Shirika la Uvuvi laiangukia Serikali changamoto zake

Kaimu Mtendaji Mkuu Tafico, Ahmed Byabato akisoma ripoti ya utendaji wa shirika hilo pamoja na changamoto wakati wa uzinduzi wa baraza la wafanyakazi wa Tafico ofisi za Kigamboni. Picha na Sute Kamwelwe.
Muktasari:
- Uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la Shirika la Uvuvi umefanyika leo Aprili 8, 2025
Dar es Salaam. Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico), limesema kutokuwepo kwa bodi ya shirika, upungufu wa watumishi, mitaji ya uendeshaji miradi ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili shirika hilo.
Pia, kukosekana kwa wenye ujuzi wa uendeshaji meli za uvuvi za bahari kuu, madeni ya watumishi, watoa huduma na ukosefu wa fedha za kuendeshea meli itakayokamilika Novemba 2025.
Changamoto hizo zimesomwa mbele ya mwakilishi wa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Daudi Mayeji, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kwenye uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la Tafico lenye wajumbe 24.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumanne Aprili 8, 2025 katika ofisi za shirika hilo, Kigamboni Dar es Salaam huku ukihudhuriwa na sekretarieti na wafanyakazi wa Tafico.
Akizisoma changamoto hizo, Kaimu Mtendaji Mkuu Tafico, Ahmed Byabato amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 shirika linaiomba Serikali lipate Sh4.8 bilioni kama fedha za maendeleo zitakazotumika ikiwamo kuendeshea meli za uvuvi wa bahari kuu.
“Fedha za maendeleo zitatumika katika ukarabati wa ghala la ubaridi kuhifadhia mazao ya uvuvi, kuendeshea meli ya uvuvi wa bahari kuu na kiwanda cha barafu,” amesema.
Ameongeza utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza mapato ya shirika, uzalishaji samaki, morali ya utendaji kazi, ajira na lishe bora kwa Watanzania kwa kupunguza udumavu hatimaye ustawi wa jamii na uchumi.
Akielezea changamoto hizo, Mayeji ambaye ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathimini Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema kwa kuwa shirika lilikuwa limekufa na sasa linafufuliwa, hivyo Serikali inaendelea kuongeza wafanyakazi.
“Kila mwaka Serikali inatenga fedha kuongeza watumishi na hata mwaka unaokuja inatarajiwa kuongeza watumishi. Meli moja imeshanunuliwa na mbili ziko hatua za mwisho za manunuzi.”
Amesema hayo yote yatahitaji wafanyakazi zaidi. Tutaanza kupata mazao ya uvuvi ambayo kwa sasa hatuyapati, kufanya hivyo kutaongeza mapato na shirika litaanza kujitegemea lenyewe.
Mayeji ambaye amemwakilisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema sekta ya uvuvi itakuwa na mchango mkubwa kwa Taifa.
Aidha amelitaka shirika kuendelea kufanya kazi kazi kwa bidi, ubunifu na maarifa ili kuongezea tija shirika kujiendesha kibiashara.
Kuhusu umuhimu wa baraza la wafanyakazi katika kuongeza ufanisi wa shirika, Byabato amesema Serikali inahimiza utawala bora, hivyo kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake.
Amesema kupitia baraza hilo watashirikishwa watumishi katika maeneo yote kupitia chombo hicho kilichopo kwa mujibu wa sheria.
“Tutapokea mawazo, michango mbalimbali ya watumishi katika kufanya uamuzi wa shirika. Baraza hili litasaidia kupata michango ya pamoja ya watumishi wetu,” amesema Byabato.
Aidha, Mkurugenzi Mayeji amesema baraza hilo ni kiungo cha watumishi na
daraja litakalounganisha maoni na mependekezo ya watumishi na menejimenti ili yatakayotekelezwa yawe ya uwazi na makubaliano ya pamoja.
“Sasa shirika litakuwa na ushirikishwaji mpana, mkataba umesainiwa baina ya wafanyakazi, menejimenti na idara ya kazi, kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa shirika hili katika utendaji kazi,” amesema.
Amesema wafanyakazi watawasilisha maoni yao juu ya namna gani shirika liweze kwenda.
Hali ya Shirika kwa sasa
Akizungumzia hali ya Tafico kwa sasa Byabato, amesema shirika limeendelea kupokea mashine za kuzalisha barafu, magari ya ubaridi na sasa linatarajia kupokea meli ya uvuvi wa bahari kuu.
“Kupitia miradi ya maendeleo kuna maghala ya ubaridi, viwanda vya kuchakata samaki, viwanda vya kuzalisha barafu na sasa tunaendelea na ukarabati wa gati kuegesha meli za uvuvi hapa Ras ya Mkwavi na Kilwa kuna ujenzi wa bandari ya uvuvi,” amebainisha.