Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kubeba ajenda ya vijana, wenye ulemavu mkutano UN

Balozi  Noel Kaganda (katika) akipokea vitabu vya mawasilisho ya maoni.

Muktasari:

  • Makundi ya vijana na watu wenye ulemavu yamejadili na kupokea mapendekezo yakiwemo ya kutaka yashirikishwe katika mikutano muhimu ya Umoja wa Mataifa ili kutatua changamoto zao.

Dar es Salaam. Ushirikishwaji wa vijana na watu wenye ulemavu ni miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa na yatakayowasilishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uitwao Summit of the Future, utakaofanyika nchini Marekani Septemba 22 hadi 23, 2024.

Hayo yameelezwa leo Septemba 6, 2024 wakati wa ukusanyaji maoni ya kupeleka kwenye mkutano huo unaohusisha asasi za kiraia, makundi ya vijana na watu wenye ulemavu.

Summit of the Future ni mkutano wa ngazi za juu, unaowaleta pamoja viongozi wa dunia ili kuunda makubaliano mapya ya kimataifa ya jinsi kuleta maendeleo ya sasa na kulinda maisha ya baadaye.

Mwakilishi wa jopo la vijana nchini, Caren Khan, amesema kiu yao ni kutaka kuona vijana wanashiriki kikamilifu katika mikutano ya Umoja wa Mataifa, kwani wamekuwa wakiwakilishwa na watu wasio vijana, ambao hawajui mahitaji yao.

Caren amesema pia wanataka kushirikishwa katika vikao vya Baraza la Ulinzi na Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Kuna masuala ya vijana kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi na hasa kujisemea mahitaji yao na kuona yanafanyiwa kazi katika umoja huo ndiyo tunayotaka," amesema.

Katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago amesema kati ya mapendekezo waliyoyatoa ni ushiriki mpana wa watu wenye ulemavu katika kufanya maamuzi.

"Pia tumetaka uwepo wa miundombinu rafiki kwenye huduma za kijamii, ikiwemo usafiri wa umma, majengo na na kupewa nafasi ya kuwasilisha matatizo yetu,” amesema.

Akizungumza baada ya utoaji wa maoni hayo, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda, amewahakikishia kuwa watakuwa mstari wa mbele kuzungumza kwenye mkutano huo na mengi yatakuwa maoni yaliyotolewa na wananchi.

"Kuhusu suala la Tanzania kushiriki katika mchakato huo, niwahakikishie Watanzania hatutakuwa watazamaji tu tutakapofika huko kwa kuwa tunajua kinachoenda kujadiliwa ni kuhusu mustakabali wa dunia ambao pia ni mustakabali wa nchi yetu," amesema Balozi huyo.

Amesema hatua ya wananchi kushirikishwa kutoa maoni, ni kielelezo cha dhamira njema ya Serikali inavyothamini maoni, mitazamo katika michakato ya kisera ya ndani na nje ya nchi.

"Yote haya ni kuhakikisha kunakuwepo na ushirikishwaji na hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma, sio tu kutoa mawazo bali pia kwenye michakato ya kisera na kimaamuzi," amesema.

Awali mwakilishi wa UN Tanzania, Shabnam Mallick, amesema moja ya mafanikio waliyoyapata ni kutengeneza ushirikiano na vijana katika mapendekezo, kuwatia moyo na kuwawezesha wwatu wenye ulemavu kupaza sauti.

Mkurugenzi wa Asasi ya Vijana wa UN Tanzania, Ibrahim Mwenda, amesema katika mchakato huo, wameshirikisha asasi zaidi ya 500 kukusanya maoni.