Prime
Tamisemi yavitega vyama uchaguzi serikali za mitaa

Bango linaloonyesha kituo cha kupigia kura. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imevialika vyama vya siasa vye usajili kamili kwenda kutoa maoni ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa Juni 15, 2024 jijini Dodoma
Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa vikisubiri kutolewa kwa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Ofisi ya Rais (Tamisemi) imetoa mwaliko kwa viongozi wa vyama hivyo kukutana jijini Dodoma kuzijadili, bila kuwapa rasimu.
Kwa mujibu wa baadhi ya vyama vya siasa vilivyozungumza na Mwananchi leo Juni 11, 2024 utaratibu uliozoeleka ni wa Tamisemi kutuma rasimu ya kanuni kwao kabla ya kuitwa kwenye mkutano wa kuzijadili.
Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alipoulizwa kuhusu kutotolewa kwa rasimu za kanuni kwa vyama vya siasa, amemtaka mwandishi awaulize Tamisemi.
Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru alipoulizwa, amemtaka mwandishi kumuuliza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, Nteghenjwa Hosea, ambaye naye hakupokea simu yake.
Akizungumza na Mwananchi Machi 23, 2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliwataka wadau wawe na subira, akisema kanuni hizo zitakuwa shirikishi.
Mwaliko wa Tamisemi
Barua ambayo Mwananchi imeiona iliyoandikwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya Juni 10, 2024 imesema wanaendelea na maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
“Katika maandalizi hayo, kama ilivyo kawaida, wameona ni muhimu kupata maoni ya vyama vya siasa maoni vyenye usajili kamili kuhusu rasimu ya kanuni hizo,” imesema sehemu ya barua ya mwaliko.
Barua hiyo imevitaka vyama vya siasa kutuma wenyeviti wa Taifa, makatibu wakuu na wenyeviti wa jumuiya za wanawake kuhudhuria kikao hicho.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Uenezi, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema chama hicho kimepokea barua hiyo kutoka kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hawajapata rasimu ya kanuni.
“Utaratibu ni kwamba huwa wanatutumia rasimu ya kanuni tunazijadili kabla ya kwenda kwenye mkutano, lajini wametuma bila kanuni. Bado tunashauriana kuhusu suala hili,” amesema Mrema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mkurugenzi wa Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa ambaye licha ya kusema hawajapata mwaliko, amesema kwa kawaida huwa wanatumiwa kwanza rasimu ya kanuni.
“Kwanza huwa kanuni za uchaguzi zinasambazwa kwenye vyama vya siasa na wadau wa demokrasia, vyama vinapitia vinatoa mapendekezo halafu baadaye kunakuwa na mkutano wa Msajili kwa ajili ya kuweka fikra pamoja kabla ya kutolewa rasimu ya mwisho ambayo ndio inakwenda kuwa kanuni kwa uchaguzi husika,” amesema.
Amesema suala hilo linatakiwa lifanyike kabla ya uandikishaji wa wapigakura kwa sababu kanuni pamoja na mengine inaelekeza kuhusu kujiandikisha.
Ngulangwa amenukuu ibara ya 10c ya Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inayosema, “kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge.”
“Tulichotarajia ni Bunge la Jamhuri ya Muungano kutunga sheria itakayoongoza kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Maana yake ni kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itashindwa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu haitakuwa na chombo cha kusimamia, lakini wakati huohuo, Tamisemi walishaondolewa kusimamia uchaguzi huo.
“Kinachokwenda kufanyika ni Tamisemi kuendelea kuhodhi mamlaka ambayo wameshapokonywa na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” amesema.
Maoni kama hayo pia yametolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo aliyesema, “ni dalili kuwa Tamisemi inataka tu kukitumia kikao hicho kujenga picha kuwa imeshilikisha wadau lakini ukweli ni kwamba haina nia ya dhati ya kubadili chochote.
“Kwa lugha nyepesi, kanuni zimeshatungwa, ndio maana hawataki kutupa mapema tuzichambue.”
Naye Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasili amesema kanuni hizo zimecheleweshwa na mpaka sasa vyama havijui ratiba ya uchaguzi.
“Pamoja na mchakato kutokujulikana mapema, zamani walikuwa wanatuletea rasimu ya kanuni mapema ili tuijadili pamoja na wataalamu ndani ya vyama, halafu tunapokutaa tunakuwa na mapendekezo.
“Lakini kama hawajatuma hizo kanuni, hao wanaokwenda, wanakwenda kufanya nini kama sio kufata rubberstamping (kupiga muhuri) ya wanaoutaka Tamisemi?”