Teknolojia inavyoibadili Mwananchi, AI kuwahudumia wasomaji wake
Picha na Akili Unde.
Muktasari:
- Inayoyafanya Mwananchi kwa wasomaji wake, ‘full dijitali, AI’.
Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), imeeleza katika kipindi hiki sekta ya habari inaendelea kubadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia huku ikiendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kidijitali na matumizi ya akili unde (AI), ili kuwapa wasomaji huduma zinazokwenda sambamba na uhitaji wa sasa.
Mbali na kuendelea kuchapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, kampuni hiyo imepanua huduma zake kupitia majukwaa ya kidijitali yanayomwezesha msomaji kupata habari popote alipo duniani, kuzisoma kwa urahisi, kuzishiriki na hata kuzisikiliza kupitia teknolojia ya AI.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Mpoki Thomson, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuwafuata wasomaji walipo badala ya kusubiri wasomaji wafike kwenye vibanda kunapouzwa magazeti.
Akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM leo Alhamisi Julai 23, 2026, Mpoki amesema kampuni imekuwa kinara wa mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya habari nchini kwa kuanzisha mfumo wa usajili wa kidijitali (digital subscription), unaomwezesha msomaji kulipia huduma za habari kwa siku, mwezi au mwaka.
"Tumekuwa wa kwanza kuweka mfumo wa usajili wa kidijitali kwa sababu tunaamini mustakabali wa biashara ya habari upo kwenye majukwaa ya kidijitali," amesema Mpoki.
Amesema uwekezaji huo umeiwezesha MCL kuwafikia wasomaji waliopo ndani na nje ya Tanzania, bila kulazimika kutegemea upatikanaji wa nakala za magazeti kwenye maduka au vituo vya mauzo.
Kwa mujibu wa Mpoki, kampuni pia hutumia takwimu za usomaji na mwenendo wa hadhira kuelewa uhitaji wa wasomaji wake ili kuzalisha maudhui yanayowagusa zaidi.
"Tunafahamu msomaji wetu yuko wapi, anahitaji nini na anapendelea kupata habari kwa namna gani. Hiyo inatusaidia kuendelea kuboresha huduma zetu," amesema.
Mbali na mfumo wa usajili wa kidijitali, MCL imeanzisha majukwaa ya Mwanaclick na Gazeti Mkononi, yanayomwezesha msomaji kupata habari kwa haraka kupitia simu au vifaa vingine vya kidijitali, huku akipewa nafasi ya kuzishiriki kwa urahisi kama ilivyo kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ubunifu wa Kidijitali wa MCL, Siael Macha, amesema kampuni imekwenda hatua moja mbele zaidi kwa kuunganisha teknolojia ya AI kwenye majukwaa hayo ili kuboresha uzoefu wa wasomaji.
Amesema kupitia teknolojia hiyo, msomaji anaweza kusikiliza habari zikisomwa na AI badala ya kuzisoma mwenyewe, jambo linalowapa urahisi watu wanaokuwa safarini, kazini au wanaofanya shughuli nyingine.
“Ndiyo maana tukienda mbali zaidi kiteknolojia tukaweka na AI kwenye majukwaa hayo ili kumpa urahisi msomaji wetu katika shughuli zake za kila siku anaweza akawa amekaa anatembea au anaendesha gari huku AI inamsomea habari,” amesema.
Hata hivyo, pamoja na uwekezaji mkubwa katika teknolojia, Mpoki amesema haijaondoka kwenye misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mpoki amesema kampuni inaendelea kusisitiza ukweli, usahihi, uwiano na uthibitishaji wa taarifa kabla ya kuchapishwa, akieleza kuwa kasi ya teknolojia haiwezi kuwa sababu ya kupuuza ubora wa habari.
“Ndio maana huwa nawaambia waandishi tusiwe na haraka ya kutaka kuwa wa kwanza kutoa habari, tuhakikishe tuna mifumo ya habari kutoka hatua ya kwanza ya uhakikishaji hadi pale inapotoka,” amesema.
Amesena moja ya sifa zinazotofautisha maudhui ya Mwananchi ni uchambuzi wa kina unaomsaidia msomaji kuelewa si tu kilichotokea, bali pia sababu, athari na mwelekeo wa matukio.
Kwa mujibu wa MCL, mabadiliko hayo yanaakisi namna sekta ya habari inavyoendelea kubadilika, huku kampuni ikiweka mkazo kuunganisha ubunifu wa kidijitali, matumizi ya AI na uandishi wa habari unaozingatia weledi ili kuwahudumia wasomaji wa sasa na wa baadaye.