TaCRI waongeza nguvu kutafiti miche ya kahawa

Muktasari:
- Utafiti huo mpya unalenga kuwasaidia wakulima wa kahawa waweze kuendelea kunufaika na shughuli hiyo hasa kipindi hichi ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Arusha. Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa nchini (TaCRI) wameamua kuwekeza nguvu kubwa katika kutafiti miche mipya itakayoweza kustahimili hali ya ukame ili kuwasaidia wakulima kutumia fursa iliyopo sokoni ya uhitaji mkubwa wa zao hilo.
TaCRI wamefikia hatua hiyo baada ya hivi karibuni kuwepo na ongezeko la uhitaji mkubwa wa kahawa katika soko la ndani na kimataifa hali iliyopaisha bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh1, 500 kwa kilo hadi 8,000.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 31, Mtafiti mwandamizi wa TaCRI, Amani Evance alisema kuwa bei ya zao ya kahawa limepanda nchini kutokana na ongezeko la mahitaji katika soko la kimataifa iliyosababishwa na nchi ya Brazil kushindwa kuendelea kulima kutokana na baridi kali iliyowakumba.
“Fursa kubwa ya zao la kahawa iliyopo kwa sasa inakwenda kuirudishia Tanzania hadhi yake katika soko la kimataifa.
“TaCRI tumewekeza katika utafiti wa kupata miche mipya itakayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi ambayo Tanzania tunakumbana nayo kwa sasa hasa Ukame,” amesema Evance.
Alisema kuwa wameanza utafiti huo unaohusisha aina 19 za miche ya Arabika inayostahimili magonjwa ya kahawa kwa ajili ya kupata mche bora mmoja utakaoweza kustahimili hali ya ukame na uwezo wa kuzaa.
“Arabika ni mche wa kisasa tulioutafiti na unafanya vizuri katika mikoa ya kanda ya kaskazini na kusini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhimili magonjwa na kuzaa vizuri, huku pacha wake inayofahamika kama Robusta ikifanya vyema Mikoa ya Kanda ya Ziwa,” alifafanua Evance.
Evance aliwataka wakulima walikwisha kupata magawo wa miche msimu wa kilimo uliopita kuotesha miti kati kati ya miche ya kahawa ili kupatia kivuli sambamba na kuweka matandazo chini ya mashina yote ikiwa ni njia ya kupunguza kasi ya kupoteza unyevu wake hali inayosaidia pia kukabiliana na Ukame.
Kwa upande wake Mtafiti wa miche ya Arabika na Robusta, Rehema Mwaipopo alisema kuwa aina hizo za kisasa za miche ya kahawa zinaongezeko la uzalishaji wa zaidi ya asilimia 50 kulinganisha na miche za kienyeji zilizokuwa zinatumika zamani.
“Miche hii inauwezo wa kumpunguzia mkulima gharama za utunzaji kwa zaidi ya asilimia 60, hasa katika kupambana na visumbufu mimea kwani hizi zinahimili magonjwa lakini pia inazaa sana tofauti na ile ya zamani na pia inaweza kuzaa mapema tu baada ya kupanda,” amesema mtafiti huyo.