Ujasiriamali mwarobaini wa tatizo la ajira nchini

Afisa Mtendaji Mkuu wa Biashara Afrika Mashariki (EABC), Imani Kajula (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabishara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kissanga wakiweka sahihi katika mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi pamoja, Jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa elimu ya fedha pamoja uendeshaji wa biashara umetajwa kama baadhi ya sababu zinazowafanya vijana kushindwa kunufaika na fursa zilizopo katika eneo hilo.
Dar es Salaam. Uwekezaji katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali imetajwa kuwa moja ya suluhisho la kukabiliana na tatizo la ajira nchini haswa kwa vijana.
Kupitia shughuli hizo vijana haswa waliohitimu katika ngazi mbalimbali za kielimu wanaweza kujiajiri na hata kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.
Hata hivyo imeelezwa kuwa upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa elimu ya fedha pamoja uendeshaji wa biashara umetajwa kama baadhi ya sababu zinazowafanya vijana kushindwa kunufaika na fursa zilizopo katika eneo hilo.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Imani Kajula katika hafla ya kusaini makubaliano ya kufanya kazi na Chemba ya Wafanyabishara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Makubaliano hayo ya miaka mitano yamelenga kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo katika ujasiriamali ili kusaidia kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kusaini makubaliano hayo Kajula amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 43 zilizokubali kuanzishwa kwa soko huru la Afrika yaani (afCFTA).
Kajula amesema soko hilo linatoa fursa pana kwa wajasiriamali na wafanyabiashara nchini kunufaika na kutanua wigo wa biashara zao.
Ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa fursa hizo baadhi ya vijana wanashindwa kunufaika au kuingia katika ujasiriamali kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa fedha pamoja na elimu kuhusu masuala ya biashara.
“Ili kutatua changamoto hizo na kuwawezesha vijana kuingia na kunufaika na shughuli za ujasiriamali na bishara kwa ujumla tumeingia makubaliano na TCCIA ili kuwafikia vijana mbalimbali nchini kuwapa elimu pamoja na kuwawezesha kifedha”anasema.
Amesema makubaliano hayo ambayo ni moja kati ya mkakati kukuza ujasiriamali yanalenga kufanya vijana wengi kuwa na ujuzi na kujikita kwenye ujasiriamali.
Hiyo itawawezesha kutumia fursa nyingi zinazotokana na ukuaji wa uchumi na pia soko pana la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Ameongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi sana ambazo zinahitaji jicho la kijasiriamali kuweza kuzitumia, hivyo kuwajengea uwezo wa ujasiriamali vijana utakuza uwezo wao wa kutambua na kutumia vizuri fursa zilizopo na zinazokuja.
“Tunalenga kutengeneza kizazi cha vijana wenye kuona ujasiriamali
kama njia bora ya kujiajiri na hivyo kutoka kuwa waajiriwa hadi kuwa waajiri’’amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Oscar Kissanga amesema ushirikiano huu unaenda kuwapa mafunzo, uzoefu na mbinu vijana ambao ni moja kati ya kundi muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa nchi.
“Elimu hiyo itajikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna sahihi y ya uendeshaji wa biashara, nidhamu ya pesa, uwekaji wa akiba mikopo na mambo mengineyo muhimu katika ustawi wa biashara.
Ameongeza kuwa watawafikia vijana katika maeneo mbalimbali ikiewemo wale waliopo vyuoni.
Kijana Stanley Mahyenga ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa vijana haswa wahitimu
Anasema itawasaidia kupata mwangaza wa wapi kwa kuanzia ili waweze kujiajiri kupitia ujasiriamali.