Tatizo la madawati mwisho Januari 2024

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlimani jijini Mbeya wakishangilia baada ya kupokea madawati 65 kutoka Benki ya Biashara Tanzania (TCB) yaliyokabidhiwa leo Novemba 14 shuleni hapo.
Muktasari:
- Shule ya Msingi Mlimani imesema licha ya kuwa na ufaulu mzuri kitaaluma, lakini inao upungufu wa madarasa 13, madawati 146, ofisi za walimu, matundu ya vyoo 29 na kuomba Serikali na wadau kumaliza tatizo hilo.
Mbeya. Halamshauri ya Jiji la Mbeya imesema hadi Januari 2024, upungufu wa madawati katika shule zote za msingi jijini humo utakuwa umemalizika, huku ikiahidi kuendelea kutafuta wadau ili kumaliza changamoto nyingine za miundommbinu.
Akizungumza leo wakati akipokea madawati 65 yaliyotolewa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika Shule ya Msingi Mlimani, Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson amesema tayari Halamashauri hiyo imeazimia kufikia Januari, 2024 tatizo la madawati kwa shule zote za msingi jijini humo litabaki historia.
Amesema wanafahamu zipo changamoto nyingi kwenye shule za msingi lakini tayari Halmashauri hiyo chini ya mkurugenzi na Meya wa Jiji, wameshaazimia na tayari zipo hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwamo kukarabati shule chakavu.
“Ndio maana katika shule hii ilipewa Sh30 milioni kwa ajili ya ukarabati wa madarasa mawili, ofisi na vyoo, lakini mkakati wetu ni ifikapo Januari mwakani hakutakuwapo changamoto ya madawati,”
“Niwapongeze walimu wa shule hii mnajitahidi sana kutoa elimu licha ya mazingira magumu, hizi kero nyingine nitazungumza na wadau wengine kuona tunazitatuaje,” amesema Dk Tulia ambaye ameahidi mifuko 200 ya simenti shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo, Baitha Sanga amesema hadi sasa wanao upungufu wa madarasa 13 madawati 146, matundu ya vyoo 29 na uchakavu wa madarasa kwa wanafunzi 1,096 waliopo shuleni hapo
“Pamoja na changamoto hizo, lakini shule yetu imekuwa na ufaulu mzuri kwani kwa miaka mitatu mfululizo tumepanda kuanzia asilimia 87 hadi 96, kwa sasa wananchi wameanza kujitolea kujenga shule na wapo hatua ya boma tunahitaji sapoti,” amesema Baitha.
Kwa upande wake Meneja wa benki hiyo tawi la Mwanjelwa, Simon Mlelwa amesema walipokea maombi kufuatia changamoto hiyo, hivyo walichokitoa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.
“Tunafahamu mahitaji ni mengi lakini tulichoweza kwa kuguswa kwenye elimu katika kurudisha kidogo kwa jamii tumeweza kukabidhi leo madawati 65 yenye thamani ya Sh 5 milioni,” amesema Mlelwa.