Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania, Kenya zatakiwa kutekeleza sera zao za kilimo

Mshauri wa Masuala ya Mabadiliko ya tabia nchi kutoka Shirika la Vi Agroforestry Dk, Monica Nderuti (mwenye fulana nyeusi) akiongea na wanahabari.

Muktasari:

  • Uganda imeshauriwa kutunga sera ya kilimo misitu ili ianze kutekelezwa nchini humo kwa masilahi ya wakulima hasa waishio katika maeneo kame.

Musoma. Mtandao wa Vikundi vya Kilimo vya Uswis (Siani) umeziomba Serikali za Tanzania na Kenya kuanza utekelezaji wa mipango iliyopo kwenye sera za kilimo za nchi kuhusu kilimo misitu, ili kuweza kuwanufaisha wakulima na wananchi wa nchi hizo mbili.

Pia, mtandao huo umeiomba Serikali ya Uganda kutunga sera ya kilimo misitu ili ianze kutekelezwa nchini humo kwa masilahi ya wakulima hasa waishio katika maeneo kame.

Wito huo umetolewa mjini Musoma leo Novemba 11, 2025 na wana mtandao hao walipokuwa wakizungumza  na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano la kilimo misitu, lililoandaliwa na mtandao huo ambao una wanachama katika nchi hizo tatu.

Wamesema uwepo wa sera ya pamoja kwa nchi hizo kutasaidia kutekeleza kwa pamoja suala la kilimo mseto hivyo kuwa na matokeo chanya kwenye suala zima la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, na kuboresha hali ya uchumi kwa wananchi wa nchi hizo.

Mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Shirika la Vi Agroforestry, Dk Monica Nderuti amesema kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyoikumba dunia nzima, nchi hizo tatu zinapaswa kuwa na sera ya pamoja ya kilimo misitu.

Amesema pamoja na mambo mengine, sera hiyo itasaidia kuboresha kipato cha watu pamoja na kupambana na madhara yatokanayo na mabadiliko hayo.

“Kutunga sera ni jambo moja na kutekeleza ni jambo jingine tunashukuru Tanzania tayari wametunga sera hii  ya kilimo misitu mapema kidogo. Kenya pia wameitunga Septemba sasa tunaomba utekelezaji wake uanze na kwa Uganda nao pia wanapaswa kutunga sera hiyo ili kutimiza malengo na wakati ni sasa,” amesema.

Amesema sera ya kilimo misitu pamoja na mambo mengine inahusisha kilimo cha mazao na miti rafiki hasa katika maeneo yenye ukame na hali ya ukame ipo kwa kiasi kikubwa kwa nchi hizo tatu.

Amesema faida za kutekeleza sera ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli mahususi za kilimo misitu kwa nchi hizo.

Elizabeth Githendu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, amesema suala la ushirikishwaji wa wanawake katika utekelezaji wa sera hiyo ni la muhimu, ambapo mbali na kuleta usawa kijinsia lakini pia litasaidia kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo kwani wanawake wengi wanajihusisha na kilimo katika nchi hizo.

“Kwanza wanawake ni kundi ambalo lina watu wengi kwenye nchi hizi lakini pia wengi ndio wanajihusisha na kilimo kuanzia ngazi ya familia lakini bado hawajashirikishwa vema kwa hiyo tunaomba wakati wa utekelezaji wa sera hii hili kundi lishirikishwe,” amesema.

Amefafanua kuwa kutokana na ukweli kuwa wanawake wengi wanashiriki shughuli za kilimo ni vema wakapata elimu ya kutosha juu ya kilimo misitu, ili wafanye shughuli hizo kulingana na hali ilivyo na kuleta tija kwenye kilimo kwa ujumla.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Deusdedit Mlay amesema endapo kilimo misitu kitapewa kipaumbele itasaidia kuleta na kuboresha uchumi wa wakulima, kwani watakuwa na uwezo wa kuzalisha vitu vingi kwa wakati mmoja.

“Kwenye kilimo misitu mkulima atakuwa na uwezo wa kuzalisha vitu vingi kwa wakati mmoja, mfano mazao ya biashara wakati huohuo anavuna asali, anapata kuni au matunda katika eneo moja,” amesema.