Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shivji ataka Bunge kubatilisha azimio mkataba bandari

Muktasari:

  • Mwanazuoni Profesa Issa Shivji amekosoa mkataba baina ya Tanzania na Dubai unaohusu uboreshaji na uendeshaji wa bandari, huku akishauri Bunge kubatilisha azimio la kuridhia mkataba huo wa awali.

Dar es Salaam. Mwanazuoni Profesa Issa Shivji amekosoa mkataba baina ya Tanzania na Dubai unaohusu uboreshaji na uendeshaji wa bandari, huku akishauri Bunge kubatilisha azimio la kuridhia mkataba huo wa awali.

Profesa huyo ambaye ni nguli wa sheria amependekeza njia hiyo leo Jumatano Juni 28, 2023 wakati akizungumza kwenye mjadala uliokuwa na mada isemayo: “Njia kuu za uchumi na tafakuri ya mkataba wa mahusiano ya kijamii na kiuchumi kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.”

Mwanazuoni huyo amedai njia zilizochukuliwa na wadau wengine ikiwemo kwenda mahakamani, hazitasaidia kuondokana na sintofahamu iliyopo hivi sasa kuhusu mkataba huo ambao mjadala wake unazidi kupamba moto kila kukicha.

Katika mchango wake, Profesa Shivji amesema zipo njia nyingi zilizopendekezwa baadhi ya wadau wakiwemo viongozi wastaafu na watalaamu wa sheria, lakini kwa maoni yake hadhani kama zitasaidia Taifa kutoka katika sintofahamu hiyo, kwa madai kuwa Bunge limesharidhia mchakato huo.

“Haiwezekani hata kurekebisha vifungu kwa aina ya mkataba huo. Kuna wengine wanakwenda mahakamani, lakini kama mnavyojua mahakama zetu zinachukua muda mrefu kusikiliza kesi,” amesema Profesa Shivji.

Mjadala huo ambao uliandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), ndaki ya Sayansi ya Jamii, ulishirikisha wasomi na wadau mbalimbali ambapo walipa fursa ya kutoa maoni yao juu ya mada hiyo ambayo bado imeendelea kuwa gumzo.

Oktoba 25 mwaka 2022 Serikali ya Tanzania na Dubai ziliingia makubaliano katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari na uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Hatua hiyo imebua mjadala na kuwagawa baadhi ya wadau na vigogo wakiwemo viongozi wastaafu wa zamani. Wapo wanaounga mkono hatua ya Serikali huku wengine wakipinga mchakato huo wakidai hauna manufaa kwa Taifa, lakini kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikisisitiza manufaa ya suala hilo.

Juni 25, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alishauri kuangaliwa upya kwa vifungu vyenye mkanganyiko katika mkataba huo. Alisema ni kweli uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam haukuwa wa kuridhisha kwa muda mrefu, lakini makubaliano yaliyopo yana vipengele vinavyoleta wasiwasi.

Wakati Jaji Warioba akitoa ushauri huo jana Jumanne, kundi la mawakili wanne wa kujitegemea wakiongozwa na Alphonce Lusako walikwenda mahakamani kupinga mkataba huo.

Lakini leo Profesa Shivji amehoji,”hata ukiingia mahakamani utachallange nini? Utakuwa una challenge azimio la Bunge sio makubaliano yaliyoingiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai,” amesema Profesa Shivji.

Mawazo ya Profesa Shivji hayana tofauti na mwanasheria mwingine Tundu Lissu ambaye hivi karibuni alisema haona haja kwenda mahakama kupinga mchakato huo, kulingana na mkataba wenyewe ulivyo.

Profesa Shivji amesema njia ya pekee ni Bunge kuketi upya na kusema kwamba baada ya  maoni ya wananchi wameona na azimio walilolipitisha halikuwa sahihi, hivyo wanaazimia kulifuta, akisema jambo hilo linawezekana.