Prime
Simulizi mauaji ya Jenerali Imran Kombe-4

Moshi. Katika Makala iliyopita, tuliangalia namna askari wawili wa Jeshi la Polisi, Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku waliommiminia risasi 15, mkuu wa zamani wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe walivyojitetea kortini.
Katika simulizi hiyo tuliona namna polisi hao waliokuwa na silaha aina ya bastola na bunduki Sub Machine Gun (SMG), walivyoamriwa na kiongozi wa timu, Sajini Thomson Mensah, kushuka kwenye gari na kufyatua risasi kadhaa hewani.
Kila mmoja alieleza namna alivyoshuka kwenye gari na kufyatua risasi hewani na baadaye kuamua kulenga magurudumu ya gari aina ya Nissan Patrol lililokuwa likiendeshwa na marehemu Kombe akiwa na mkewe, Roseleen Kombe.
Wote walikana kumlenga moja kwa moja Kombe na kusababisha kifo chake Juni 30, 1996 saa 10 alasiri katika kijiji cha Mailisita wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, mauaji ambayo hadi leo bado wananchi wana hisia tofauti.
Washtakiwa katika kesi hii walikuwa sita, Sajini Thomson Mensah, Koplo Elisante Tarimo, Koplo Juma Mswa, Chediel Elinisafi na Konstebo Mataba Matiku na raia pekee, Ismail Katembo ambaye alifariki akiwa mahabusu kabla kesi kusikilizwa.
Tukio hilo liligubikwa na simulizi na hisia tofauti juu ya nini hasa kiini cha mauaji ya Luteni Jenerali Imran Kombe.
Kumekuwepo na nadharia ya ulaji njama kwamba pengine kuna mkono wa mtu katika mauaji hayo na nyingine ni kweli aliuawa na polisi.
Leo tunawaletea simulizi ya namna Jaji Buxton Chipeta wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alivyochambua ushahidi wa upande wa mashtaka na wa polisi hao wawili na kuona kuwa wana hatia na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa.
Hukumu ya Jaji Chipeta
Katika hukumu hiyo iliyotolewa Januari 26,1998, Jaji Chipeta aliyesikiliza kesi hiyo aliwaachia huru askari watatu baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yao na kuwatia hatiani askari wawili kati ya hao watano.
Jaji alisema ni ukweli wakati mshtakiwa wa tatu, Koplo Mswa kutoka jijini Dar es Salaam na wa tano, Mataba Matiku kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro, walipoanza kufyatua risasi waliamini mtu aliyekuwa na gari ni mhalifu mwenye silaha.
“Lakini wakati marehemu alipotoka kwenye gari, washtakiwa hawa wawili walijua kuwa hakuwa na silaha. Mbali na hilo, marehemu hakujaribu kukabiliana nao wala kuwafuata. Badala yake alikimbia huku akiyumba.
Wakati huo mshtakiwa wa tatu na wa tano hawakuwa umbali unaozidi mita 30 kulingana na ushahidi wa shahidi wa tatu wa mashtaka na inaweza kuwa ni chini ya umbali huo kulingana na maelezo ya ziada ya mshtakiwa wa tano,”alieleza.
Jaji Chipeta aliendelea kusema kuwa “Kwa hiyo, washtakiwa hawa wawili walikuwa na kila fursa ya kumkamata bila kutumia silaha za kuua. Kulingana na ushahidi na mazingira haya, nimeridhika na ninaona washtakiwa hawa kwa makusudi na bila uhalali walimuua marehemu”
“Pengine walimfyatulia risasi na kumuua marehemu ili kuondokana na jambazi maarufu (kama walivyoshuku). Hii kwa maoni yangu ilikuwa ni kuua kwa nia mbaya,”alisema Jaji na kuwahukumu adhabu ya kifo polisi hao wawili.
Washtakiwa walivyokata rufaa
Washtakiwa hao wawili hawakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa Mahakama ya Rufani huku mrufani wa kwanza, Juma Mswa akitetewa na wakili Ignas Itemba huku mrufani wa pili, Mataba Matiku alitetewa na wakili Godwin Sandi, wote wa Moshi.
Katika hoja ya kwanza, mtufani Mswa alilalamika kuwa Jaji aliyemuhukumu adhabu ya kifo alikosea kisheria kwa kutojibu swali kuwa wakati anatoka kwenye gari alifanya hivyo kutekeleza amri ya kiongozi wa timu ya mapolisi, Sajin Mensah.
Hivyo Profesa Itemba akasema kwa sababu hiyo, kitendo cha mteja wake kushuka na kufyatua risasi tatu kilikuwa halali kwani alitekeleza amri ya kijeshi.
Akijibu hoja hiyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Ama-Isario Munisi, alisema mshtakiwa wa kwanza aliwaamuru washtakiwa wengine watoke kwenye gari na kufyatua risasi hewani, hakuagiza wamfyatulie risasi na kumuua Kombe.
Majaji waliosikiliza rufaa hiyo katika kushughulikia hoja hiyo, walinukuu ushahidi wa mshtakiwa anayetajwa kutoa amri, Mensah aliyesema “Kama mshukiwa anatoroka, hutumii silaha ya moto labda kama naye ana silaha ya moto.
“Ni lazima utafute mbinu nyingine ya kumkamata. Unapomfyatulia risasi unaweza kumuua. Unaweza kufyatua risasi hewani kumuonya.
Huwezi kumpiga mguu kwa risasi kama hana silaha. Unatumia nguvu nyingine kumdhibiti.
“Kwa kuwa walimuona akitoka kwenye gari akiwa hana silaha, haikuwa busara kumshambulia marehemu kwa risasi.
Sio sahihi kusema walitumia nguvu ya wastani ili kumkamata kwa kuwa walimuua mtu asiye na silaha.
Katika ushahidi wake huo, Mensah aliongeza kusema “Baada ya gari (la marehemu Kombe) kusimama, ingekuwa ni rahisi kwa washtakiwa (Mswa na Matiku) kumfukuza marehemu na kumkamata kirahisi kabisa.
Majaji hao walisema kumfukuza na kumkamata marehemu kungekuwa rahisi zaidi kwa sababu tayari alikuwa amejeruhiwa kwa risasi na ndio maana alionekana akikimbia huku akiyumba, hivyo wakaamua kuitupa hoja hiyo.
Katika hoja ya pili ambayo iliibuliwa pia na mrufani wa pili,Mataba Matiku na mrufani wa kwanza, Juma Mswa ilieleza kuwa Mahakama ilikosea iliposema wakati marehemu anatoka ndani ya gari, warufani walifahamu hakuwa na silaha.
Majaji walisema warufani wanakiri kuwa marehemu hakutoa kitisho chochote kwao, kwa hiyo wanakubaliana na Jaji aliyewahukumu kuwa walifahamu au walitakiwa wafahamu kulingana na mazingira, kuwa marehemu hakuwa na silaha.
Katika hoja ya tatu, mrufani Mswa alilalamika kuwa Mahakama ilikosea kumtia hatiani kama msaidizi wa mrufani wa pili katika kufanya mauaji hayo, wakati kulikuwa hakuna ushahidi wowote kuwa wawili hao walikuwa na dhamira moja.
Majaji walikubaliana na hoja hiyo na kusema Jaji aliyewahukumu alikosea kumuhukumu mrufani wa kwanza kama msaidizi wa mauaji wakati tayari alishawaona kuwa kwa makusudi na bila uhalali walisababisha kifo cha Kombe.
Walisema kuna ushahidi uliopokelewa kuwa warufani wote wawili walimfyatulia risasi marehemu na daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu hakuweza kutofautisha ni silaha ipi ilisababisha majeraha yale tisa ya risasi aliyoyabaini.
“Kulikuwa hakuna nafasi kwa mazingira yale kumchukulia mmoja kama ni mhalifu msaidizi na mwingine ndiye muuaji mkuu , kwani hata mwisho wa kesi Jaji aliwatia hatiani wote wawili kwa nia yao ovu ya kumuua marehemu,”walisema majaji.
Kesho tutawaletea simulizi ya hoja za rufaa ya Konstebo Mataba Matiku na namna majaji waliosikiliza rufaa walivyozipima hoja zake hizo.
Usikose sehemu inayofuata ya simulizi hii kesho