Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: Mahakama yaridhia kufunguliwa kesi kuupinga, yakataa kuusimamisha

Mleta Maombi, Ananilea Nkya (kushoto) akitoka kwa furaha na Wakili, Jebra Kambole (kulia) katika chumba cha Mahakama jijini Dar es Salaam leo, baada ya maombi yao ya kufungua shauri  la kupinga Uchaguzi wa Serikali za mitaa kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tamisemi. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wananchi watatu walifungua shauri wakiomba kibali kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 kusimamiwa na Tamisemi pamoja na kanuni za uchaguzi huo ziliizotungwa na Waziri wa Tamisemi. Mahakama imetoa kibali hicho, lakini imekataa kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo unaoendelea.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeridhia maombi ya wananchi watatu ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kwa lengo la kupinga utaratibu wa uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.

Hata hivyo, Mahakama hiyo imekataa maombi ya amri ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo unaoendelea chini ya kanuni za mwaka 2024, zilizotungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Uamuzi huo umetolewa  leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera, kutokana na shauri namba 19721/2024, lililofunguliwa na wananchi watatu--- mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe, mwenyekiti wa Jukata, Ananilea Nkya na Buberwa Kaiza.

Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 umepangwa kufanyika nchini Novemba 27, 2024. Agosti 15, 2024, Waziri wa Tamisemi ametangaza kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo, kuanzia tarehe hiyo.

Hata hivyo, wananchi hao walifungua shauri hilo wakiomba kibali kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi, wakihoji mamlaka yake.

Pia wanakusudia kupinga uchaguzi huo kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi, badala yake usimamiwe  Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Hata hivyo, wajibu maombi, Waziri wa Tamisemi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliweka pingamizi dhidi ya maombi hayo, wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali wakidai yana kasoro za kisheria, huku walibainisha hoja nne za pingamizi hilo.

Mahakama ilisikiliza pingamizi hilo kwa pamoja na shauri la msingi (maombi ya kibali).

Hivyo, katika uamuzi wake Mahakama imeanza kutoa uamuzi wa hoja za pingamizi, kabla ya uamuzi wa shauri lenyewe la maombi ya kibali.


Uamuzi wa pingamizi

Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo, leo Jumatatu, Septemba 9, 2024 Jaji Dyansobera amekubaliana na hoja za waombaji kuwa hoja za pingamizi hilo hazina mashiko kisheria na akakataa hoja wa wajibu maombi.

Hivyo, ametupilia mbali hoja zote za pingamizi la wajibu maombi akieleza hazikuwa na mashiko ya kisheria.

Amefikia uamuzi huo wa kutupilia mbali pingamizi hilo, baada ya kupitia hoja za pande zote, sheria na kesi rejea mbalimbali na kuchambua kustahili na kutokustahili kwa hoja moja baada ya nyingine.

Baada ya uamuzi wa pingamizi hilo ndipo Jaji Dyansobera akatoa uamuzi wa shauri lenyewe la maombi ya kibali.


Uamuzi wa shauri la msingi

Katika uamuzi wake, Jaji Dyansobera alirejea matakwa ya kisheria kwa mtu anayeomba kibali kama hicho kuona kama waombaji wamekidhi vigezo.

Vigezo hivyo ni pamoja na kufungua maombi hayo ndani ya muda wa miezi sita tangu kutokea kwa jambo au kutolewa kwa uamuzi unaolalamikiwa, ambacho amesema haikuwa kinabishaniwa na pande zote.

Vigezo vingine viwili ambavyo ndivyo vilivyokuwa vinabishaniwa na pande zote kama waombaji wameonekaa kuna hoja inayobishaniwa ambayo inahitaji kujadiliwa na kama wameonekana kuna maslahi mapana katika uamuzi wanazokusudia kuzipinga.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mawakili wa waombaji Mpale Mpoki (Kiongozi wa jopo) na Jebra Kambole wakisaidiwa na Maria Mushi, waliieleza Mahakama kuwa wateja wao wamekidhi vigezo hivyo.

Hata hivyo, jopo la mawakili wa wajibu maombi likiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Mulwambo, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang'a, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Erighi Rumisha na Mawakili wa Serikali, akiwemo Ayoub Sanga wakipinga maombi hayo.

Kwa nyakati tofauti mawakili hao waliieleza Mahakama waombaji wameshindwa kuonyesha na kuithibitishia Mahakama kuwa wamekidhi matakwa hayo ya kisheria kustahili kupewa kibali hicho.

Hata hivyo, Jaji Dyansobera katika uamuzi wake ametupilia mbali hoja za mawakili wa wajibu maombi na badala yake amekubaliana na hoja za mawakili wa waombaji.

Amesema Mahakama imeridhika waombaji wamethibitisha vigezo hivyo viwili kwamba wana hoja ya kujadili na maslahi mapana.

"Kwa hiyo waombaji wana haki ya kupata kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama," amesema Jaji Dyansobera baada ya kujadili kwa ufupi matakwa hayo mawili ya kisheria na kusisitiza:

"Baada ya kusema hayo nimeridhika maombi haya yana msingi, kwamba waombaji wamethibitisha wana haki na ninatoa kibali kwa waombaji kufungua shauri la mapitio kwa mujibu wa Sheria."


Amri ya kusimamisha uchaguzi

Hata hivyo, Jaji Dyansobera amekataa maombi ya kutoa amri ya kusimamisha utekelezaji wa sheria ndogo (kanuni za mwaka 2024 zilizotolewa na Waziri wa Tamisemi) baada ya kuridhika haikuwa miongoni mwa nafuu walizokuwa wameziomba katika nyaraka za kesi walizoziwasilisha mahakamani.

Amesema baada ya kusoma kiapo na hati ya maelezo ya waombaji suala hilo la kusimamisha utekelezaji wa kanuni hizo, halikuwekwa kama moja ya nafuu walizokuwa wanaziomba.

Amesema kwa mujibu wa taratibu za Mahakama Kuu (uendeshaji wa Mashauri) wadaawa wanafungwa na nafuu walizoziomba kwenye nyaraka zao tu.

"Kama kulikuwa na haja ya kusimamisha utekelezaji wa Kanuni zilizotolewa na mjibu maombi wa kwanza (Waziri wa Tamisemi) wangeziweka kwenye hati ya maelezo na kiapo," amesema Jaji Dyansobera.

Hata hivyo, amesema kwenye hatua hii ambayo ndio kesi inaanza ndio muda muafaka maombi kama hayo yanaweza kutolewa kwa sababu wadaawa wanakuwa na nafasi pana ya kujieleza.

"Nina imami kuwa nafuu nyingine ambazo hazikuwepo kwenye maombi ya kibali zinaweza kushughulikiwa kwenye shauri la mapitio ya Mahakama," amesema Jaji Dyansobera


Nje ya Mahakama

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili wa Serikali Mkuu, Deodatus Nyoni amesema wanauheshimu na kwamba jambo jema ni kwamba mchakato mzima wa uchaguzi haujasimamishwa kama mawakili wa waombaji walivyoomba.

Amesema kwa sasa wanasubiri shauri la mapitio ya Mahakama litakalowasilishwa na upande wa pili katika hatua ya pili ili wayafanyie kazi.

"Ukiangalia katika mazingira ya kawaida, maombi ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi, yalikuwa hayapo katika maombi yao ya msingi ya kibali waliyoyaleta," amesema Nyoni.

"Hivyo, wenzetu waliona hayo ndio sehemu ya msingi wanaweza kusimamisha huu mchakato wa uchaguzi."

Kuhusu kutupiliwa mbali mapingazi ya Serikali, Nyoni amesema maombi ya kibali yanakuwa na sehemu tatu, ambayo ni mapingamizi ya awali, kibali chenyewe na kuomba mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa usimame.

"Sisi mapingamizi yetu ya awali tuliyowasilisha mahakakani yalikuwa ya msingi kwa sababu wenzetu walikuwa wana njia mbadala ya kuyawasilisha malalamiko yao, lakini tunaheshimu uamuzi wa Mahakama," amesema Nyoni.

"Pingamizi la pili, tuliona lina shida katika aya karibia 10 hivi, ambapo sisi kama Serikali tuliona zina shida katika kiapo chao kwa sababu kilikuwa hakiendi sambamba na amri ya 19 ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, lakini Mahakama imeona aya kama nne hivi ambazo ni aya ya 10, 15, 17 na 19 kama zilikuwa na shida," amesema.

Kuhusu pingamizi la tatu walilowasilisha dhidi ya waleta maombi, Mahakama ililiona halieleweki na pingamizi la nne, pia Mahakama imeona halina mashiko.

Lakini, Nyoni amesema wao wanaona mapingamizi yao yana maana kwa sababu wakati mtu anatengeneza kiapo lazima kikathibitishe maelezo aliyoyaweka katika hati ya maelezo yake.

Kwa upande wake, Nkya ambaye ni mwanaharakri na mwanahabari mstaafu, mmoja wa waombaji hao amesema wamefungua shauri hilo na kusimamia kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Amesema kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 8 wananchi wamepewa mamlaka ya kuhakikisha shughuli za uchaguzi zinasimamiwa na wananchi.