Ufahamu ugonjwa wa Parkinson na athari zake

Muktasari:
- Siku ya Parkinson Ulimwenguni huadhimishwa Aprili 11 kila mwaka ili kuhamasisha kuhusu ugonjwa wa Parkinson, ambao ni ugonjwa endelevu wa neva za fahamu na kukuza utafiti na kuwasaidia wale waliougua ugonjwa huo.
Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukitarajiwa kuadhimisha Siku ya Parkinson duniani, kesho, ugonjwa huo umetajwa kuathiri neva za fahamu na kuathiri ufanisi wa mwili kwa mgonjwa ikiwemo kushiriki tendo la ndoa.
Siku ya Parkinson Ulimwenguni huadhimishwa Aprili 11 kila mwaka ili kuhamasisha kuhusu ugonjwa wa Parkinson, ambao ni ugonjwa endelevu wa neva za fahamu na kukuza utafiti na kuwasaidia wale waliougua ugonjwa huo.

Miongoni mwa watu maarufu walioishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu ni bondia maarufu, Muhamad Ali ambaye alibainika kuwa na ugonjwa huo mwaka 1984 hadi alipofariki mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 74.
Wengine mwongozaji wa filamu, George Roy Hill, mwasisi wa taifa la China, Mao Zedong, mwigizaji Bob Hoskins, mchezaji na kocha wa zamani, Forrest Gregg na aliyekuwa mbunge na mtia nia wa wa urais wa Marekani, Eugene McCarthy.

Licha ya kwamba ugonjwa huu upo, bado haufahamiki nchini na mtaalamu anaeleza kwamba baadhi ya watu wanawaweka nyumbani wagonjwa wao wakiuhusisha na uzee, hivyo kusababisha ugonjwa huo kukomaa.
Parkinson ni ugonjwa gani?
Kwa mujibu wa jarida la mtandaoni la Mayo Clinic la Marekani, ugonjwa wa Parkinson ni tatizo linalohusiana na mfumo wa neva na linazidi kuongezeka kadri muda unavyokwenda. Mfumo wa neva ni mtandao wa seli za neva zinazodhibiti sehemu nyingi za mwili, ikiwemo mwendo.
Dalili huanza polepole. Dalili ya kwanza inaweza kutetemeka kunaoonekana kidogo kwenye mkono mmoja au wakati mwingine mguu au kidevu. Kutetemeka ni jambo la kawaida katika ugonjwa wa Parkinson.
Ugonjwa huu pia unaweza kusababisha kukakamaa kwa mwili, kupungua kwa kasi ya mwendo na tatizo la kuwianisha mwili, hali inayoongeza hatari ya kuanguka.
Katika hatua za awali za ugonjwa wa Parkinson, uso unaweza usionyeshe dalili kabisa. Mikono yako inaweza isipishane wakati wa kutembea. Uzungumzaji unaweza kuwa chini au wenye kuzongwa. Dalili zinaendelea kuwa mbaya kadri muda unavyokwenda.
Ingawa ugonjwa huu hautibiki, dawa zinaweza kusaidia kupunguza dalili. Wakati mwingine mtaalamu wa afya anaweza kupendekeza upasuaji kusaidia kudhibiti sehemu za ubongo. Upasuaji huu unasaidia kupunguza athari.
Mtaalamu afafanua
Mtaalamu wa Fiziotherapia kutoka Hospitali ya CCBRT iliyopo jijini Dar es Salaam, Dk Andrew Charles anasema Parkinson ni ugonjwa endelevu ambao unasababishwa na tatizo kwenye mishipa ya fahamu hasa kwenye ubongo.
Anasema mishipa ya fahamu inaanza kupungua uwezo wake kwa sababu ya kutumika kwa muda mrefu.
“Kusema Parkinson unaizuia vipi, kuna ugumu hapo, kwa sababu inaenda taratibu, kila siku inaongezeka. Kwa hiyo, ikijulikana mapema, mgonjwa anaweza kupewa dawa,” anaeleza mtaalamu huyo.
Parkinson na mabondia
Dk Swai anasema ugonjwa huo ni wa kijenetiki kwa maana kwamba unarithiwa, hata hivyo anasema hakuna sababu iliyothibitishwa kusababisha ugonjwa huo, ingawa inaweza kuchochewa pia na umri na mazingira.
“Kwa mabondia, pengine wanakuwa wanaushughulisha mwili kupita kiasi kwenye mazoezi, lakini pia wanapata concussion (mtikisiko), kwamba zile ngumu wanazopigwa usoni zinaathiri ubongo.
“Kwa hiyo, minor concussion zinapotokea mfululizo kwa muda mrefu, baadaye wanakuja kupata dalili za Parkinson, lakini specifically (kipekee) sidhani kama wanakuwa na Parkinson kama Parkinson,” amesema.
Ameongeza kwamba wanaweza kuonekana na magonjwa mengine lakini hizo dalili zinazowapeleka kwenye Parkinson. Amebainisha kwamba moja ya dalili za ugonjwa huo ni mtu kutetemeka mikono.
Dk Swai amesema kutetemeka kunasababishwa na vitu vingi, kwa hiyo wataalamu wanaangalia vitu vingine kama vile kukakamaa au mtu kufanya vitu taratibu kuliko kawaida, mfano kutembea au kufanya jambo.
“Wagonjwa wa Parkinson wana aina yao ya kutembea, ukimwona tu unasema hii inawezekana ni Parkinson. Lakini kusema mtu ajikinge vipi na ugonjwa huu, labda kwa kuangalia sababu za kimazingira, kwamba asikae kwenye mazingira yenye sumu hatarishi.
“Ikibainika mapema, tunajaribu kuingilia kati ili kupunguza kasi ya athari zinazojitokeza, wakati huohuo, sisi wanafiziotherapia tunawahudumia hawa wagonjwa ili kuwasaidia balance yao iendelee kuwa nzuri, spidi ya kufanya kazi iendelee kuwa nzuri, pia kumfundisha kutembea kawaida,” amesema.
Hali ikoje Tanzania?
Dk Swai amesema ugonjwa wa Parkinson ni nadra kutokea, hakuna wagonjwa wengi wanaopelekwa katika hospitali, hivyo hawezi kuwa na takwimu za moja kwa moja kuhusu idadi ya wagonjwa wanaowapata.
“Wagonjwa hawaletwi hospitalini kwa sababu wanadhani ni uzee, kwamba mtu anakuwa slow (taratibu), anashindwa kutembea, kwa hiyo watu wanahusianisha na uzee kumbe ni Parkinson,” amesema mtaalamu huyo.
Amesema inawezekana wapo wagonjwa wengi majumbani lakini watu hawaelewi kama ni ugonjwa huo unawakabili. Ameongeza kwamba wagonjwa wa Parkinson huwa wanaandamwa pia na magonjwa mengine.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa dalili za Parkinson kama vile kukosa balance (uwiano) ya mwili na kutembelea polepole kunawafanya watu kuwalaza wagonjwa nyumbani wakiamini kwamba ni uzee.
“Wagonjwa wa Parkinson huwa wanapata depression (msongo wa mawazo) na uoga. Hicho ni kitu muhimu kukifahamu, wanakuwa waoga kupitiliza, wanahisi wataanguka,” amesema mtaalamu huyo.
Parkinson na tendo la ndoa
Dk Swai amesema ugonjwa wa Parkinson unaweza kumpata mtu yeyote lakini kwa kiasi kikubwa uko kwa wanaume na amesema mtu mwenye ugonjwa huo anaweza kushindwa kushiriki tendo la ndoa kama mtu wa kawaida.
Amesema ugonjwa huo unahusisha mifumo ya fahamu na tendo la ndoa linahusika moja kwa moja na mifumo ya fahamu, hivyo kama mifumo hiyo ina tatizo, basi tendo la ndoa haliwezi kufanyika.
“Mishipa ya fahamu ni kama umeme, taarifa zote kwenye ubongo zinapita kwenye mishipa ya fahamu. Kwa hiyo, kukiwa na tatizo lolote kwenye mishipa ya fahamu, msuli wako hautafanya kazi vizuri.
“Sasa, sehemu zetu za siri ni misuli, kwa hiyo bila taarifa kutoka kwenye mishipa ya fahamu kwenda kwenye ubongo, haitafanya kazi, ndiyo maana mtu akipata changamoto yoyote ya mishipa ya fahamu, mwili wote unahusika,” amesema.