Ukinunua umeme mwezi Agosti unakatwa Sh2, 000

Muktasari:
- Shirika la Umeme (Tanesco) limetangaza kuanzia Agosti 2021, mteja atatakiwa kununua umeme wa zaidi ya Sh2,000 ili alipe kodi ya majengo ya Julai na Agosti.
Dar es Salaam. Shirika la Umeme (Tanesco) limetangaza kuanzia Agosti 2021, mteja atatakiwa kununua umeme wa zaidi ya Sh2,000 ili alipe kodi ya majengo ya Julai na Agosti.
Utaratibu huo unatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza utaratibu mpya wa ukusanyaji kodi ya majengo kupitia ununuzi wa umeme kuanzia Agosti 20.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 21,2021 kupitia ukurasa wa Twitter wa shirika hilo imeeleza kuwa; “Ili mteja aweze kupata umeme kwa mwezi Agosti tunakushauri ununue umeme wa zaidi ya Sh2,000 kwa ajili ya kulipa kodi ya majengo ya Julai (Sh1,000) na Agosti (Sh1,000)”
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wametoa maoni tofauti kupitia mtandao huo.
Mtumiaji wa mtandao huo anayeitumia jina moja la Ambakisye ameandika; “Mimi napoishi tuna mita sita nyumba moja. Nashauri watafute njia nyingine au mwenye nyumba apeleke namba za mita za wapangaji wake ili zisikatwe kodi akatwe mwenye nyumba tu.”
Soma zaidi: Utaratibu mpya kodi ya majengo
Kwa upande wake, Chulendagula amesema tatizo ni kumkata mpangaji kodi ya jengo. “Nadhani serikali waweke njia kwenye mfumo wao wa malipo iingizwe hati namba ya nyumba ili ikiwa nyumba inavyumba zaidi ya kimoja na wanamita tofauti tofauti isikatwe mara mbili kwa wakati mmoja.”
Tamko la TRA
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata imesema kila jengo la kawaida lililopo ndani ya kiwanja litalipiwa Sh12,000 badala ya Sh10,000 ya awali na Sh60,000 kwa kila sakafu ya ghorofa kutoka Sh50,000 ya mwanzo. Kwa halmashauri za wilaya na miji midogo, nyumba za ghorofa zitatozwa Sh60,000.