Stendi ya Magufuli waweka vijana wa kutoa elimu ya Corona

Muktasari:
- Uongozi wa Standi ya Magufuli iliyopo Mbezi Dar es salaam imeandaa vijana kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu maambukizu ya Corona kwa kuwatangazia wananchi kuzingatia taratibu zote zilizotolewa na wataalamu wa afya.
Dar es Salaam. Uongozi wa Standi ya Magufuli iliyopo Mbezi umeanzisha mbinu mpya ya kutoa elimu itakayowasaidia kuwahamasisha abiria wanaingia kwenye standi hiyo kuchukua tahadhari ya kujikinga na wimbi la tatu la Corona.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 29,2021, Meneja wa Stendi hiyo, Maira Mkama amesema kuna vijana wameandaliwa kwa ajili ya kuzunguka standi hiyo wakiwa na vipaza sauti,na kurusha matangazo muda wote kutoa elimu na kuwaambia wananchi ugonjwa hupo hivyo wachukuea tahadhari.
Amesema wamekuja na mtindo huo baada ya kubaini watu wanaendelea kuishi kimazoea kwa kupuuza taratibu ziliotolewa na wataalamu wa afya namna ya kujikinga na Corona.
“Tumeweka vifaa kama sabuni ya kunawia maji, vitakasa mikono lakini abiria hawazingatii na wamekuwa wakiingia kwenye mabasi kusafiri bila kuchukua tahadhari yeyote,tumekuja na mfumo wa watu kuzunguka standi zima watoe elimu watu waelewe janga hili lipo,” amesema Mkama
Mkama ameeleza kwamba wameongea na viongozi wa Chama cha wamiliki wa mabasi nchini (TABOA) waweze kuwafahamisha wa miliki wa mabasi waweze kuwabana wafanyakazi wao kwa kuwasimamia abiria kufuata muongozo ulikwisha kutolewa na mamlaka husika.
“Wafanyakazi wa mabasi wanawategemea matajiri wao wawape maelekezo wakati huo sisi tunatoa maagizo kama serikali lakini wao kwa kuzingatia hili hawatakuwa na ugumu kutimiza wajibu wake,” amesema
Mkama amesema uongozi wa standi hiyo upo kwenye hatua za mwisho kuomba vifaa ikiwemo ndoo, sabuni na vitakasa mikono, vipima joto ili kuimarisha huduma kuzunguka standi hiyo hasa nyakati za asubuhi wanapokuwa watu wengi.
“Hivi vipima joto mara nyingi huwa tunaviomba kutoka uwanja wa ndege kwa sababu wanavyo kwa wingi na taasisi ipo kwenye mchakato wa mwisho kuomba tupate vingi ili tuanze kutumia kuwapima abiria wanapoingia katika standi hii pamoja na kuongeza ndoo sabuni na vitakasa mikono,” amesema