Uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27

Muktasari:
Tangazo hilo amelitoa leo Alhamisi, Agosti 15, 2024 jijini Dodoma, akisema kampeni za uchaguzi huo zitaanza Novemba 20-26, 2024.
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerewa ametoa tangazo la uchaguzi wa Serikali za mitaa akisema utafanyika Novemba 27, 2024.
Tangazo hilo amelitoa leo Alhamisi, Agosti 15, 2024 jijini Dodoma, akisema kampeni za uchaguzi huo zitaanza Novemba 20-26, 2024.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Adolf Ndunguru ameuhakikishia umma kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki kwa kuwashirikisha wadau wote wa siasa nchini.
“Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imefanya kazi yote ya maandalizi ya uchaguzi ikiwemo kuandaa nyaraka zinazohitajika kwa kushirikisha wadau kwa asilimia 100 hadi tulipofikia.”
“Waziri wakati unatoa tangazo hili utatoa na mwelekeo wa shughuli zitakazofanyika hadi siku ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na tunakuahidi kufanya kazi usiku na mchana kuandaa na kuendesha uchaguzi huru na haki,” amesema.
Ndunguru amesema wamejipanga kuongeza ufanisi na kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ili kuutendea haki uchaguzi huo, uache alama na historia iliyotukuka na kujenga Taifa lenye umoja.