Shule 10 Ilagala hazina madawati

Muktasari:
Akitoa taarifa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ilagala juzi, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilagala, Mwita Mwitiba alisema upungufu huo wa madawati unasababishwa na wananchi ambao hawakushiriki vyema kutengeneza madawati.
Kigoma. Shule 10 za msingi katika Kata ya Ilagala Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, zinakabiliwa na upungufu wa madawati hali inayosababisha wanafunzi kusoma wamekaa sakafuni, kwenye miti na mawe.
Akitoa taarifa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ilagala juzi, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilagala, Mwita Mwitiba alisema upungufu huo wa madawati unasababishwa na wananchi ambao hawakushiriki vyema kutengeneza madawati.
Alisema hadi sasa kuna madawati 968 kati ya 2,344 yaliyokuwa yanahitajika kwa shule hizo, hivyo upungufu uliopo ni madawati 1,376.
Diwani wa Ilagala, Kafunya Kassim Kafunya alisema ili kupunguza changamoto hiyo, madawati 124 yametengenezwa na mafundi kutoka Gereza la Ilagala.
Aliwaomba viongozi kuhamasisha wananchi waweze kukamilisha utengenezaji wa madawati kwa kuomba vibali vya kuchana mbao na kupeleka kwa mafundi wa Gereza la Ilagala.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ilagala, Jumanne Kisiki alisema baadhi ya wakazi kijijini hapo walisusa kuchangia madawati wakisema Serikali imetangaza elimu ni bure.