Prime
Simulizi ya baba aliyepoteza watatu kwa mauaji, mke akijeruhiwa Dodoma

Baba wa familia ambaye imepoteza watu watatu na mkewe kujeruhiwa na watu wasiojulikana usiku wa kumkia jana (Septemba 16,2024), Robert Mgema akizungumza na waandishi wa Habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Leo Septemba 17,2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Miongoni mwa waliouawa ni binti aliyehitimu darasa la saba
Dodoma. Baba wa familia iliyopoteza watu watatu na mkewe kujeruhiwa na watu wasiojulikana amesimulia namna alivyopokea taarifa za tukio hilo.
Vifo vya watu hao viligundulika jana Septemba 16, 2024 saa 9.00 alasiri katika Mtaa wa Segu Bwawani uliopo Kata ya Nala jijini Dodoma.
Waliofariki dunia ni Milcah Robert (12), aliyemaliza darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi ya Chilohoni, mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20) na Micky anayekadiriwa kuwa na miaka 16. Mama wa familia hiyo, Lusajo Mwasonge (40) alijeruhiwa kichwani.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 17, 2024, Robert Mgema, mwalimu wilayani Ikungi, mkoani Singida amesema Septemba 14 kulikuwa na mahafali ya darasa la saba shuleni kwa mwanaye ambayo alihudhuria.
Amesema aliondoka siku hiyohiyo kurudi kazini kwake Singida.
“Niliwasiliana na mke wangu kwa sms (ujumbe mfupi wa maneno) Jumapili, jioni niliwahi kulala kwa sababu nilikuwa nimechoka kutokana na safari. Mke wangu alinitafuta saa 3.00 usiku sikusikia,” amesema.
“Jana (Septemba 16) nilimtafuta kwa simu kuanzia asubuhi hadi saa 8.00 mchana sikumpata. Nikatoka kwenda maeneo yangu ya kazi. Saa kumi kasoro jirani yangu (baba Kelvin) alinitafuta akaniambia hapa nyumbani kwako mbona hatukuelewi?” amesema.
Amesema baba Kelvin alimwambia hajaona mtu aliyetoka nje tangu asubuhi, amejaribu kugonga milango imefungwa na hajaona watoto wakicheza nje ya nyumba.
Baba Kelvin alimweleza baada ya kuchungulia dirishani alimuona binti wa kazi amelala sebuleni na kuna michirizi ya damu kwenye vigae.
Kwa mujibu wa maelezo yake, alimuuliza iwapo anadhani kuna tatizo akajibiwa huenda mkewe ameenda mjini anakofanya biashara.
“Nikamuuliza hakuna mtu yeyote hapo, akasema kuna mtoto mdogo anaitika lakini anasema anaogopa kwenda kufungua mlango. Nikamwambia hapo kutakuwa na tatizo hebu mtafute rafiki wa mke wangu mama Geofrey,” amesema.
Wakati huohuo amesema alipigiwa simu na jirani mwingine aliyemweleza mfanyakazi wa ndani amekutwa akiwa amelala sebuleni.
Amesema alipohoji iwapo ni mzima alijibiwa hawaelewi bali wameona mchirizi wa damu.
“Nikaona sina namna lazima niondoke kurudi Dodoma. Nikawa natembea huku nafanya mawasiliano, jirani yangu mwingine alinipigia akaniambia kuna watu watatu wamefariki dunia,” amesema.
Alipouliza kuhusu waliokufa, anasema aliambiwa kuwa ni binti wa kazi na wengine hawawatambui hivyo akifika nyumbani atajua ni nini kimetokea.
“Nilijitahidi kuendesha gari nilipofika nyumbani nikauliza kuhusu binti yangu Careen, nikajibiwa ni mzima na ndiye aliyefungua mlango. Nilikuwa najua kulikuwa na watu watano, mabinti wawili wakubwa na mdogo aliyekuwa na mahafali yake Jumamosi,” amesema.
Amesema alipoingia ndani alikuta miili ya mabinti wawili ambayo haiwezi kutambulika, ila kwa sababu ndio waliokuwa chumbani akajua ni ya wanawe.
“Wakati huo mke wangu alikuwa ndani nadhani walimpiga akawa amezimia. Sijui, akiwa mzima atakuja kutueleza kilichompata. Nikiwa njiani walinipigia wakanieleza mke wangu hali aliyokutwa nayo, niliomba wampeleke hospitali,” amesema huku akitokwa machozi.
Amesema mkewe yuko hospitali na hadi alipokuwa akizungumza na Mwananchi leo Septemba 17 saa sita mchana hakuwa amemuona.
Mgema amesema alipofika Dodoma jana, Polisi walimchukua kwenda kutoa maelezo hadi saa 7.00 usiku na aliporejea nyumbani watu wote walikuwa wametawanyika.
“Nyumba ilikuwa imefungwa kwa hiyo nililala nje. Nasikitika aliyevamia nyumbani kwangu alikuwa anataka nini, sijawahi kuwa na uhasama na mtu yeyote. Sisi pale Nala ni wageni tuna miezi sita tu tangu tuhamie. Sijui kama kuna mtu niliwahi kumkwaza au familia yangu kumkwaza,” amesema.
Amesema majirani zake wamemweleza hapakuwahi kuwa na mgogoro wowote wa ardhi naye hana shida hiyo na yeyote.
Mgema amesema awali alikuwa akiishi Mailimbili mkoani Dodoma kabla ya kuhamia hapo.
“Vitendo vya mauaji yanayoendelea nalaani. Serikali lazima iangalie hatuwezi kwenda kwa namna hii tukadhani kuwa tunaendelea kujenga nchi yetu. Wamekufa watoto wadogo ambao wangeweza kuja kutusaidia. Mwanangu alikuwa ana ndoto ya kuwa mhandisi baadaye,” amesema.
Kauli ya Polisi
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo alisema waliofariki dunia ni Milcah Robert (12), na mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20), ambao baada ya kuuawa miili yao ilichomwa moto katika chumba walichokuwa wamelala.
Mwingine aliyeuawa ni Micky aliyekuwa mfanyakazi wa ndani aliyekutwa sebuleni, huku akiwa na jeraha kichwani la kupigwa na kitu kizito.
Alisema Lusajo alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Alieleza Polisi wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha mauaji hayo.
“Polisi Mkoa wa Dodoma linatoa wito kwa wananchi kama ulivyo utamaduni wao kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha waliotekeleza uhalifu huu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.