Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujenzi Uwanja Ndege Msalato wasababisha hasara ya Sh6 bilioni

Muktasari:

  • Dosari zilizokutwa katika ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, umelisukuma Bunge kuja na maazimio matatu ambayo Serikali imechukua ikiahidi kuyafanyia kazi.

Dodoma. Bunge la Tanzania limeazimia mambo matatu kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ikiwemo kufanya tathmini ya kina ya hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu na kuweka uwajibikaji wa gharama zilizozalishwa kwa pande zinazohusika na mkataba.

Bunge limeazimia hayo leo Jumatano, Februari 12, 2025 baada ya Naibu Spika, Mussa Zungu kuwahoji wabunge wanaoafikiana na mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambapo wengi wao walijibu ‘ndiooo.’

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mwenyekiti wa PAC, Nagenjwa Kaboyoka kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025 na wabunge kupata fursa ya kuijadili kabla ya kufikia maazimio.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Kaboyoka amesema ukaguzi wa kiufundi wa ujenzi wa uwanja wa Msalato umebainisha changamoto kadhaa katika utekelezaji wa mradi huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Nagenjwa Kaboyoka akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo leo Februari 12,2025 bungeni Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Amezitaja dosari katika uandaaji wa mipango na usanifu wa mradi, usimamizi wa mikataba, manunuzi na kuchelewa kwa malipo.

Mwenyekiti huyo amesema changamoto hizo zilizobainishwa hapo awali zina athari za kifedha kwa Serikali ikiwa ni pamoja na ongezeko la gharama za ujenzi kwa Sh6.97 bilioni kutokana na sababu mbalimbali.

Pia ametaja athari nyingine ni adhabu ya riba ya Sh322.721 milioni kutokana na kuchelewa malipo kwa wakandadarasi.

Amesema kuchelewa mchakato wa kumpata mkandarasi wa pili (wa ujenzi wa miundombinu ya majengo mbalimbali) hali ambayo itaongeza gharama.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia Serikali ifanye mapitio ya vipengele vya mikataba ya makubaliano ya ufadhili ili kuweka usawa wa malipo ya gharama zinazoongezeka kwa kuhakikisha upande uliosababisha ongezeko hilo unawajibika,” amesema.

Ameshauri Bunge likiazimia, Serikali ihakikishe Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanasimamia kikamilifu mradi na kufanya tathmini ya kina kuhusu hasara zilizotokana na dosari za awali za usanifu na kuweka uwajibikaji wa gharama zilizozalishwa kwa kila upande.

Pia amesema Tanroads ihakikishe kazi zilizoongezeka na zitakazoendelea kuongezeka zinaidhinishwa na bodi ya zabuni kwa mujibu wa masharti ya mikataba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kudhibiti ongezeko la gharama.

Kaboyoka amesema gharama za ujenzi wa mradi huu ilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 329.47 milioni.

Aidha, amesema makubaliano ya muundo wa ufadhili wa mradi huo yalifanyika Machi 13, 2020 ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ilikubali kutoa mkopo wa Dola za Marekani 271.63 milioni na Serikali ilitarajiwa kuchangia Dola za Marekani 57.84 milioni.

Mwenyekiti huyo amesema matokeo ya ukaguzi huo wa kiufundi, yamebaini kutumika kwa wahandisi ambao hapo awali hawakuwa wamesajiliwa na mamalaka husika za kitaalamu.

Amesema ukaguzi ulibaini kuanza ujenzi wa majengo bila ya kuwa na hatimiliki na vibali vya ujenzi na kuwa jambo hilo lilikuwa kinyume na matakwa ya kanuni ya namba nne ya kanuni za ujenzi wa Mipango Miji ya mwaka 2018.

Amesema kanuni hiyo inahitaji ujenzi wowote kupata kibali cha ujenzi kinachotolewa na mamlaka ya upangaji kulingana na michoro ya ujenzi iliyoidhinishwa na mamlaka ya mji husika.

Amesema ukaguzi ulibaini changamoto katika upembuzi yakinifu wa kina hali iliyosababisha ongezeko la Sh3.04 bilioni.

Amesema sehemu ya 3.3 ya mwongozo wa usanifu wa kijiometri wa barabara wa Wizara ya Ujenzi wa mwaka 2011, unaelekeza upembuzi yakinifu kufanyika kwenye masuala ya hali ya udongo, kiwango cha mteremko kwenye eneo la mradi, gharama za ujenzi na uchaguzi wa njia ya kupitisha barabara.

Aidha, amesema tofauti katika vipimo hivi ilitokana na mbinu iliyotumika wakati wa upembuzi yakinifu ambapo ndege nyuki (drones) zilitumika kupima mwinuko wa usawa wa ardhi bila kusafisha eneo la mradi, hivyo kutotafsiri kwa usahihi kuwa usawa wa vichaka kama ndiyo usawa wa ardhi.

Amesema hali hiyo ilisababisha kuathiriwa kwa utekelezaji wa mradi kutokana na tofauti kati ya viwango halisi vya mwinuko na viwango vya michoro.

“Ukaguzi ulibaini kuwepo kwa ongezeko la malipo ya Sh5.729 bilioni kwa mkandarasi kwa kazi ambazo hazikuidhinishwa na bodi ya zabuni,” amesema.

Amesema mabadiliko hayo yalitokana na changamoto katika usanifu na dosari ya vipimo vya usawa wa ardhi wakati wa upembuzi yakinifu wa topografia.

“Ukaguzi ulibaini kucheleweshwa kwa malipo ya mkandarasi wa kazi za ujenzi wa miundombinu na kusababisha malipo ya riba ya Sh303.814 milioni, hadi kufikia hati namba tisa ya mkandarasi wa kifurushi cha kwanza.

Malipo ya mradi yalicheleweshwa kwa muda wa kati ya siku nane hadi siku 70, hali hii ilipelekea gharama zilizotokana na riba kuongezeka,” amesema.

Aidha, amesema Serikali ilitakiwa kulipa riba hizi kulingana na makubaliano yake na AfDB na ukaguzi ulibaini katika mchakato wa ununuzi na Wakala wa Barabara Tanzania iliidhinisha ombi la mapendekezo ya mradi (RFPs)5 ambayo hayakukamilika.

Maombi hayo yalikosa maelezo muhimu kama vile mawanda ya kazi, michoro ya mradi na vipengele vya ongezeko la thamani na viwango vya ubora wa mradi.

Amesema hali hiyo ilisababisha zaidi ya maombi ya ufafanuzi kutoka kwa wazabuni ambapo nusu yake hayakujibiwa.


Michango ya wabunge

Akichangia, Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya kukosewa kwa usanifu wa miradi ya Serikali, jambo ambalo limeongeza gharama kutokana na riba.

“Mfano ni Uwanja wa Ndege wa Msalato. Wataalamu wetu sijui huwa wanashida gani. Walivyokuwa wakifanya usanifu walikuwa wakitumia drones, zilivyokuwa zikipita kufanya makadirio wakafanya makadirio eneo lisilosawazishwa wala kulimwa, matokeo yake mradi ukaongezeka gharama,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, gharama za ujenzi ziliongezeka zaidi ya Sh5 bilioni ambazo zingeweza kutumika kugharamia miradi mingine ya umma.

Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Stephen Byabato amesema katika uwanja wa Msalato kuna ucheleweshaji wa mradi ambao umeongeza fedha zinazodaiwa na kuwa watapata shida kuzilipa.

Akichangia taarifa hiyo, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndelianga amesema Serikali imeyapokea maazimio yote ya kamati na kuwahikikishia wabunge wizara zote za kisekta zitakwenda kuyafanyia kazi.