Takukuru yakirejeshea mali kikundi cha Asante Mbeya Project ikitoa onyo
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, Jasper Luoga akizungumza wakati wa utoaji wa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi.
Muktasari:
- Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) imerejesha mali za kikundi zenye thamani ya Sh150 milioni, ambazo zilikuwa zimesajiliwa kwa jina la mtu binafsi ambaye ni mwanzilishi kwa nia ya kuwadhulumu.
Mbeya. Wakati Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya ikirejesha mali za kikundi cha Asante Mbeya Project zenye thamani ya Sh150 milioni, wananchi wametakiwa kabla ya kujiunga na vikundi vya umoja kuhakikisha vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza leo Juni Mosi, 2026 ofisini kwake, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Jasper Luoga amesema mali zilizorejeshwa ni magari matatu aina ya Toyota na Noah na vyombo vya chakula ambavyo vilinunuliwa na kikundi hicho.
Amesema kuwa mali hizo zilinunuliwa kupitia michango iliyochangwa na wanachama na kikundi cha Asante Mbeya Project na mwanzilishi wa kikundi hicho alitaka kuwadhulumu wenzake kwa kusajili mali hizo kwa jina lake binafsi.
“Awali Takukuru ilibaini kwamba kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka 2021 kilikuwa hakijasajiliwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria za uanzishaji na uendeshaji wa vikundi vya kijamii kama hicho.
“Lakini mwanzilishi wa kikundi hicho kwa kificho alikuwa na nia ovu ya kutaka kuwadhulumu wenzake kwani alisajili mali zote kwa jina lake binafsi kupitia jina la kibiashara la Asante Mbeya Project,” amesema Luoga.
Amewaomba wananchi kuwa makini na vikundi vinavyoanzishwa bila kujisajili kwa mujibu wa sheria, akieleza kuwa Takukuru haitasita kuchukua hatua kwa vikundi ambavyo havifuati utaratibu.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi, Taasisi hiyo iliwafikia zaidi ya wananchi 15,775 waliopewa elimu kuhusu madhara na athari za vitendo vya rushwa wakiwamo watumishi wa umma, sekta binafsi, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.
“Katika uchunguzi wa mashtaka, Takukuru ilipokea malalamiko 109 ambapo kati yake 62 yalihusu vitendo vya rushwa, uchunguzi umeanzishwa na hatua mbalimbali zinaendelea” amesema.
Amesema kwa sasa Takukuru imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi, kufuatilia fedha za miradi zinatumika ilivyokusudiwa na kushirikiana na wadau kuongeza ufanisi kubaini mianya ya rushwa.