Siku 1,448, kina Gugai walivyosota gerezani

Muktasari:

  • Baada ya kusota mahabusu kwa siku 1,448 tangu wafikishwe mahakamani, hatimaye aliyekuwa Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake wawili wameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


Dar es Salaam. Baada ya kusota mahabusu kwa siku 1,448 tangu wafikishwe mahakamani, hatimaye aliyekuwa Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake wawili wameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Gugai na wenzake, George Makaranga na Leonard Aloys walifikishwa mahakamani hapo Novemba 16, 2017 wakikabiliwa na mashtaka 43, ikiwamo kumiliki mali zenye thamani ya Sh3.6 bilioni kinyume na kipato chao halali.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambaye alisema kutokana na Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka, mahakama imeshindwa kuwatia hatiani, kwa hiyo watuhumiwa wote wapo huru.

Awali, katika kesi hiyo walikuwa washtakiwa wanne, lakini Oktoba 4, 2019, Yasini Katera alihukumiwa na mahakama hiyo kulipa faini ya Sh100 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukiri kosa katika shtaka la utakatishaji fedha lililokuwa likimkabili.

Katera alilipa faini ya Sh100 milioni huku mahakama hiyo ikitaifisha nyumba yake iliyokuwa kwenye kitalu namba 438 na 439.

Simba alisema katika kesi hiyo mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi walikuwa 42 na vielelezo zaidi ya 70.

Hakimu huyo alisema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 43 yaliyokuwa yamegawanywa katika makundi 3, kundi la kwanza kulikuwa na mali ambazo hazielezeki, pili la kughushi na tatu ni kujipatia mali nyingi kushinda uwezo wao.

Alisema katika shtaka la kujipatia mali ambazo hazielezeki, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulidai kuwa Gugai alikuwa na mali nyingi zinazoweza kumtia hatiani ambazo alianza kuziuza huku hati za nyumba alizokuwa nazo alighushi tangu mwaka 2013 hadi 2015.

Hakimu Mkuu Simba alisema ushahidi huo ulieleza kuwa nyumba hizo ziliuzwa mwaka 2016, lakini walishindwa kumleta mahakamani wakili Beatus Malina ili athibitishe ndiye aliyesimamia uuzaji huo

“Kwa nini hawakumleta wakili ili aweze kuthibitisha, hivyo kutokana na hilo, shtaka halina nguvu na halijathibitika,” alisema Simba.

Alisema mashtaka ya kugushi uthibitisho waliotoa upande wa mashtaka waliuchukua kwenye kompyuta lakini ulishindwa kuangalia huyo Gugai kabla hajaanza kazi alikuwa anajishughulisha na nini na alikuwa na mali zenye thamani gani.

Alisema kutoka na mashtaka yote mawili hayana uthibitisho hivyo shtaka la kujipatia mali kushindwa uwezo wake moja wa moja shtaka halijathibitika.