Tanzania yajenga vituo vinne vya umahiri

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga akizungumza katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Dodoma kinachojengwa eneo la Nala jijini Dodoma.
Muktasari:
Katika kuhakikisha Tanzania inapata wataalam wa kutosha katika uchumi wa viwanda, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendesha ujenzi wa vyuo vya ufundi mbalimbali ikiwemo vituo vinne vya umahiri.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imetenga zaidi Dola za Marekani milioni 75 katika ujenzi wa vituo vinne vya umahiri vitakavyozalisha wataalamu wa kada mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme Jadidifu na usafirishaji wa anga, majini na reli.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Februari 28, 2022 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati wa ziara ya kukagua miradi ya wizara hiyo jijini Dodoma.
Kipanga amekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Dodoma kilichopo katika kata ya Nala na Shule ya Mfano ya Iyumbu iliyopo katika kata ya Iyumbu.
Amesema vituo hivyo vya umahiri ni kinachojengwa Jijini Arusha ambacho kitajikita katika kuzalisha wataalam wa nishati jadidifu na Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam (DIT) wanajenga chuo kitakachotoa mafunzo ya Tehama.
Vingine vitajengwa katika Chuo cha Usafirishaji (NIT) cha jijini Dar es Salaam ambacho kitahusika na usafirishaji katika anga, reli na majini na Mwanza ambacho kitahusika na masuala ya ngozi.
“Kwa mara ya kwanza nchi yetu tutazalisha marubani wetu wenyewe lakini mnafahamu tunareli yetu ya mwendo kasi (SGR) tunaenda kuzalisha vijana wahandisi watakaotumika katika reli hiyo,”amesema.
Kuhusu ujenzi wa chuo cha ufundi Dodoma, Kipanga amesema mradi huo ulioanza Juni mwaka jana unahusisha ujenzi wa majengo 18 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo ikikamilika unatarajiwa kuchukua wanafunzi 600 na wanafunzi 1500 ujenzi wote ukikamilika.
Pia amesema wamemwagiza mkandarasi kuhakikisha kuwa anaongeza idadi ya mafundi kuhakikisha ujenzi unaendelea katika majengo yote ya mradi huo.
Kuhusu Shule ya Mfano Iyumbu, Kipanga amesema ujenzi wa shule hiyo ambayo itachukua wanafunzi 1,000 wa kidato cha kwanza hadi cha sita ulipaswa kukamilika Februari mwaka huu lakini kutokana na sababu mbalimbali ulishindwa kukamilika kwa muda huo.
“Lakini niahidi hapa mbele yenu changamoto zote ambazo zimesababisha kuchelewa kwa mradi huo tutazifanyia kazi ambapo Ijumaa (Machi 4) tutakuwa na kikao cha kuzijadili changamoto zote ambazo zimesababisha mradi kuchelewa,”amesema.