Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri iliyopo kitambulisho cha Nida

Muktasari:

  • Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imesema vitambulisho vinavyotolewa kwa wananchi vimebeba usalama wa nchi huku wakibainisha atakeyeomba uraia wa nchi nyingine ataondolewa kwenye mfumo.

Mwanza. Ofisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Geofrey Tengeneza amesema kitambulisho cha Nida ni nyeti na kimebeba usalama wa nchi na ulinzi wa wananchi pia endapo mwananchi ataomba uraia wa nchi nyingine watamuondoa kwenye mfumo wao.

Akizungumza jana Jumatano, Februari 22, 2023 kwenye mjadala wa Mwananchi Twitter Space uliohoji 'Vitambulisho vya Taifa kuondolewa ukomo kuna athari gani?, Tengeneza amesema kutokana na unyeti wake wakati wa utoaji lazima wajiridhishe maeneo mengi kwa kushirikiana na uhamiaji pamoja na taasisi zingine.

“Kitambulisho cha Taifa ni nyeti sana.  Hiki kinabeba usalama wa nchi, usalama wako, ulinzi wa nchi yetu na mambo mengi kadha wa kadha.

“Hata namna ya utoaji wake ni lazima uwe ni wakujiridhisha katika maeneo mengi sana, na hii ndio sababu mnaona wakati mwingine vinachukua muda. Lazima watu wa Uhamiaji wajiridhishe, Serikali za Mitaa, kinapita maeneo mengi ili mwisho wa siku tuhakikishe kinatoka kwa mtu anayestahili na ni Mtanzania vinginevyo kikiangukia kwa mtu ambaye siyo raia itakuwa na shida yake,”amesema Tengeneza

Kutokana na watu kulalamikia kupata tu namba za Nida badala ya vitambulisho, Tengeneza amesema hiyo inatokana na taasisi kujiridhisha baadhi ya vitu lakini kama kila kitu kipo sawa na bado kitambulisho kikachelewa ni matatizo ya ndani ikiwemo mashine kupata shida.

“Muda si mrefu sana mtaona vitambulisho vinaanza kutoka kwa wingi kwa sababu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatoa vitambulisho hivyo,” amesema.

Kuhusu kubadilisha uraia, amesema endapo mwananchi atabadilisha uraia lazima aukane uraia wa kwanza ambao ni wa Tanzania kwakuwa bado nchi hiyo haijawa na uraia pacha na atakapokana basi kitambulisho chake cha Nida kitaondolewa kwenye mfumo na kuonyesha ni raia wa nchi nyingine.

Akijibu swali la iwapo mtu akifariki taarifa zake zitatumika au la amejibu “Kwa kawaida mtu anapofariki, kuzaliwa kuna hati zinatolewa na Rita. Katika kutolewa hizo taarifa na kwenye mfumo zitaingia. Kwahiyo katika hili hakuna wasiwasi wowote kwa sababu kwenye mfumo wetu itaonyesha mtu huyu amefariki na hakuna mtu yoyote ataweza kukitumia kitambulisho hicho,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto ya alama za vidole kutoonekana kwa baadhi ya watu wanampango wa kuanzisha matumizi ya macho ambayo yatakuwa mbadala wa alama ya kidole kwa watu hao.

“Nida utambulisho mkubwa sana tunaoutumia ni ule wa baiolojia kwa maana ya fingerprint(alama ya kidole) hata kama picha yako ni ile ile hata kama ulipiga wakati wa utoto hiyo haitupi shida sana:sisi kitu cha kututambulisha kwamba wewe ni wewe ni finger print yako pale. Hiyo ndiyo itatutambulisha”

“Hizi ndizo za kuaminika (alama ya kidole na macho) kwa sababu hazibadiliki”

Amesema Serikali ina dhamira nzuri ya kutoa ukomo wa vitambulisho vya nida ikiwemo ya kuondoa usumbufu kwa wananchi pamoja na kuondoa gharama za utengenezaji na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.