Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanesco yatakiwa kueleza faida matumizi majiko ya kisasa ya umeme

Mita janja zinazosambazwa na kufungwa Kwa wateja wa Shirika la umeme Tanesco mkoa wa Morogoro ambazo zimekuwa na uwezo wa kubaini hitirafu ya umeme Kwa mteja lakini pia inauwezo wa kudhibiti wizi wa umeme na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wateja wasiokuwa waaminifu. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya Kitaifa, hivyo jamii inapaswa kupewa elimu kuhusu faida zake kwa afya na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima, amelielekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia kitengo chake cha masoko kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za matumizi ya majiko ya kisasa ya umeme, pamoja na kuondoa hofu iliyojengeka kuhusu usalama wake.

Agizo hilo amelitoa baada ya kuzindua vyombo vya usafiri vilivyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Tanesco mkoani Morogoro, ambavyo ni magari manane, bajaji tano na pikipiki mbili vyenye thamani ya Sh1.8 bilioni.

Malima amesema ili kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), ni muhimu jamii ielimishwe na kubadili mitazamo hasi kuhusu matumizi ya majiko ya umeme.

 “Watu wengi wanayaogopa majiko haya kwa sababu kuu mbili, kwanza yanadaiwa kutumia umeme mwingi, na pili yanaweza kusababisha milipuko na kuunguza nyumba. Lakini majiko ya sasa si kama ya zamani yanatumia umeme kidogo na ni salama kwa matumizi ya familia. Tanesco ina wajibu wa kuwafahamisha wananchi ukweli huu,” amesema Malima.

Ameongeza kuwa Tanesco ina jukumu muhimu katika kufanikisha mkakati huo kwa kuhakikisha majiko yanayohamasishwa ni salama na yenye matumizi madogo ya umeme.

Katika hatua nyingine, Malima amekagua matumizi ya mita janja zinazofungwa kwa wateja mbalimbali, akielezwa namna zinavyorahisisha usimamizi wa matumizi ya umeme.

Akitoa maelezo, fundi wa kitengo cha mita Tanesco, Mkoa wa Morogoro, Aredy Mselela, amesema mita hizo zimetengenezwa kulingana na mahitaji ya watumiaji, zikiwemo za matumizi makubwa kama viwandani na za matumizi ya kawaida majumbani.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adamu Malima (mwenye kofia) akiangalia mita janja zinazosambazwa na kufungwa Kwa wateja wa Shirika la umeme Tanesco mkoa wa Morogoro, kushoto aliyeshika kipaza sauti ni fundi kitengo cha mita Aredy Mselela akieleza faida za mita hizo. Picha Hamida Shariff

Mselela amesema tofauti na mita za zamani, mita janja zinamwezesha mteja kununua na kuingiza umeme moja kwa moja bila kutumia kifaa cha ziada, huku pia zikitoa taarifa za hitilafu moja kwa moja kwa Tanesco.

Amesema mita hizo zina uwezo wa kugundua wizi au udanganyifu wa umeme bila ya ulazima wa kumtembelea mteja.

“Tukiishazifunga mita hizi, tunaweza kufuatilia utendaji wake tukiwa ofisini. Tukibaini zimechezewa au kuna hitilafu yoyote, tunachukua hatua haraka,” amesema Mselela.

Ameongeza kuwa katika Manispaa ya Morogoro, tayari mita janja 3,135 zimefungwa kwa wateja wa matumizi ya kawaida, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya huduma za umeme.