kwenye wilaya zote na utekelezaji unatarajiwa kuanza Mei, 2024.
Alitolea mfano wa baadhi ya barabara za wilaya ya Ilala zitakazoboreshwa ikiwemo ya Banana, Kitunda, Kivule hopitali, Barakuda, Chang’ombe, Bombambili, Vingunguti, Kigilagila na Msongola na kwa wilaya ya Temeke kuna Gombe, Basir, Keko Machungwa, Kilimahewa na Tuangomama, Kizota, Madizini na Masaki.
Kwa upande wa wilaya ya Kinondoni ni Amri, binti Matora,Tegeta,Togo, Mivumoni, Makalekwa na Togo umoja na wilaya ya Kigamboni barabara ya Dege mbata, Full shangwe, Gezaulole na Edd.
Mkinga amesema zabuni nyingine wanatarajiwa kuzitangaza barabara zaidi ya kilometa 120 Julai, mwaka huu, hivyo wanatarajia kutengeneza kilometa 270 za barabara ambazo walikubaliana kuzipa kipaumbele walipokutana na watumiaji pamoja na viongozi.