TFS yaonya uharibifu mikoko, mazingira ya bahari

Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo (kulia) akihutubia katika ufunguzi wa mradi mradi wa Usimamizi wa mikoko uliofanyika jana jijini hapa. Kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la mazingira (WWF), Amani Ngusaru.
Muktasari:
- Shirika la kimataifa la mazingira la WWF linatekeleza mradi wa miaka mitatu la uhifadhi wa miti ya mikoko katika wilaya za Kibiti na Mafia (Pwani) na Wilaya ya Kilwa (Lindi).
Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imewataka wananchi wanaoishi karibu bahari kushiriki katika utunzaji wa mazingira ya bahari ikiwemo miti aina ya mikoko inayoharibiwa kutokana na shughuli za binadamu.
Hayo yameelezwa leo Juni 19 na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo alipokuwa akizindua mradi wa Usimamizi wa mikoko kwa kstahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi na uboreshaji wa maisha ya jamii, jijini hapa.
Uzinduzi huo ulihusisha baadhi ya wanachi kutoka wilaya za Kibiti na Mafia (Pwani) na Kilwa (Lindi).
Profesa Silayo amesema kuwa mikoko ndiyo misitu ya kwanza kutungiwa sheria ya uhifadhi na Wakoloni mwaka 1928 kabla ya kuja kwa sheria nyingine zilizobadilika kwa uhifadhi wa misitu yote.
Amesema wakati robo ya watu wote duniani zaidi ya bilioni saba wakiishi maeneo ya pwani, Tanzania ina fukwe zenye umbali wa zaidi ya kilometa 1,420 kutoka Mkinga (Tanga) hadi pwani ya Mikindani (Mtwara) ambazo kati yake kilometa 800 zina mikoko.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto ya uharibifu wa miti hiyo kutokana na shughuli za binadamu ukiwemo ujenzi karibu na bahari, uchimbaji wa chumvi na uvunaji usiozingatia utaratibu.
“Watu wanapojenga karibu na bahari, wanakata mawasiliano na maji ya bahari. Wanazuia maji ya bahari yasifike kwenye mikoko, wanajaza udongo, vifusi ili wafanye ujenzi, kwa hiyo wanatuibia rasilimali zetu kwa namna ya polepole.
“Kwa hiyo tunawafikishia ujumbe ninyi wanavijiji mnaohifadhi, mnapoona watu wanazuia maji mchukue hatua.
“Mtu amekuja leo na lori amemwaga kifusi, kesho unaona lori jingine, akishamwaga mara tatu mara nne panakuwa siyo bahari tena,” ameonya Profesa Silayo.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa rasilimali watu, rasilimali fedha na utaalamu.
Amesema katika mifumo ikolojia ya misitu, ikolojia ya mikoko ndiyo ina uwezo mkubwa wa kuhimili, hivyo ikiharibiwa na ukapa nafasi, inarejea uwezo wake haraka.
“Ndio maana atunashirikiana na mradi huu ili kurejesha mifumo hii,” amesema.
Awali akimkaribisha Profesa Silayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alisema mradi ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM iliyoahidi uhifadhi wa mazingira.
“Ilani ya CCM pia inazungumzia kuondoa ujinga umasikili na maradhi katika kuwajengea wananchi uchumi.
“Uchumi katika maeneo yetu hasa ya pwani ni pamoja na utunzaji wa mazingira ya bahari ambayo tukiyaacha tunarudi nyuma,” amesema.
Awali akielezea mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), mratibu kutoka shirika la kimataifa la Mazingira la WWF, January Ndagala amesema utawezesha wanajamii kuimarisha usimamizi wa mikoko na kuimarisha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Inatarajiwa kwamba Jamii za ukanda wa pwani zitaendelea kutambua haki na wajibu wao katika
kusimamia na kunufaika na mikoko iliyolindwa na kwamba fursa za maisha na biashara zitaendelezwa kwa jamii za pwani zinazotegemea mikoko nchini Msumbiji na Tanzania,” amesema.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika nchi za Tanzania, Msumbiji na Madagascar kwa miaka mitatu (2023 - 2025).
Amesema katika mradi huo, Tanzania imepokea Sh3.311 bilioni zitakazotumika katika Wilaya za Mafia vijiji vya Jimbo na Kanga, Wilaya ya Kibiti vijiji vya Mchungu na Msindaji na Wilaya ya Kilwa vijiji vya vya Marendego na Somanga.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa WWF Tanzania, Dk Amani Ngusaru amesema kutokana na uhifadhi bora wa maeneo ya pwani, eneo la Rufiji, Mafia na Kibiti (Rumaki) limepandishwa hadhi na Shirika la Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kuwa hifadhi hai katika tathmini iliyofanyika jijini Paris nchini Ufaransa Juni 14, 2023.
“Hiyo kazi ilianza mwaka 2019 na iliratibiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likishirikiana na Wizara mbalimbali na taasisi zote za uhifadhi ikiwemo TFS, TAWA (Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania), MPRU (Hifadhi ya Bahari) na TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa),” amesema