Udom yaanza utafiti kusaidia wataalamu wa afya

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (Udom) Profesa Lughano Kusiluka
Muktasari:
- Mradi unalenga kutengeneza mfumo utakaosaidia madaktari na wakunga kutabiri hali ya wajawazito, hivyo kutoa maamuzi yatakayookoa maisha yao.
Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimeanza utafiti utakaowasaidia wataalamu wa afya kutabiri viashiria hatari kwa wajawazito, hivyo kutoa maamuzi yatakayookoa maisha yao na ya watoto.
Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lughano Kusiluka alisema hayo jana alipozindua mradi wa takwimu katika makundi yenye hatari ya afya ya uzazi nchini.
Mradi huo unafanywa na Udom kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Profesa Kusiluka alisema lengo la mradi huo ni kutengeneza mfumo utakaosaidia madaktari na wakunga kutabiri hali ya wajawazito, hivyo kutoa maamuzi yatakayookoa maisha yao.
“Ili kuufanikisha mfumo huo katika hatua ya kwanza ni kukusanya takwimu za kutosha na kisha kutengeza kituo cha takwimu,” alisema.
Mhadhiri wa Ndaki ya Tehama na Elimu Angavu wa Udom, Dk Rukia Mwifunyi alisema mradi huo umejikita katika kutatua changamoto za uzazi kwa wanawake na wajawazito.
“Mara nyingi wanapata changamoto na haijulikani mama atajifungua kwa njia gani, kabla, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua,” alisema.
Alisema mradi huo umejikita katika kuandaa data zitakazotumika kutabiri vihatarishi vinavyoweza kujitokeza wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.
Alisema data hizo zitakusanywa siku ya kwanza wanapoanza na wakati wakiendelea na kliniki, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Taarifa hizo, alisema zitasaidia katika kuandaa moduli itakayotumika kufanya maamuzi ya kujua mama huyo anastahili matibabu ya namna gani.
Pia alisema itasaidia kujua aina ya kituo atakachopaswa kuhudumiwa na vifaa vitakavyotumika kwenye matibabu husika.
Dk Rukia alisema wamechagua wilaya tano kwenye mikoa mitano na kuwa uchaguzi huo umetokana na miundombinu iliyopo katika hospitali na hali ya uchumi ya wananchi kwenye wilaya hizo.
Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Chamwino mkoani Dodoma, Meatu (Simiyu), Mkuranga (Pwani), Mbulu (Manyara) na Kilolo (Iringa).