Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukata unavyoliandama Bunge la Afrika Mashariki,Spika alia

Muktasari:

  • Spika wa Bunge la Afrika Mashariki amekiri kuwepo na changamoto za kifedha na kusema shughuli za Bunge hazijasimama

Dar es Salaam. Siku tatu baada ya kuahirishwa kwa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Spika wa Bunge hilo, Joseph Ntakirutimana amesema hakuna shughuli za Bunge hilo zilizosimama licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili jumuiya hiyo.

Ntakirutimana amebainisha hayo baada ya kutafutwa na Mwananchi kufafanua kuhusu athari zitakazojitokeza baada ya kufanyika kwa uamuzi wa kuahirisha vikao vya Bunge na kama shughuli nyingine za uendeshaji wa Bunge zimeathirika, ndipo akaandika taarifa yake.

Februari 7, 2025, Ofisa Habari Mwandamizi wa Eala, Nicodemus Ajak alitoa taarifa za kuahirishwa kwa vikao vyake kwa muda usiojulikana kutokana na changamoto za kifedha.

Upungufu huo wa kifedha umetokana na baadhi ya nchi wanachama kushindwa kulipa michango yao, jambo lililosababisha kushindwa kufanyika kwa vikao vya Bunge vilivyokuwa vimepangwa kuanza Januari hadi Juni 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Ajak, uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Kamisheni ya Eala na viongozi wa kamati kilichofanyika Februari 6, 2025.

Alieleza kwamba uamuzi huo ambao unahusisha shughuli zilizopangwa kutoka Januari hadi Juni 2025, umetokana na tathmini ya hali ya kifedha ya Bunge iliyofanywa katika kikao cha Kamisheni ya Eala na viongozi wa kamati kilichofanyika.

Hata hivyo, katika taarifa yake ya leo Februari 10, 2025, Spika Ntakirutimana amebainisha kwamba hakuna shughuli za Eala zilizosimama na kwamba anawahakikishia wadau kwamba Eala imejitoa kufikia ajenda ya utengamano, usimamizi na uwakilishi.

“Napenda kufafanua kwa umma wa Afrika Mashariki kwamba hakuna shughuli za Eala zilizoahirishwa licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili Jumuiya. Vyombo vya EAC vinavyohusika vimelichukua jambo hili, na kama ilivyokuwa zamani, wanashauriana ili lishughulikiwe.

“Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuwahakikishia wadau wetu kwamba Eala itaendelea na dhamira yake ya kufikia ajenda ya utengamano kupitia sheria, usimamizi, na uwakilishi wa watu wa Afrika Mashariki katika nia ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa,” amesema Spika Ntakirutimana katika taarifa yake.

Akizungumzia jambo hilo, Dk Ngwaru Maghembe ambaye ni katibu wa wabunge kutoka Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki, amekiri kwamba ni kweli Bunge hilo limeahirishwa kutokana na kukosekana kwa fedha ambazo ni michango ya nchi wanachama.

Hata hivyo, Dk Maghembe amesema Tanzania na Kenya zimelipa michango yao kwa asilimia 100 na kwamba Uganda nao hawako mbali.

“Kama tunataka kuelimisha jamii, ni muhimu wajue kwamba nchi yao imetimiza wajibu…Desemba hapa wamelipa kikamilifu. Tangu Mama Samia amekuwa Rais, inalipwa once off (mara moja)” amesema mbunge huyo wa EALA.

Amesema kazi kubwa wanazozifanya ni usimamizi wa miradi kwa kuangalia thamani ya fedha na kama ina malengo ya kuboresha mtengamano. Kwa hiyo, amesema kama Bunge halitakuwepo kufanya kazi, miradi inayoendelea haitaangaliwa au kusimamiwa.

“Kazi yetu ya pili ni kupitisha bajeti ya jumuiya. Haijawahi kutokea kwenye miaka yangu saba ya ubunge, kwamba fedha zikakosekana mpaka bajeti haipitishwi, lakini inawezekana, kwa sababu sasa mchakato wa bajeti unapaswa kuwa umeanza,” amesema Dk Maghembe.

Ameongeza kuwa athari za kukosekana kwa fedha zilikwenda hadi kwenye kamati za Bunge ambapo anasema hawakufanya shughuli za kamati zilizopangwa kufanyika Januari na Februari kwa sababu hakukuwa na fedha.

Kwa upande wake, Ofisa Habari Mwandamizi wa EAC, Simon Owaka amebainisha kwamba shughuli za sekretarieti zinaendelea kama kawaida, hata hivyo hakutaka kuzungumzia zaidi jambo hilo, akisema Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva ndiyo mwenye mamlaka.

“Shughuli za sekretarieti (ya EAC) zinaendelea kama kawaida,” amesema.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa EAC ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameeleza kwamba kwa kawaida michango ya nchi wanachama inatumika kwa ajili ya shughuli za uendeshaji, kulipa mishahara wafanyakazi, kulipa bili mbalimbali, posho au matibabu.

Amesema fedha hizo ambazo ni takribani asilimia 66, hazitumiki kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara, bali fedha za miradi zinagharamiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

“Haijawahi kutokea wafanyakazi wasilipwe mshahara ndani ya mwezi, inaweza ikachelewa tu, labda ikalipwa tarehe sita huko,” amesema ofisa huyo.