Soko jipya mboga za majani lapatikana Marekani

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mboga Duniani, Marco Wopereis
Muktasari:
- Huenda wakulima wa mboga za majani nchini wakawa wamepata suluhisho la kuepeukana na kuharibika kwa mboga zao baada ya kupatikana kwa soko jipya nchini Marekani linalonunua mbogamboga kavu na zilizozosagwa.
Dar es Salaam. Huenda wakulima wa mboga za majani nchini wakawa wamepata suluhisho la kuharibika kwa mboga zao baada ya kupatikana kwa soko jipya nchini Marekani linalonunua mbogamboga kavu na zilizozosagwa.
Hii lilisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mboga Duniani, Marco Wopereis katika Mkutano wa Mfumo wa Chakula wa Afrika 2023 (AGRF) wakati wa mjadala juu ya upotevu wa usalama wa chakula baada ya mavuno.
Akizungumza katika mkutano huo, Wopereis alisema kuna fursa nyingi katika bidhaa hizo kwani badala ya kuuza mbogamboga mbichi pekee bali wanaweza kuzalisha bidhaa mpya kwa ajili ya watumiaji wengine.
"Kuna masoko kwa ajili ya watu wa Afrika Mashariki pamoja na Tanzania ambayo wanaweza kuuza mboga kavu iliyo sagwa nchini Marekani," alisema.
Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, kusaga mbogamboga baada ya kukaushwa zinaweza kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika jambo ambalo litaondoa wasiwasi wa upotevu wa mazao hayo kwa wakulima.
Katika hatua nyingine alisema serikali za mitaa hasa Manispaa zinaweza kuweka maeneo ya ukusanyaji mbogamboga kwa ajili ya vyama vya ushirika vya wakulima ili viweze kuhifadhi kuweka nemba na kisha kuuza bidhaa zao.
Pia alishauri kuwapo kwa masoko ya jumla ambayo yatawawezesha wakulima kukodi maeneo ambayo wanaweza kuhifadhi mboga zao kwa bei nafuu kwa muda mfupi kabla ya kupata watumiaji.
"Suala muhimu hapa ni vifaa vya kuwezesha uhufadhi kama suluhisho kwa sababu mboga zinaharibika sana na zinapaswa kuwa na mfumo mzuri," alisema.
Alisema ni muhimu kuja na uvumbuzi ambao utasaidia wakulima kuuza kile wanachozalisha.
Mmoja wa wakulima wa mbogamboga na matunda waliohudhuria mkutano huo, Leyla Msangi alitaka fursa hizo kuwa zinawekwa wazi ili watu wenye uwezo waweze kuzitumia kikamilifu.
"Fursa huwa zipo, ila ili ujue kuwa ipo laxima uwe na watu ambao wanazo taarifa moja kwa moja au uwe ni mfuatiliaji wa mitandao mbalimbali na taarifa za masoko. Taarifa kama hizi zingekuwa zinawekwa wazi ili watu tuzitumie kikamilifu," alisema Leyla.