Simulizi mwenyekiti wa mtaa aliyemsuluhisha JPM na jirani

Muktasari:
- Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele nyumbani kwake Chato juzi.
Mwanza. Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele nyumbani kwake Chato juzi.
Wengi waliowahi kuishi na kufanya kazi naye, wamejitokeza kusimulia maisha ya kiongozi huyo tangu alipofariki dunia Machi 17.
Hussein Salum, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro B maarufu kama mtaa wa Selemani Nasoro jijini hapa, ni mmoja wa watu wenye simulizi na kumbukumbu ya kusisimua kuhusu maisha halisi ya kawaida ya Magufuli, aliyewahi kuwa mkazi wa mtaa huo enzi hizo akiwa waziri.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu ofisini kwake juzi, Salum, anayeongoza mtaa huo tangu mwaka 1994 hadi sasa anakumbuka tukio analosema hatalisahau la Magufuli kufika ofisini kwake kuomba usuluhishi wa mgogoro wa mpaka kati yake na jirani yake.
“Sikumbuki ni mwaka gani; lakini tukio hilo bado litakuwa kwenye kumbukumbu zangu daima. Siku hiyo nilikuwa nyumbani kwangu, ghafla watoto wakanitaarifu kuwa kuna mgeni ananiita nje,” alisema Sulum
Aliongeza; “Ile natoka nje nakutana uso kwa uso na Magufuli akiwa na walinzi wake na kuniambia ana shida na mimi. Niliogopa nikahisi kuna jambo baya ukizingatia wakati huo tayari alikuwa waziri. Nakumbuka wakati huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.”
Alisema baada ya kuona hofu aliyokuwa nayo, Magufuli alimweleza kuwa kuna mgogoro wa ardhi kuhusu mpaka umetokea kati yake na jirani na kumuomba kama kiongozi wa mtaa aende kuwasuluhisha.
“Maelezo hayo yaliniondolea hofu; niliamua kuongozana naye hadi eneo lenye mgogoro na kumwita jirani waliyekuwa wakivutania eneo la mpaka. Kwa pamoja tulijadiliana na kufikia mwafaka ndani ya dakika 10 tu,” alisema Salum.
Akifafanua, mwenyekiti huyo alisema awali jirani yake Magufuli aliyemtaja kwa jina la Hemed Patasi, alihisi kiongozi huyo alitaka kutumia nafasi yake ya uwaziri kupora ardhi yake kwa kuongeza eneo la mpaka.
“Awali Patasi ambaye pia ni marehemu hakuelewa ambacho jirani yake alitaka kufanya baada ya kuona vifaa vya ujenzi vikiwamo mawe, mchanga na matofali vimerundikwa mpakani. Alihisi jirani yake anataka kutwaa eneo lake,” alisema.
Aliongeza: “Baada ya mazungumzo na mashauriano, alielewa kuwa vifaa hivyo havikuwa vya kujenga nyumba, bali ukuta. Baada ya kuelewa hivyo Patasi hakuwa na pingamizi, aliruhusu kazi ya kujenga ukuta iendelee bila kuathiri eneo la mpaka.”
Funzo la kujishusha
Akizungumzia uamuzi wa Magufuli kama waziri tena wa sekta ya inayohusika na ardhi kuacha kutumia madaraka yake na kuamua kutafuta suluhu na jirani yake, Salum alisema kuwa kitendo hicho kilimpa funzo kuwa cheo si chochote, bali ni dhamana.
“Hayati Magufuli angeweza kutumia madaraka yake kuendelea na ujenzi bila kujali hisia wala kizuizi kutoka kwa jirani yake. Lakini hakufanya hivyo. Alikuja ofisini kwangu kwa mwenyekiti wa mtaa kutafuta mwafaka wenye kudumisha amani na utulivu kati yake na majirani. Alitambua, kuthamini na kuelewa nafasi ya Serikali ya mtaa. Hili ni funzo kwa viongozi wote,” alisema Salum.
Maisha ya Dk Magufuli mtaani
Akisimulia namna Magufuli alivyokuwa akiishi mtaani hapo, alisema: “Kwangu binafsi na hata kwa wakazi wengine wa mtaa wa Nyamanoro B, Magufuli alikuwa mwananchi na mkazi wa kawaida. Japo hakuwa akiishi hapa kipindi kirefu, lakini yeye binafsi na ndugu zake waliokuwa wakiishi kwenye nyumba yake, walishiriki shughuli zote za mtaa ikiwamo misiba na michango ya maendeleo. Alichanga hata fedha ya tochi na betri kwa vijana wanaojitolea kulinda usiku.’’
Alisema kila mara kiongozi huyo alipofika nyumbani kwake Nyamanoro hakuondoka bila kufika nyumbani kwa mwenyekiti na majirani wengine wa karibu kuwajulia hali.
“Watanzania wote tumefiwa; lakini sisi wa mtaa wa Nyamanoro B na Chato alikokuwa akiishi tunahisi kupoteza zaidi. Kwetu hakuwa tu kiongozi, bali alikuwa jirani na mkazi mwenzetu,” alisema
Msafara wa mwili wa Dk Magufuli wasimama mtaani
“Kati ya mambo yaliyotufariji na kuamini viongozi wa mkoa wa Mwanza wanatuthamini ni kitendo cha msafara wa mwili wa Magufuli uliokuwa ukitokea uwanja wa ndege kwenda uwanja wa CCM Kirumba kusimama kwa dakika kadhaa mtaani kwetu kama ishara ya kuagana na jirani na mpendwa wetu,” alisema.
Alisema tukio hilo lililotokea Machi 24, siku ambayo wakazi wa Mwanza na mikoa jirani walitoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo.
Alisema hatua hiyo iliwapa faraja licha ya kuwa mwili wake haukuingizwa katika nyumba yake
Damian Mukama, mkazi wa mtaa wa Nyamanoro B alisema: “Mtaa wa Nyamanoro B tumepewa heshima kama walivyofanyiwa wakazi wa Busisi ambako ni ukweni kwa hayati Magufuli ambako pia msafara ulisimama kwa dakika kadhaa. Tunawashukuru uongozi wa Serikali kwa kutupa heshima hiyo ya msafara kusimama mtaani kwetu.”