Tabata Darajani walia kukosa maji miezi sita, Dawasa yajibu
Muktasari:
- Wakazi wa Tabata Darajani wanalalamikia kukosa maji kwa zaidi ya miezi sita, wakilazimika kununua au kutumia maji ya visima visivyo salama. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imetoa maelezo ya nini kinafanyika kumaliza tatizo hilo.
Dar es Salaam. Wakazi wa Tabata Darajani, maeneo ya Mtaa wa Amani, Magufuli na Jamhuri maarufu Kichefuchefu, Kata ya Kimanga, Wilaya ya Ilala, wameeleza kilio cha muda mrefu cha tatizo la maji wakidai baadhi yao wamefikisha miezi sita bila kupata huduma hiyo.
Hata hivyo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imezungumzia tatizo hilo wanalopitia wakazi hao wa jijini Dar es Salaam na kueleza mikakati mbalimbali ya kulimaliza.
Leo Alhamisi, Juni 4, 2026, Mwananchi limefika maeneo hayo na kuonesha visima wanavyotumia kuchota maji ambavyo wanadai si salama kutokana na hali yake, hivyo kuhofia usalama wao.
Mkazi wa Tabata Darajani, Mariam Mwambele, amesema maji yamekatika katika eneo lake tangu Novemba 2025 na hadi sasa hajawahi kupata maji ya bomba nyumbani kwake.
"Kwenye mtaa wetu wa Magufuli tangu mwezi wa 11 mwaka jana, sijawahi kupata maji nyumbani kwangu kwa miezi sita mpaka sasa na jana maji yametoka kwa saa mbili tu, hata ndoo haijajaa yakakatika," amesema Mariam.
Amesema tatizo la maji limekuwa sugu kiasi kwamba hata baada ya wananchi kuandamana na kufikisha malalamiko yao kwa mamlaka za maji bado hakuna suluhisho la kudumu lililopatikana.
Wakazi wa Tabata Darajani wakifunua sehemu ambayo inaunganisha maji inayotumiwa na wafanyakazi wa Dawasa kufunga na kufungua maji katika eneo hilo
"Walituahidi maji yatakuwa yanatoka Jumatano, Alhamisi na Ijumaa, lakini ahadi hizo hazikutimia. Kuna nyumba chache sana zinazopata maji na hata hayo yanatoka kwa muda mfupi kabla hayajakatwa tena," amedai.
Kutokana na ukosefu huo wa maji, amesema wengi wao wamejikuta wakitumia maji ya kisima kifupi ambacho wanaamini kinaweza kuchanganyika na maji taka kutoka kwenye makazi ya jirani.
"Tunatumia maji ambayo hata hatujui yanatoka wapi. Tuna hofu yanaweza kuwa si salama kwa matumizi ya binadamu, lakini hatuna mbadala," amesema.
Amesema baadhi ya wanawake hulazimika kununua maji ya chumvi kwa Sh800 kwa dumu huku maji mengine yakiuzwa hadi Sh2,000, hali inayoongeza ugumu wa maisha.
"Maji hayo ya chumvi huwezi kupikia maharage, huwezi kupika chai vizuri wala kufanya matumizi mengine ya kawaida ya nyumbani. Tunaumia sana," amesema.
Halima Omary amesema mgao wa maji unaotekelezwa sasa hauzingatii mahitaji halisi ya wananchi kutokana na muda mfupi wa upatikanaji wa huduma hiyo.
"Wakati mwingine maji yanatoka kwa shinikizo dogo. Kufikia muda wa kuyahifadhi tayari huduma imekatwa na wengine hawajapata hata tone," amesema Halima.
Mbali na hilo, amesema eneo hilo halina vyanzo mbadala vya maji salama vinavyoweza kusaidia wakati wa ukosekanaji wa maji, na kisima wanachokitegemea kina maji yasiyoridhisha kwa matumizi ya nyumbani kutokana na ubora wake kuwa wa mashaka.
"Tunalazimika kutumia maji hayo kwa sababu hatuna chaguo lingine. Hata afya za watoto wetu ziko hatarini kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama," amesema.
Naye, Majuma Amiri amesema moja ya mambo yanayowasikitisha ni kuona watu wakifika katika eneo lao na kufunga mtandao wa maji bila kutoa maelezo ya kutosha kwa wananchi.
"Hawa watu wanakuja mchana, wanafunga maji na kuondoka. Ukimuuliza anasema wanafungulia upande mwingine wapate maji, lakini huku kwetu maji hayafiki kabisa," amesema.
Swalihia Msuya, mkazi wa eneo hilo, amesema kinachowashangaza zaidi ni kuendelea kupewa bili za maji wakati huduma yenyewe haipatikani.
"Tunashangaa kuendelea kupokea bili za maji wakati mabomba yetu hayatoi maji. Maji yakitoka yanatoka kwa saa chache usiku kisha yanakatwa, lakini bili zinaendelea kuja kama kawaida," amesema Swalihia.
Amesema wananchi wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa viongozi wa mamlaka ya maji lakini bado hawajapata majibu ya kuridhisha kuhusu sababu za bili hizo.
Wakazi hao pia walidai baadhi ya mita zao zimekuwa zikisomewa na kutolewa bili hata katika kipindi ambacho hawajatumia maji ya bomba kwa muda mrefu.
Wakazi wa Tabata Darajani wakionyesha kisima wanachotumia kipindi cha ukosekenaji wa maji katika eneo hilo
Ilichokisema Dawasa
Mwananchi limezungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro, ambaye amesema mamlaka hiyo imechimba kisima kirefu chenye urefu wa mita 180 ambacho kipo katika hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kuanza kutumika.
"Kwa sasa mkandarasi yupo katika hatua ya kupima kiwango cha maji, ubora wa maji na aina ya pampu itakayofaa kutumika kwenye kisima hicho.
Pia tunafanya maandalizi ya mfumo wa umeme na vifaa vitakavyowezesha maji kuingizwa kwenye mtandao wa usambazaji," amesema Everlasting.
Amesema kisima hicho hakitanufaisha eneo la Darajani pekee bali kitasaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika Kata nzima ya Kimanga.
"Tumechimba kisima kikubwa ambacho kitawanufaisha wakazi wengi wa Kimanga. Hii ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma ya maji katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji," amesema.
Amesema ifikapo mwisho wa mwezi huu hatua zote muhimu zitakuwa zimekamilika na wananchi wataanza kunufaika na huduma hiyo.
Kuhusu malalamiko ya watumishi wa mamlaka hiyo kuwa sehemu ya ukosekanaji wa maji, amesema mamlaka hiyo imepokea malalamiko hayo na itayafanyia kazi, na itafika eneo hilo kesho Ijumaa, Juni 5, 2026, kwa ajili ya kufuatilia. Endapo wafanyakazi watakuwa wanahusika, watachukuliwa hatua.
Everlasting amesema inawezekana baadhi ya wananchi walipokea vibaya maelezo yaliyotolewa na mafundi wa maji wakati wa utekelezaji wa ratiba za mgao wa maji katika maeneo mbalimbali.
"Labda mwananchi alikuwa hajapata taarifa ya ratiba ya upatikanaji wa maji. Inawezekana fundi alipomweleza muda wa eneo lake umekwisha na wanahamia eneo lingine, maelezo hayo yakapokelewa vibaya.
Hata hivyo, tunasisitiza watumishi wetu wamepewa mafunzo ya huduma kwa wateja na wanaelewa namna ya kuwasiliana na wananchi kwa lugha nzuri na yenye staha," amesema Everlasting.
Amesema Dawasa inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu huduma kwa wateja kwa kuwa mazingira na mahitaji ya wananchi hubadilika kila wakati.
Wakazi wa Tabata Darajani wakionyesha kisima wanachotumia kipindi cha ukosekenaji wa maji katika eneo hilo
"Sisi tunaamini mteja ni wa kwanza. Dawasa ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo tunasisitiza matumizi ya lugha nzuri, hasa wakati wa changamoto za upatikanaji wa maji. Mwananchi akiwa tayari yupo kwenye hali ngumu ya kukosa maji, hatupaswi kuongeza maumivu kwa kutumia lugha isiyofaa," amesema.
Everlasting amesema taasisi hiyo imekuwa ikiwakumbusha watumishi wake umuhimu wa kuwapa wananchi matumaini na taarifa sahihi wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali za huduma.
Kuhusu malalamiko ya bili kubwa kwa wananchi wanaopata maji kwa mgao, Everlasting amesema Dawasa hutoza gharama kulingana na kiwango cha maji kilichotumika na kusomwa kwenye mita za wateja.
"Hatumtozi mtu kwa makadirio au kwa uongo. Bili zote zinatokana na usomaji wa mita. Kabla ya bili kutumwa, tunafanya usomaji wa mita na baada ya hapo mteja hutumiwa ujumbe wa kuhakiki usomaji huo, na akiona kuna tofauti yoyote anatakiwa kutoa taarifa mapema kabla bili haijathibitishwa," amesema.
Amesema wananchi wanaopata maji kwa ratiba ya mgao mara nyingi hujaza maji kwa wingi wanapopata huduma hiyo ili kujihifadhi kwa siku zijazo, jambo ambalo linaweza kuongeza kiwango cha matumizi kinachoonekana kwenye mita.
"Mtu anayepata maji kila siku anaweza kutumia kiasi kidogo kwa wakati mmoja, lakini anayepata maji kwa ratiba hulazimika kuhifadhi mengi kwa matumizi ya baadaye. Hiyo inaweza kufanya matumizi yaonekane makubwa zaidi katika kipindi husika," amesema.
Everlasting amesema Dawasa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za maji pamoja na taratibu za uhakiki wa bili ili kuepuka malalamiko yanayoweza kutatuliwa mapema kupitia mifumo iliyopo.