Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi mauaji ya Jenerali Imran Kombe-2

Muktasari:

  • Ni mauaji yaliyogubikwa na simulizi na hisia tofauti juu ya nini hasa kiini cha mauaji ya mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini (TISS), Luteni Jenerali Imran Kombe aliyeuawa kwa risasi Juni 30, mwaka 1996.

Moshi. Ni mauaji yaliyogubikwa na simulizi na hisia tofauti juu ya nini hasa kiini cha mauaji ya mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini (TISS), Luteni Jenerali Imran Kombe aliyeuawa kwa risasi Juni 30, mwaka 1996.

Kumekuwepo na nadharia ya ulaji njama (conspiracy theory) kwamba pengine kuna mkono wa mtu katika mauaji hayo yaliyotokea Kijiji cha Mailisita Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na nyingine ni kwamba, ni kweli aliuawa na polisi?

Simulizi hii inaegemea ushahidi uliotolewa mahakamani katika kesi hii na kesi ya madai ya fidia iliyokuwa imefunguliwa na mkewe, Roseleene Kombe dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na simulizi zilizogubika mauaji hayo.

Maneno yalisemwa mengi, mojawapo ni hisia kuwa huenda aliuawa kwa sababu ya urafiki wake wa karibu na Agustino Lyatonga Mrema, mgombea urais wa NCCR-Mageuzi 1995, lakini kwa kesi ilivyokuwa mahakamani haikuwa sahihi.

Ni kutokana na hisia pengine mauaji yake yalikuwa ya kupangwa, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliamua kuunda tume ambayo iliwasilisha ripoti yake 1997 ambayo sio wazi, ikisema Serikali haikuwa na mkono katika mauaji hayo.

Katika mfululizo wa makala hii, mwandishi wetu atakuletea simulizi ya nini hasa kilisababisha mauaji yake, nani walimfyatulia risasi zaidi ya 15, maelezo ya maungamo ya wauaji wake yanasemaje na familia ililipwa fidia ya kiasi gani cha fedha.

Katika makala iliyopita, tuliona namna makachero wa Jeshi la Polisi Dar es Salaam walivyosafiri hadi Moshi na kuungana na wenzao na kuanza kutafuta gari aina ya Nissan Patrol namba TZG 50, mali ya DW Ladwa lililokuwa limeibwa Juni 24,1996.

Tuliishia pale ambapo dereva wa gari lililokuwa linatumiwa na makachero, ambalo nalo ni mali ya Ladwa, alipoona gari la Kombe linalofanana na wanalolitafuta likitokea barabara ya Arusha na kusema ndilo gari lililoibwa.

Dereva, Ismail Katembo ambaye sasa ni marehemu alitoa sauti ya mshangao akisema gari lililopo mbele yao likitokea barabara ya Arusha-Moshi ndio gari ambalo wanalitafuta, hivyo akaliwashia taa lisimame, lakini dereva hakusimama.

Hapa, Kombe hakujua kuwa ndio mwisho wa maisha yake umefika.

Badala ya kusimama, alipowapita, Luteni Jenerali Kombe alikata kushoto na kuendelea kuingia ndani kidogo, hapo polisi nao waligeuza gari lao na kulifukuza gari ambalo waliamini ni mshukiwa hatari anatoroka, huku wakifyatua risasi.

Gari hilo lililokuwa likiendeshwa na marehemu lilisimama baada ya kugonga kisiki, ambapo risasi zilizofyatulia na mshtakiwa wa tatu, Koplo Juma Mswa na wa tano, Konstebo Mataba Matiku zilimpata Kombe na kumuua papo hapo.

Baada ya mauaji, taarifa ilipelekwa kwa RCO Kilimanjaro na kumjulisha kuwa gari lililokuwa limeibwa limepatikana na mwizi hatari aliyekuwa nalo ameuawa.

Lakini, muda mfupi baada ya RCO kujulishwa hivyo, alipokea taarifa kwa simu kutoka kwa mtu aitwaye Iwisi Shoo akimtaarifu kuwa gari la Ladwa lililokuwa limeibwa Dar es Salaam bado halijapatikana na aliyeuawa si jambazi ni Luteni Jenerali Kombe.

Hapo ndipo askari wote watano na dereva walipokamatwa ambao ni Sajini Mensah na Koplo Mswa na dereva wa kiraia waliyetoka naye Dar es Salaam, Katembo na makachero Tarimo, Elinisafi na Matiku walipotiwa mbaroni.

Ushahidi wa mke

Roseleen Kombe ambaye ni mke wa Luteni Jenerali Kombe ambaye walikuwa pamoja kwenye gari, alitoa ushahidi na kueleza kuwa katika kipindi gari hilo la Ladwa linalofanana kwa rangi na lao lilipoibwa, walikuwa jijini Dar es Salaam.

Ni kutokana na mfanano huo wa rangi, gari lao lilitiliwa shaka na lilikakamatwa na Polisi jijini Dar es Salaam na baadaye kuthibitika silo na wakakabidhiwa gari lao.

Alisimulia mbele ya Jaji Chipeta kuwa Juni 30, 1996 alirejea Moshi na kumkuta mumewe nyumbani kwao kijiji cha Mailisita na ilipofika saa 10 alasiri, yeye na mumewe waliondoka nyumbani kutumia gari hiyo kuelekea Moshi.

Njiani walikuwa na miadi ya kukutana na mfanyakazi wao mpya, lakini baada ya kusafiri kwa kipindi fulani, aliona gari inayokuja mbele yao ikiwa na watu wanne.

Kabla ya kuwafikia, mumewe ambaye ndiye alikuwa akiendesha gari, alionyesha indiketa kuwa anaingia kushoto, lakini hawakwenda mbali sana ndipo aliposikia mlipuko wa bunduki na ziliendelea na moja ilimpata mumewe kwenye bega.

Kwa mujibu wa Roseleen, alimsikia mumewe akisema “Jiiii” na akamshauri watoke ndani ya gari na kukimbia, na kwamba yeye alitoka na kuanza kukimbia lakini katikati ya kukimbia, alianguka na kusimama tena kisha kuendelea kukimbia.

Roseleen aliiambia mahakama kuwa aliwasikia watu waliokuwa wakiwashambulia wakisema “Tena wako wawili”, na muda wote huo yeye na mumewe walikuwa wanaamini wamevamiwa na majambazi waliokuwa wanataka kuwapora gari.

Anaeleza kuwa yeye aliendelea kukimbia hadi alipofika kwenye nyumba fulani na kujificha nyuma ya gari lililoegeshwa hapo ambapo alikaa hapo hadi alipojiridhisha kuwa hali imetulia ndipo alipoamua kujitokeza kutoka mafichoni.

Alipotoka mafichoni alisikia watu wakisema “majambazi mengi, upoteze maisha kwa sababu ya gari,” hapo ndipo alibaini mumewe ameuawa.

Uchunguzi wa daktari ulibaini kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na matundu tisa ya risasi, manne yanatokana na risasi zilipoingilia na manne mahali zipotokea na risasi hizo zilimpata marehemu eneo la kifua na tumboni na kumuua papo hapo.

Kulingana na uchunguzi huo, wauaji walimshambulia katika umbali usiozidi mita 30 au chini ya hapo na hiyo pekee ilithibitisha kuwa kulikuwa na lengo la kumuua (intention) na risasi zote zilizoingia kwenye mwili zilitoka kupitia kwenye mifupa.

Pamoja na Roseleen Kombe, lakini upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi zaidi ya 15 ambao baada ya kufunga ushahidi wao, mahakama iliwaona washtakiwa watano walikuwa na kesi ya kujibu, ambapo walipanda kizimbani kujitetea.

Hii ni baada ya mshtakiwa wa sita, Ismail Katembo aliyekuwa dereva akiwaendesha washtakiwa ambao ni askari, kufariki dunia akiwa mahabusu.

Usikose simulizi hii inayoendelea kesho